KUISIKIA SAUTI YA ROHO MTAKATIFU.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 2, 2017
- 5 min read

Na Mch.Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
Kuna namna ambayo Mungu anasema nasi hata sasa kwa njia ya Roho mtakatifu. Husema nasi mara moja hata mara mbili,kusudi tuweze kumsikia vizuri;lakini ikiwa tumekataa kusikia basi Yeye hunyamaza kwa kuwa Mungu wetu sio dikteta. Roho mtakatifu ana sauti kabisa inayoweza kusema na wewe lakini inategemea umekaa mkao gani kwake. “Kukaa mkao” ni ile hali ya mahusiano uliyonayo na Yeye,ikiwa una mahusiano mazuri tena ya karibu basi uwe na uhakika atazungumza na wewe mambo mengi.
Roho mtakatifu ana utaratibu mzuri wa kuhakikisha anasema na wewe mambo kadha wa kadha ikiwa kama umekaza kumuelekea Mungu na U mtii mbele za Mungu. Mojawapo ya utaratibu ambao Roho mtakatifu anautumia kusema na wewe ni kwa njia ya kiongozi wako wa kiroho mahali ulipo. Kumbuka jambo hilo,kwamba sauti ya kiongozi wako wa kiroho ni sauti ya Mungu,na ndio sauti ya Roho wa Bwana. Tunaweza tukajifunza jambo hili katika mapana yake tukimuangalia Samweli.
Biblia inatueleza vizuri juu ya Samweli tangu alipokuwa mtoto akiwa amewekwa wakfu kwa Bwana. Samweli alikuwa chini ya baba yake wa kiroho,kuhani Eli. Hivyo Samweli alikuwa akichungwa chini ya baba wa kiroho kama ulivyo wewe unayechungwa chini ya baba/mama yako wa kiroho. Ingawa neno la Mungu kipindi kile lilikuwa hafifu na hapakuwa na mafunuo mengi kama katika agano jipya kipindi cha Roho,lakini bado Mungu alikuwa akizungumza na watu wake.
“ basi, wakati huo BWANA akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.” 1 Samweli 3:4-5
BWANA alimuita Samweli mara tatu “ Samweli! Samweli!” Lakini Samweli alimuendea Eli kuhani (baba yake wa kiroho). Ingawa Samweli alikuwa hamjui BWANA bado,na neno la BWANA lilikuwa halijafunuliwa kwake;lakini Sauti aliyoisikia aliisikia sauti kama ya Eli,na ndio maana akawa akimuendea Eli na kumuuliza baba uliniita? Lakini kumbe baba yake Eli hakumuita kabisa!
Samweli anamshangaa Eli babaye,kwamba “mbona nasikia sauti yake kabisa lakini yeye anasema sio yeye aliyeniita? Inakuwaje jambo hili!!!” Sauti ya Mungu iliingia masikioni mwa Samweli kwa mfano wa sauti ya Eli,na ikamchanganya Samweli kabisa. Huu ulikuwa ni moja ya utaratibu wake Roho mtakatifu kukufundisha kwamba,Yeye Roho wakati mwingi husema na wewe kwa kinywa cha baba yako wa kiroho. Sasa ikiwa hutamsikiliza baba yako wa kiroho,hii itakuwa ni sawa na kukataa sauti ya Mungu.
Ukiwa chini ya baba/mama wa kiroho basi ni lazima utambue kwamba huyo kiongozi wako amebeba sauti ya Roho mtakatifu kwa ajili yako,Sasa jiulize maswali haya;
Je ni mara ngapi unapuuzia sauti ya baba/mama yako wa kiroho? Mfano anakuambia wahi kwenye ibada lakini umekuwa mchelewaji namba moja! Mfano anakuambia utoe sadaka iliyo njema pamoja na uwe mwaminifu kulipa fungu la kumi lakini hufanyi hata moja alafu wala huogopi ukijua si mchungaji kasema bhana! Au mfano baba/mama yako anakuagiza jambo fulani lakini hutaki kufanya! Au ni mara ngapi unamsema vibaya huko nje baba/mama yako wa kiroho ? Hujui kwamba humsemi mwanadamu bali Mungu aliyemuweka? Wewe u nani unayesema mapotovu juu ya sauti ya Mungu katika kinywa cha baba/mama yako wa kiroho? N.K
Sasa leo wengi wamefungwa na laana kwa sababu ya kutoisikia sauti ya Mungu kwa vinywa vya wazazi wao wa kiroho. Inawezekana kweli baba/mama wa kiroho akawa na mapungufu falani kama mwanadamu wa kawaida lakini mapungufu yao yasikufunge katika kuisikia sauti ya Mungu; Kumbuka kila mtu ana mapungufu yake kwa sehemu,lakini pungufu la kibinadamu bado ni la kibinadamu tu;Mungu bado ataendelea kusema katika hayo mapungufu.
Jambo moja la kujifunza kwako ni kuweza kuisikia sauti ya Mungu kwa sauti ya mchungaji wako. Yeye Roho mtakatifu mara nyingi huwatumia vingozi wako wa kiroho kwa maana wao ndio wamepewa dhamana na Mungu kusimama mbele yako.
Kuisikia sauti ya Roho mtakatifu sio kazi ndogo,kwa kuwa ni wale tu walio na mahusiano mazuri na Mungu kwanza wameoshwa kwa damu ya Yesu,tena ni wale walijikana nafsi zao kwa ajili ya Bwana;na tena ni watiifu kwa wachungaji wao; Watu wa namna hiyo wamepewa neema ya kumsikia Roho. Lakini,tujifunze kiundani kwa kupitia mtume Paulo,Yeye aliyekuwa akiongozwa na Roho mtakatifu muda wote wa utumishi wake.
Paulo mtume alitumwa kwa mataifa kuwapelekea injili,na alipokwisha kuagizwa juu ya injili aliyokuwa nayo,BWANA akamtuma akimwambia atoke Yerusalemu upesi,kwa sababu hawatakubali ushuhuda wake Paulo katika habari za Yesu. Hivyo Bwana kwa njia ya Roho mtakatifu akamuagiza aenende kwa mataifa ( maana Petro alipewa injili kwa waliotahiriwa,Yerusalemu bali Paulo kwa mataifa) ( Matendo 22:17-21)
Lakini kwa kuwa Paulo aliazimia kwenda Yerusalemu,hali akijua ya kwamba Bwana amemwambia husiende Yerusalemu. Paulo alipozidi kufuliza katika nia yake,basi Roho mtakatifu alisema naye kwa namna tofauti tofauti. Na ndivyo ilivyo hata sasa;ikiwa Mungu anasema nawe kwa mara moja na husikii,basi hutumia njia nyingine kusema nawe,lah! Ukiwa tena husikii basi ujue Roho atajaribu kusema nawe kwa njia ya kawaida inayoonekana katika mwili kusudi sasa uelewe. Kusudi lake akuokoe na hatari iliyopo mbele zako.
Bwana akasema na Paulo (Matendo 22:17-18),lakini ikawa Paulo akataka kwende alikoambiwa asiende,Roho akajaribu njia nyingine kupeleka sauti yake kwamba Huko Yerusalemu kuna vifungo na dhiki yamngoja,na kwa kuwa alikaza sana kwenda Yerusalemu;Roho akamfunga asijue mambo yatakayomkuta ( Matendo 20:22). Walipoendelea mbele katika safari yao,Roho mtakatifu kwa rehema na upendo mkuu anajidhihirisha jambo lile lile,kwamba Paulo asipande kwenda Yerusalemu (Matendo 21:4).
Katika huo mstari wa nne,Paulo sasa anaambiwa na wanafunzi wake kwa uweza wa Roho mtakatifu tena.Na kwa kuwa akazidi kukaza kwenda Yerusalemu,Roho mtakatifu akajaribu kusema nae katika njia ya kawaida sana ili aweze kuelewa kile ambacho Roho anasema. Roho mtakatifu akaweka sauti yake kwa nabii mmoja anaeitwa Agabo,biblia inasema;
“ Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.” Matendo 21:10-11
Paulo alipokataa shauri hilo,basi ilibidi wote wanyamaze,kisha mapenzi ya Mungu na yatendeke. Ukiendelea kusoma Matendo 21 na sura 22 utaona kweli kabisa,Paulo akiingia Yerusalemu naye akikamatwa na kupata mateso na vifungo. Kwa Paulo ilikuwa ni mpango wa Mungu,kwamba mapenzi ya Mungu yatendeke katika hali ya kukaza kupanda Yerusalemu ingawa alionywa kwa sauti ya Roho mtakatifu.
Leo sasa,wengi hujikuta wakiangukia katika makosa ya kutomsikiliza Roho mtakatifu,utakuta Roho kakuambia usipite pale lakini wewe unapita. Au utakuta Roho kakuzuilia kuolewa na fulani lakini kwa sababu unampenda na anapesa basi unaolewa nae,angalia utapata shida kwa kushindwa kuisikia sauti ya Roho mtakatifu. Au utakuta Roho anakushuhudia usiibe mke wa jirani yako,lakini unaipuuzia sauti hiyo na hatimaye unadondokea dhambini,angalia utakuja kufa!!Yapo mengi ambayo Roho mtakatifu anatuzuilia lakini kwa sababu ya jeuri yetu tunayafanya na hatimaye tunajikuta tukipata maumivu mengi. Kwa nini usiisikize sauti ya Roho mtakatifu?
Angalia;
Kuna kipindi ambapo Roho wa Bwana anakuamsha usiku ili uombe kwa kuwa kuna hatari fulani imepangwa juu yako,au juu ya familia au juu ya kanisa na watu wako wa karibu,lakini ni mara ngapi unapoamshwa usiku kiasi kwamba usingizi unakata kabisa,sasa mara ngapi ukiamshwa na unapotezea hiyo? Jiulize;ni mara ngapi unadiriki hata kutumia muda huo wa usiku katika kuwaza maovu,badala ya kuomba kama vile Roho alivyosema na wewe kwa kuukata usingizi wako!!
Wengine wakiamshwa usiku waombe ndio uchukua smart phones zao na kuanza kutafuta mtu aliyepo online waanze kuchati mambo yakipuuzi mpaka asubuhi. Wewe hujui kwamba huyo ni Roho mtakatifu anataka uongee naye akupe mafunuo juu ya mambo yako mengi yaliyofungwa. Sasa jifunze sana jinsi ya kuisikia sauti ya Roho mtakatifu ili uweze kuvuka zaidi hapo ulipo.
Kwa msaada zaidi,piga sasa kwa;
+255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch.GasperMadumla
UBARIKIWE.
Comments