KRISMASI NI WEWE UZALIWE NDANI YA YESU
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 26, 2017
- 2 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi sana…
Mimi ni mmoja kati ya watu ninaokereka nionapo mtu au watu tena viongozi wenye kutumia maneno wakati wa kufundisha kwako,wanatumia maneno pasipo kujua maana ya hayo maneno au misemo kibiblia. Ni jambo baya na la kushangaza kubeba jambo pasipo kulijua kisha na wewe ukalifundisha vivyo hivyo bila hata kutafakari. Imefika wakati sasa wa kukataa misemo ya kidini dini bali tuliangalie neno la Mungu linasemaje.
Tunaposherekea kuzaliwa kwa mwokozi haina maana kwamba Yesu azaliwe moyoni mwako kama wengi wasemavyo leo bali wewe ndiwe unayetakiwa uzaliwe upya ndani ya Yesu yaani uokoke. Tumekuwa na misemo mingi ya kidini kidini na tumekuwa tukiitumia pasipo kujua,lakini ukweli upo ndani ya biblia. Biblia haisemi kwamba Yesu azaliwe ndani yako,bali wewe ndiwe uzaliwe upya..
Ni muhimu sasa kubadilisha misemo tusioijua bali tutumie neno la Mungu. Ukweli ni kwamba,anayehitaji badiliko la maisha mapya sio Yesu,wala sio Mungu,bali ni wewe mwanadamu. Ikumbukwe kwamba Yesu alizaliwa mara moja tu,na hatutegemei kuzaliwa tena. Ila tunachokifanya sasa ni kukumbuka ujio wake kama masihi,ikiwa ndivyo basi ni dhahiri kabisa hatuwezi kumtarajia aje tena kuleta ukombozi,bali ukombozi umekwisha kuja kazi iliyopo ni wewe na mimi tumpokee Yeye naye awe Bwana na mwokozi wa maisha yetu.
“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa” Yohana 15:1-2
Kile ambacho Yesu anasema hapo ni kwamba Yeye ni shina,nasi tu matawi,Baba yake ni mkulima. Ametumia lugha ya ukulima akiwa na maana ya kwamba,matawi ni lazima yajiambatanishe na shina,na sio shina lijiambatanishe na matawi. Hii ikiwa na maana kwamba sisi tuliofananishwa na matawi ndio tuna kazi ya kujishikamanisha na shina. Kwa lugha nyepesi ni matawi yanatakiwa yazaliwe ndani ya shina,na ndani ya shina tuzae na tuzae ili tusafishwe zaidi. Shina ni lile lile bali matawi yazidi kuzaa ndani ya shina.
Sasa angalia mfano huo mmoja tu,jinsi ambavyo sisi ndio tuliokusudiwa kupata badiliko la rohoni la kuzaliwa au kuokoka na si Yesu azaliwe tena ndani yetu. Yesu ni shina ambalo limekwisha wekwa tayari,sasa kazi ni wewe ujiunganishe na shina hilo kwa kuzaliwa upya katika roho yako na hiyo ndio maana ya Krismasi.
Hakuna shida kuwa na kumbukumbu ya ujio wa masihi na kisha tukasherekea lakini shida iko tunasherekea vipi? Je tunasherekea kwa maana ya kiroho au kidunia? Je tunaelewa vizuri mambo haya? Je nia yetu ya ndani ni nini? Naogopa nionapo watu wenye kufanya mambo nje ya uelewa wa neno la Mungu.!! Mimi sijui kwa upande wako kama una uelewa mzuri kuhusu jambo!
Ebu nicheki kwa simu kwa maelezo zaidi,na pamoja na msaada wa maombi. Piga sasa kwa +255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments