KUCHUKULIANA KATIKA UPENDO.
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 2, 2018
- 4 min read
Updated: Sep 5, 2022

Na Mch Gasper Madumla.
Siku moja nilikuwa harusini,na ikafika wakati wa nasaha za wazazi wa maharusi. Akaanza kuzungumza baba wa bwana harusi kisha akamaliza,kisha akaja mzazi wa bibi harusi naye akazungumza. Mojawapo ya mazungumzo ya mzazi wa bibi harusi yalikuwa ni haya “ …mwanangu,sasa umekuwa na mmeshafunga ndoa takatifu…. nakuomba ukienda nyumbani kwa kina mumeo,ukiona wao wakilala wanageukia kulia,nawe lala ukigeukia kulia huko huko,ufanye kama wafanyavyo.…”
Unajua kitu gani alikuwa akimwambia,? Alikuwa akimuhasa mwanaye kujaribu kuendana na mazingira mageni ya watu wa mumewe. Ni sawa na kumwambia binti aweze kuchukuliana na mazingira ya mumewe. Ikiwa ndivyo basi ni lazima huyo binti akubali kushuka hata kama alikuwa na elimu ya juu lakini sasa ndio kaolewa na mtu ambaye kwao kijijini wanalalia mkeka ndani ya kijumba cha manyasi! Naye hana budi kujishusha,na kuchukuliana nao katika hali hiyo hiyo aliyoikuta. Hivyo ; huo ni mfano wa kawaida tu,ebu tuangalie maana neno hili “kuchukuliana”
“Kuchukuliana” ni hali ya kumvumilia mwenzako juu ya tabia au mwenendo mbaya aliokuwa nao kisha kukubali kuishi / kukaa naye pasipo kuhesabu udhaifu wake kwa lengo la kumlekebisha hata amjue Mungu wa kweli.
“ kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;” Waefeso 4:2
Hali ya kuchukuliana inategemea kiwango chako cha“unyenyekevu,uvumilivu pamoja na pendo” juu ya yule unamchukulia. Kwa sababu ni vigumu kumchukulia mtu yeyote ikiwa huna hali ya unyenyekevu,uvumilivu pamoja na pendo. Mfano ukiwa na mtu ambaye kwa kweli ni msumbufu kwa tabia au mwenendo wake nawe unahitaji uchukuliane naye,kwanza utahitajika ujishushe wewe mwenyewe(unyenyekevu)na kujaribu kufanana naye ingawa wewe ni mtu wa viwango vingine,kisha uwe na uvumilivu kwamba ukubali kumvumilia katika madhaifu yake huku ukionesha upo naye ijapokuwa anaweza akawa akiendelea kukuumiza kwa tabia yake. Kwa lengo moja tu,kumfanya huyo mtu amgeukie Mungu.
Kuna wakati mwingine unatakiwa ujifanye kana kwamba ni mjinga kwa mjinga ili umpate huyo mjinga amuelekee Bwana -( 1 Wakorintho 9:19-22). Usipofanya hivyo ujue huwezi ukamrejesha huyo vizuri. Ebu angalia,mfano mtu huyo ni mwenzi wako wa ndoa ambaye kusema ukweli anakera sana kwa tabia yake,nawe ulikwisha tumia mbinu tofauti tofauti za kumrekebisha lakini mpaka sasa hakuna badiliko lolote,sasa ufahamu ya kwamba ikiwa utajifunza namna ya kupuuzia mambo yake kana kwamba hawakusumbui huku ukimuombea ujue atabadilika tu,hata kama itachukua muda kwa sababu hakuna tabia au jambo gumu kwa Bwana.
Kitu cha kwanza na muhimu ni wewe mwenyewe kukubali kuchukuliana naye kwa kujishusha (kutoangalia thamani yako jinsi ulivyo) kwa lengo la kumleta katika wokovu. Tabia ya kuchukuliana ni tabia ya Mungu mwenyewe,Yeye Bwana alichukuliana nasi katika udhaifu tulionao kwa kiasi kikubwa sana na hata sasa amekuwa Mungu mwenye kuchukuliana nasi katika Pendo (maana yeye ni Pendo),hivyo kama alivyo Mungu nasi tunapaswa kuwa.
Si rahisi kumchukulia mtu ambaye kwako ni msumbufu,lakini inawezekana ukamchukulia vile alivyo kwa lengo la kumfanya aokoke na kumjua Mungu wa kweli.
“Kuchukuliana“kunahitaji uvumilivu wa hali ya juu na ndio maana utaona watu waliokosa uvumilivu hawakuweza kuchukuliana,bali waliwaacha wenye udhaifu waangamie kwenye udhaifu wao. Lakini ebu jiulize leo,ni kweli Mungu anapendezwa kuona watu wake wakiangamia kwa sababu wamekosa msaada? Utagundua kwamba Mungu hapendezwi na hali hiyo,bali hupenda kutuona tukibebeana mizigo,tukisaidiana kwa maombi,hali na mali!
Jambo moja muhimu unapohitaji kumchukulia mwenzako juu ya tabia yake ni kumuombea bila kukata tamaa huku ukimuonesha upendo kana kwamba hakusumbui kwa lolote lile.
Ukifanya hivyo ujue mtu huyo atabadilika tu hata kama tabia yake ikoje,kumbuka MUNGU ni muweza wa vyote katika vyote. Unajua huu ndio wakati maalumu wa kupambana na mwanzako ili Bwana ambadirishe,inawezekana!
Omba Mungu aongeze upendo wako kwake ili kweli umpende Yeye kwa moyo wako wote,kwa roho yako yote,kwa nguvu zako zote,na kwa akili zako zote. Kisha endelea kuomba pendo la Mungu likae zaidi ndani yako,na hapo itakuwa rahisi kuchukuliana na watu katika pendo. Ukiwa mtu uwezaye kuchukuliana na watu wa aina zote,hakika huyo ndiye mkristo halisi huku akiwaombea hao watu wasiookoka waokoke.
Leo kuna shida hii kwetu sisi wapendwa,shida ya kushindwa kuchukuliana mizigo ipasavyo! Yaani imefika wakati watu wa dunia wanatushinda maana utakuta wapendwa hawaelewani wao kwa wao,wakati mwingine hawasaidiani kwa kushindwa kuchukuliana tu! Lakini papo hapo watu dunia hii(wamataifa) wakisaidiana kweli kweli kwenye maisha yao!!! Hii ni mbaya sana! Anyway😂😐
“ Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.” Wagalatia 6:1
Mtu wa kwenu akiwa amekosea kwenye eneo lolote lile,wewe mtu wa Roho unapaswa kumrejeza kwa Bwana katika hekima yote,na kwa roho ya upole. Hili jambo ni muhimu sana,unapoweza kumchukulia mtu wa namna hiyo,hapo ndipo unapotakiwa kuzungumza naye kwa roho ya upole. Hivyo;ikiwa utatumia maneno makali ujue utampoteza zaidi mtu huyo badala ya kumuokoa. Na hili ndilo shida,leo akina mama wapendwa wanashindwa kuwachukulia vizuri mabinti wa kazi za ndani kiasi kwamba pale wanapokosea kidogo tu! Weee utaona moto wake huyo mama!!!
Sasa ukiwa ndiye mama wa nyumba na kufanya hivyo,ujue itagua ni vigumu kumrejeza mtu huyo kwa Bwana,au itakuwa ni vigumu binti huyo kukuelewa hata aokoke. Wokovu wako hautaeleweka kabisa!!! Sasa angalia badala ya kumfanya huyo binti aokoke badala yake ndio unampoteza kabisa kumbuka mtu yeyote afanyaye hivi hata kumpoteza mtu dhambini,atadaiwa damu yake!
Ebu sasa jifunze kutembea kwa kumchukulia huyo unayeishi naye huku ukiendelea kumuombea kwa maana Mungu ni mwema sana, Mungu atambadilisha huyo mtu lakini kazi inaanzia kwako.
Kwa msaada zaidi waweza kunipigia simu sasa;
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900/762 414 446.
Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments