top of page

KUANDIKA URITHI SIO KUJICHULIA KIFO!

Na mch.G.Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi sana.

Mzee mmoja aliyekula chumvi nyingi alikuwa akiumwa hoi, amelazwa. Lakini alikuwa akijitambua ingawa alikuwa anaumwa sana ; basi akiwa katika hali kama hiyo mwanae mmoja akamwambia “baba ebu sasa andika urithi wa mali zako” yule mzee alimtupia jicho mwanae kisha akamjibu “hafi mtu hapa! Unaniombea nife ili mgawane mali zangu, kwa taarifa yako, ninyi niombeeni, mimi nitapona bhana, kwa nini mnafikiria kifo?!! ! “ ona sasa!

Wazo la mzee lilikuwa kwamba wanamtakia afe ili wachukue mali zake, hivyo akaona kana kwamba wanamuombea afe! Lakini lengo la kijana lilikuwa ni zuri tu, kwamba aweke mrithi mapema kuepusha kugombana kwa maana alikuwa na mali nyingi. Kumbe swala la kifo ni lingine na suala la urithi ni lingine, na suala la kuomba ni lingine.

Hapo nikagundua wengi tumekuwa na mtazamo huo kwenye eneo la “ kuandika urithi ” tunafikiri ukiandika tu, basi huzungushi wiki lazima ufe! Nimeziona familia nyingi zikigombana kwa sababu ya mali ya marehemu mzee wao. Kwa sababu tu mzee alikufa “ kimya kimya ” akaacha malumbano! Sisi haswa waafrika tupo nyuma sana na kuandika mambo ya mirathi tukizania sivyo ndivyo. Sisi wapendwa ndio kabisaa kwa maana tunajua mambo haya sio ya kiroho, weeh ni jambo la kiroho hili ndio maana leo nataka nikupitishe kidogo kwenye biblia ili kwamba upate ufahamu sahihi katika kuandika urithi wako sahihi. Biblia inasemaje?

“ Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. ” Mwanzo 25:5-6

Ibrahimu alikuwa ni mtu mwenye mali nyingi na kwa sababu hiyo alihitajika mtu atakayeweza kuzisimamia na kuziendeleza iwapo kama Ibrahimu hatakuwepo. Ilikuwa si jambo dogo kwa mtu kama Ibrahimu kushindwa kupanga mikakati juu ya yote aliyokuwa nayo. Hivyo ; Kabla Ibrahimu hajafa alihakikisha amekabidhi mali zake zote kwa Isaka atakayerithi. Kisha akawapa na zawadi tu watoto aliyewazaa na suria Ketura, (kwa sababu Isaka ndiye atakayerithi na ni mtoto wa agano)

Isaka akapewa urithi wakati Ibrahimu alipokuwa hai. Biblia haituambii kwamba Ibrahimu alitoa urithi kwa wanawe kwa sababu alijua atakufa punde, bali biblia inatuambia Ibrahimu alitoa urithi kama sehemu ya kuwafanya watoto waanze kujua mikakati ya kutunza na kuendeleza mali na kuondoa ugomvi wa mali hapo baadae. Ni dhahiri Ibrahimu asingeliweza kuishi milele, hivyo ni kweli alijua kwamba siku moja na yeye atakusanywa kwa watu wake ( atakufa, kama wafavyo wengine)

Ikawa ni jambo la hekima kwa Ibrahimu kuandika urithi kwa kumgawia Isaaka mali zake zote na kisha akawafikilia watoto wa ndoa yake nyingine nao akawapa zawadi tu. Ebu fikiria, kama Ibrahimu asingelifanya jambo hili, je pasingelitokea magomvi katika watoto wake? . Ibrahimu baba wa watu hakutaka shida, mwenyewe akampa kabisa mwanae mali zake mapema.

Hatuoni ugomvi wa kugombania mali ukitokea kati ya watoto wa Ibrahimu maana kila mmoja alijua afanye. Ibrahimu alifaulu kwa hili, kazi ipo kwetu sasa.

“ Kuandika urithi kwa watoto “ ni utaratibu wa kihekima ili kuondoa mafarakano ikiwa mwenye mali hayupo. Wakati mwingine mwenye mali anaweza akawagawia watoto wake hususani mmoja kati yao, na mwenye mali akawa akimkotroo na kumuelekeza juu ya hizo mali. Ikiwa kama una mali, sasa kuna shida gani kuandaa urithi wa mali zako? Hakuna shida.

Ibrahimu ajua Isaka anatakiwa kuwa nani na wale wengine wanatakiwa kuwa akina nani. Kama asingelijua hili basi ni dhahiri kabisa angeliweza kuchanganya katika kugawanya mali zake. Lakini alimjua Isaka ni nani hasa, akampa yote aliyokuwa nayo. Nikuulize mzazi mwenzangu, Je unawajua watoto wako vizuri ni akina nani hasa?

Leo kuna shida katika hili, kwa sababu wazazi wengi wamekosa kuwajua fika watoto wao hata kuwalazimisha kuwa kama wao. Mfano baba alikuwa ni daktari, hivyo anataka na watoto wake wawe madaktari kama alivyo yeye. Hivyo baba wa namna hii atawapangia na masomo ya kusoma, lakini kumbe watoto walitakiwa wawe mmoja ni injia na mwingine mwana siasa. Lakini kwa sababu mzee hawajui vizuri watoto wake wanataka kuwa nani, basi yote hupanga yeye.

Ukimwangalia Ibrahimu, alitambua ni nani anapaswa kupewa urithi wake wote na ni nani anapaswa kupewa zawadi tu. Kuna wakati kwenye maisha ukikosea, hutapata nafasi ya kurekebisha tena! Mfano kama Ibrahimu angelikosea hapa mwisho, na amekufa Je angeliwezaje kurekebisha? Jifunze kuwaamini watoto wako mapema ukiwa u hai.

Ninajua hofu kubwa kwa wenye mali ipo pale wanapofikiria kwamba kama wataandika wosia wao basi wanaweza kuuwawa . Kwa mfano mwanaume anaweza akafikiri kama ataandika na kumwonesha mkewe basi kunaweza kukatokea tafurani kwenye familia, ni kweli inawezekana ikawa hivyo; bali mimi ninasema inategemea na mke gani uliyekuwa naye.  Lakini unaweza kutumia njia hizi, ikiwa kama inahofia;

  1. Kwa mwana-sheria – kwamba umjulishe yeye mwanasheria wako kama sehemu ya kutunza docs vizuri.

  2. Kiongozi wako wa wokovu.  Hakikisha umemshirikisha vizuri na kukufundisha namna utakavyofanya vizuri.

  3. Mwenzako wa ndoa ni vyema akajua yeye peke yake.  Lakini ni lazima apate kwanza elimu ya kutosha kwa maana asije akawa ndio chanzo cha mlipuko wa kufarakana, au chanzo cha kukuangamiza.

Hizo ni njia nzuri za kuhifadhi urithi au wosia wako.  Ni jambo muhimu sana hilo, kwa maana litaondoa tafurani siku utakapoondoka.  Si unajua kila mmoja ataondoka / kufa.  Hivyo, unaweza kufanya hayo.

Hata kama nafasi ya Isaka ingelikuwa ni nafasi ya binti, lakini bado hali ya kurithi ingelibakia pale pale kwa sababu ya agano. Hii ina maana kwamba huwezi ukamdharau mtoto wa kike. Maana wapo watu / wazazi / walezi wanaowadharau watoto wa kike kwa sababu wanajua wataolewa na kuamia kwa mmji mwingine. Hapana hutakiwi kumdharau mtoto wa kike kabisa kwa maana ukumbuke utakayemdharau ndiye atakayekusaidia. ; Sasa, ikiwa huna mali sio sababu ya kushindwa kuandika urithi bali andika kwa kile ulichonacho. Ni muhimu kuweka mambo yako vizuri wewe na mwenzako. Je umejifunza kitu? Ikiwa ndio tafadhali nijulishe na tujifunze zaidi kwako, nipigie sasa kwa namba hizi;

namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE. 

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page