KUFANYIKA NURU YA ULIMWENGU.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 14, 2017
- 5 min read

Na Mch.G.Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
>Tafsiri nyepesi ya neno nuru ni aina ya mwangaza ulio mpana wenye nguvu ya kumulika mbali zaidi. Ndani ya nuru giza halina nafasi,kwa maana panapo nuru giza hukimbia. Hata hivyo kwa mujibu wa biblia neno “nuru” limepewa maana zifuatazo;
Nuru ni mwangaza mkali (Matendo 22:6)
Nuru ni Yesu Kristo (Yoh.9:5)
Nuru ni matendo mema yanayompendeza Mungu na kumpa utukufu
Katika umbaji wa mbingu na nchi , siku ya kwanza Mungu aliumba “nuru“ashughulikie tatizo la giza,ukiwa pamoja na utupu. Na ndivyo ilivyo hata sasa,ukitaka kupambana na giza,utupu na ukiwa unahitaji nuru kwanza.Hivyo basi nuru ni muhimu sana kwenye maisha yako. Kwa sababu nuru ni njema machoni pa Mungu. ( Mwanzo 1:1-5 ).
Kwa kuwa nuru ni njema machoni pa Mungu,ndio maana biblia inasema “ Mungu amejivika Nuru kama vazi…“Zab.104:2)
Dhambi ilipoingia ulimwenguni,ikaleta giza ndani ya mtu na mwanadamu akapotea kwa kuwa kwenye giza ndipo mtu hupotea. Kumbuka hilo kwamba kwenye giza ndipo mtu hupotea.
Mtu mmoja alijaribu kufnya utafiti kuona jinsi ambavyo mtu anaweza akapotelea dhambini,hivyo mtu huyo akakusanya watu wa kila lika wakubwa na wadogo,kisha akawaleta mahali pamoja kwenye ukumbi mkubwa. Ikawa kama sherehe fulani,na ndani ya sherehe aliwawekea vinywaji vya namna mbali mbali isipokuwa hakuweka pombe kwa sababu jamii ya watu waliokusanywa walikuwa ni wapendwa ( Wameokoka).
Naye akajitenga chumba cha ndani ambapo alikuwa akiona na kusikia yote yaliyokuwa yakiendelea ukumbini. Akaanza zoezi la kuandika matokeo ya dakika za mbili za mwanzo wakati watu wanaburudika kwa vinywaji.
Sasa,akazima taa kwa dakika mbili hivi,akasikia ukimya umetawala ukumbini naye akaandika tokeo hilo la ukimya. Akaongeza dakika mbili nyingine gafula akaanza kusikia minongono fulani hivi ikianza kwa utaratibu… akaandika tokeo la pili. Akaongeza muda wa giza kwenye ukumbi,na sasa ukumbi ukawa umechangamka kana kwamba kuna taa vile kwa maana watu sasa wameshalizoelea giza,naye akaandika tukio hilo la tatu.
Akasema ngoja aone tukio la mwisho litakuwaje,sasa akaamua kuwasha taa kwa gafula naye akachungulia ukumbini; La haula!!! Akastajaabu mambo aliyoyaona!!! Kwa maana watu aliokuwa akiwaamini aliwakuta kwanza wameama kwenye siti zao za awali na akawakuta wengine wapo juu ya meza wakicheza,wengine wapo uvunguni dah! Kwa sababu giza liliwaficha kwa hiyo wakafanya mambo ya aibu! Naye akaandika tokeo hilo la ajabu! Na ndipo nami nikagundua kwamba;
Maovu yanafanyika gizani ( Wachawi,waalifu n.k wanalipenda giza)
Giza linapoingia,kwanza mtu huwa na hofu fulani,lakini giza linapoendelea kwa muda taratibu mtu huanza kulizoelea na linapozidi hulipenda tena na kuanza kuichukia nuru.
“ Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.” Yoh.3:20
Hivyo basi;dhambi ikaleta giza ulimwenguni,~ kumbuka katika uumbaji nchi ilikuwa na giza,na Mungu akatuma nuru kushughulikia giza,nayo nuru ikashuka. Unganisha na andiko hili;Yohana 3:16
“ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Ukichunguza kwa makini andiko hilo ni sawa na kusema ~ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akaitoa nuru ya pekee ili kila aipokeaye asipotee (gizani), bali awe na uzima wa milele.
YESU KRISTO ndiye nuru ya pekee. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.” Yoh.12:46
Na ndio maana Bwana Yesu alipomtokea Sauli alijidhihirisha ndani ya nuru,kama ishara ya kipekee.Na sauli alipoiona ishara hiyo pamoja na kuisikia na sauti gafula akatambua ya kwamba ni Bwana. ( Matendo 9;3-5, 22:6-7)
Hivyo basi ikiwa Yesu ndiye nuru,nawe umempokea Yesu,hii ni sawa na kusema umeipokea nuru. Mfano mwesi ni huu,ikiwa mimi nimeshika torch yenye kuwaka,nikikupa hiyo torch iwakayo basi ni dhahili utakapoichukua torch hiyo itaendelea kuwaka mahali ulipo kwa kuwa umeipokea ikiwa anawaka kutoka kwangu.
Na ndivyo ilivyo,ukiwa umempokea Yesu,umeipokea nuru moyoni mwako na hiyo nuru yatakiwa kuangaza mahali ulipo ili watu wakikuona wewe waione nuru ikiwaka. Na ndio maana imeandikwa;
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Mathayo 5:14-16,Soma pia Waefeso 5:8-9
Wapaswa kuwa nuru ya ulimwengu,watu wakikutazama wamuone Mungu ndani yako. Tena watu wakikutazama waione sura ya Yesu ndani yako. Mahali ulipo uwe nuru
Kumbuka matendo yako yana nguvu kuliko maneno. Injili ya kweli inaanzia katika matendo mema. Kabla ya kusema,matendo yako yaseme kwanza kwamba jinsi unavyoenenda Mungu ainuliwe na atukuzwe kwa jinsi tu ulivyo. Mtazame Petro mtu ambaye mwenendo wake alijulikanani mwanafunzi wa Yesu.
Sasa jiulize mwenendo wako unakutambulisha kuwa nani? Je watu wanaweza kumuona Mungu wa kweli kupitia matendo yako? Je mahali unapoishi watu wanakushuhudiaje?
Kwa maana kuna watu ni wapendwa lakini ukiambiwa kwamba ni wapendwa utakataa jinsi walivyo kimatendo!!! Wengine kwa matendo yao wamejikuta wakiwazuilia wengine kuokoka kwa sababu Mungu atukuzwi katika matendo yao. Mpendwa ukristo ni kuishi kama Kristo alivyo. Ndani ya Kristo Mungu anaonenaka,Je ndani yako wewe Mungu anaonekana?
Huwezi kuwa nuru kwa maneno tu,bali matendo kwanza. Ndio maana mafarisayo hawakuweza kuwa nuru kwa sababu ya matendo yao hali waliishika torati. (Mathayo 23:1-3)
Ukiwa nuru,watu wataiona hiyo nuru pasipo hata kuwaambia kwamba wewe ni nuru. Mfano ; Siku moja nilipokuwa nikiwa kwenye dala dala iliyokuwa imejaza kweli kweli. Gafula mtu mmoja aliyekuwa amekaa nyuma akashuka nami nikaketi pale aliposimama. Si unajua kwenye dala dala ukisimama mwenzako anaketi!
Aliposimama akashuka maana bus limesimama kituoni,lilipoondoka akapanda tena inaonekana kana kwamba alikuwa akichukua kitu fulani hapo chini au alikuwa amechanganya kituo. Sasa,akaomba apite kule nyumba alipokuwa ameketi nami ndipo nilipoketi. Akanifikia na kunitaka nisimame akiongea katika lugha isiyo nzuri,lakini mimi nilikaa kimya baadae nikampisha akae naye,akaniambi “basi sitaki tena” baadae akashuka moja kwa moja.
Sasa watu wakaanza kumsema kwa tabia yake mbaya,wakawa wakiniangalia mtu ambaye nilipewa maneno machafu pasipo kurudisha!,gafula mama mmoja aliyekuwa ameketi mkono wangu wa kushoto akaniuliza “unasali kanisa gani?“.
Angalia hapo,mama huyo aliniuliza hivyo baada ya kuona matendo yangu mema;hivyo matendo (nuru) ikiwa imekwisha hubiri kabla ya mimi kusema kitu.
Nuru inafanya kazi zifuatazo;
Kuangaza gizani (Yohana 1:5 ~[5]Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Ni muhimu kujua ya kwamba,ukiwa nuru,basi uwe na uhakika giza litakimbia lenyewe. Huna sababu ya kulikimbiza giza,bali giza litakimbia lenyewe. Mfano ukiwa na mahusiano mabaya na marafiki ulio nao,ili uweze kuepukana nao,unahitaji kwanza wewe uwe nuru,ili wao wakimbie wenyewe kwa maana hakuna urafiki kati ya nuru na giza.
Kuona vitu au mambo yaliyofichika kwa haraka na wepesi. (Yoh.8:4-6 Yesu akitegwa na kujaribiwa,lakini kwa kuwa Yeye alikuwa nuru aliona huo mtego kwa haraka na kwa wepesi)
Kumtangaza Kristo katika matendo yako ( Mathayo 5:16)
Nuru hutusaidia kutokujikwaa gizani. YOH. 11:9
Je ninawezaje kuwa nuru?
Mpokee Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yako. Maana Yeye ndio nuru,ukimpokea Yeye ni sawa na kuipokea nuru.( Yoh.9:5)
Kudumu katika neno – Wanafunzi wa Yesu walidumu katika neno, Matendo 2:46. Hatua hii ni muhimu sana kwa maana giza lililopokuwa katika Mwanzo 1:1-3 Mungu alitamka NENO kwanza ndipo nuru ikawa. Lile neno ndio kisababisho cha nuru. Hivyo unahitaji kuketi sana katika neno sahihi la Kristo,neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yako (Wakolosai 3:16)
Kumpa nafasi Roho mtakatifu, akuongoze atakavyo Yeye.
Faida za kuwa nuru ya ulimwengu;
Kuzaa matunda kwa wepesi.( Ukiwa nuru halisi ya Kristo,utapata wepesi wa kuwalet watu wengi kwa Kristo kwa sababu maisha yako ni injili tosha kabla ya kuwahubiri)
Kupata ujasiri wa kukemea dhambi- Ukiwa nuru,utafaulu kukemea dhambi kwa kiwango kikubwa kwa maana wewe u safi. Utakuwa na ujasiri kama aliokuwa nao Yohana mbatizaji,ambaye hakumuogopa mtenda mabaya bali alimwambia. Yoh.mbatizaji alimwambia Herode kwamba amefanya vibaya kumoa mke wa nduguye Filipo ( Mathayo 14:3-5)
Hasara za kuishi maisha ya ki-Kristo bila kufanyika nuru halisi;
Kuishi maisha ya unafiki kama mafarisayo na waandishi (Mathayo 23:1-3)
Uwezekano mkubwa wa kuikosa mbingu. Kwa sababu ikiwa kama utaishi katika hali ya unafiki,waweza kuikosa mbingu na ukristo wako ukawa ni bure.!!
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
ch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments