KIBALI.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 31, 2017
- 6 min read

Na Mch.G.Madumla.
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi.
Kuna kibali cha mwanadamu na kuna kibali cha Mungu. Siku ya leo tunaangazia eneo moja tu la“ kibali cha Mungu kwenye maisha yako”.Ni mpango wa Mungu kwako kwamba uishi katika kibali kitokacho kwake. Kwamba maneno ya kinywa chako na mawazo ya moyo wako yapate kibali machoni pa Mungu ( kama isemavyo Zab.19:14). Unahitaji kibali katika yale yote unayoyawaza na kuyatenda,kwa maana kibali ni muhimu sana.
Kibali ni nini?
Juzi juzi tulikuwa na uchaguzi hapa kanisani kwetu. Uchaguzi huu ulikuwa ni uchaguzi wa kuwapata viongozi watano wa idara ya vijana ( Mwkt/Mwkt msaidizi,Katibu/Kaimu katibu na mweka hazina); Sasa,kupitia uchaguzi huo,nilijifunza jambo moja muhimu sana haswa kwa wale viongozi waliochaguliwa,kwa maana kulikuwa na vijana watatu ambao hawakuwako katika kikao cha uchaguzi.
Lakini mmoja wao akachaguliwa kushika nafasi nyeti ya mweka hazina. Nilipoliangalia jambo hili,nikajifunza kwamba huyu kijana aliyechaguliwa na watu wengi ingawa yeye mwenyewe hakuwepo kabisa,kwamba ana nafasi fulani kwenye mioyo yao. Au ni sawa na kusema kijana huyo alikuwa akikubalika miongoni mwa vijana wengi kiasi kwamba vijana wakamchagua pasipo kuhitaji kupiga kampeini wala pasipo na kujipendekeza tena pasipo kuwepo kabisa. Tena inawezekana neema tu ya Bwana iliyomfanya achaguliwe kuwa kiongozi. N.K
Huyu kijana alikuwa na “kibali” Ahaa! Nilipoendelea kujifunza kuhusu kibali,nikawaangalia wale vijana wengine waliochaguliwa kwa kura nyingi pasipokuwa na kampeini. Nikagundua kwamba walikuwa na kibali machoni pa vijana wenzao lakini walikuwa na kibali machoni pa Mungu pia. Aliyekuwa mwenyekiti wa vijana,akachaguliwa tena kushika hatamu kwa ungwe nyingine,tena akachaguliwa kwa kura nyingi kuliko kijana yoyote yule. Nilipolitizama jambo hili nikajifunza,kumbe mwenyekiti alikuwa akikubalika sana na vijana wengi lakini pia pamoja na Mungu alimkubali. Ndipo nikapata maana halisi ya kibali.
Kibali ni hali ya kukubalika kufanya jambo au kitu fulani. Kibali halisi chatoka kwa Mungu. Angalia jinsi Yusufu aitwae Barsaba na Mathiya waliokuwa wanafunzi wa Yesu,nao wote wawili waliwekwa mbele ya mitume ili mmoja wao ashike nafasi ya utume alioukosa Yuda Eskalioti ( Matendo 1:21-26.)
Hata hivyo kuna utofauti kati ya “neema” na “kibali” kwa maana Neema ni pale Bwana mwenyewe anafanya kwako bila nguvu yako yoyote ile,bali kibali mara nyingi hutegemea na mkao wako. Lakini muda mwingine Mungu anaweza kutumia neema kukufanya uwe na kibali mahali fulani. Kumbuka neno hili;
“ Kama ukitenda vyema, hutapata kibali?…” Mwanzo 4:7 ( Soma pia Warumi -13:3)
Bila shaka mwenendo na taratibu za kaini zilimnyima nafasi ya kukubalika mbele za Mungu. Katika andiko hili,tunaona kibali hutegemea taratibu stahiki au mkao wako mzuri na Mungu hata kukubalika kwa maana kama Kaini angelifuata utaratibu wa matoleo uliowekwa basi ni dhahili angelikubalika na Bwana. Mazingira kama haya yanahitaji sana umakini wa kufuata kile atakacho Mungu ili upate kibali. Kama vile mmoja wa watoto wako anayetekeleza yale umwambiayo,ni ni dhahiri utamkubali zaidi.
Ninaweza kukosa kibali?
Ndio unaweza kukosa kibali kwa maana kuna mambo ukiyafanya unaweza ukakosa kibali,kwa mfano;
01.Kudumu dhambini.
Ikiwa utadumu katika kufanya dhambi,basi ujue unajitenga na Mungu,ingawa Yeye Mungu hakutengi kwasababu ya dhambi zako. Lakini hata hivyo kitendo cha kukaa mbali na Mungu kinakunyima nafasi ya kukubalika zaidi. Kuna mambo yatakupita kwa sababu ya kudumu katika dhambi,ingawa bado pendo la Mungu li kubwa sana kwa wote pamoja na kwa watenda dhambi pia.
Lakini kumbuka jambo hili; “ukiwa mbali na Mungu,basi upo karibu na shetani”. Katika ( Isaya 59:2). Tunaelezwa wazi wazi ya kuwa maovu na dhambi zenu,zinauficha uso wa Mungu. Na mahali penye uso wa Mungu ndipo mahali penye kibali,usisahau hili. Kwa hiyo ni vyema kulifanyia kazi hili,hakikisha udumu katika dhambi yoyote ile.
02. roho ya kukataliwa.
Kuna watu ambao wanasumbuliwa na roho tu! na si vinginevyo. Kwa maana hata wakifanya chochote,hujikuta wakikosa kibali. Hivi huitwa ni vifungo,na kuna aina mbali mbali ya vifungo,inabidi ujifunze somo hili. Lakini katika roho ya kukutaliwa/the spirit of rejection;tunaweza kuona vyanzo fulani ambavyo ni;
Laana – Pakiwepo maneno mabaya uliyojitamkia au kutamkiwa na hayajashughulikiwa ipasavyo,basi ujue yanaweza yakakukwamisha kabisa na ukajikuta unakataliwa kila mahali. Laana ni jambo la kiroho ambalo linaweza kutembea na wewe kama ilivyo baraka jambo la kiroho linaloweza kutembea na wewe.
Maagano – Maagano ni yale mambo ya makubaliano mabaya juu ya pande mbili. Mfano unaweza ukaingizwa kwenye maagano au ukajiingiza wewe mwenyewe na mtu au watu,mkakubaliana juu ya jambo fulani kisha mkalikabizi kwa miungu kupitia waganga,na dawa mkanywa,damu mkanywa,au ukatolewa damu na kisha damu ikachanganywa na mambo yao. Sasa ikatokea umekwenda kinyume na makubaliano hayo,basi ujue miungu/mapepo hayatakuacha salama yatakufuatilia,na unaweza ukajikuta ukikosa kibali katika yote uyafanyayo maana wewe bado ni mali ya miungu,wanakuhitaji
03. Kujiinua/kujikweza
Kujiinua ni tabia ya shetani ya kutaka kupewa sifa anazo stahili Mungu. Au ni hali ya kutaka kupewa sifa ambazo hustahili kabisa. Hivyo kila anayejiinua Bwana atamshusha tu ( 1 Petro 5:5-6) Lakini soma pia yule Farisayo alivyojikinai katika Luka 18:9-14.
Ukiwa na tabia ya kiburi basi ujue huwezi kuwa na kibali machoni p Bwana hata mbele za watu. Mfano mdogo; ukiwa mtu wa kujiinua utaona hata watu hakupendi kiivyo kwa sababu ya tabia yako hiyo,tena inawezekana ukawa unataka kusema ujumbe mzuri tu,lakini kule kujisifia sana kunakupotezea kibali cha kufikisha ujumbe huo.
Je kibali kinapatikanaje?
01.Kwa neema;
Neema ni upendeleo wa kiungu usiostahili. Unaweza ukapokea kibali kila uendako kwa njia tu ya neema ambapo kwa kweli hukufanya jitihada zako wewe mwenyewe,bali Bwana amekuchagua kwa kusudi lake. Mtazame Yusufu,ingawa alitenda mema lakini alipewa pia na neema ya kuyatenda hayo. Na kwa sababu hiyo,hata leo kuna watu hukubalika basi tu,kwa nnema ya Bwana tena sio wazuri sana,wala si wenye pesa,na wala si wachaMungu sana,bali ni neema tu.
Hujawahi kuona mabinti warembo lakini wamekosa mume,hawajaolewa – wapo wapo tu,lakini kuana binti wa kawaida tu,na ndio kaolewa tena ndoa bab kubwa! Au hujawahi kuona tajiri kakosa mtoto na ni mlokole kweli kweli,lakini maskini mmoja anawatoto si mchezo! Hivyo wakati mwingine neema ya Bwana inaweza kuachiliwa kwako.
02.Kwa kuomba. (Yakobo 5:13)
Hii ndio njia ambayo wengi tumekuwa tukiitumia kuomba kibali cha Bwana. Unaweza ukaomba kibali cha Bwana katika maisha yako,na Mungu akakupatia. Hata hivyo si wengi wanaopata kibali kwa kuomba kama wamekosa uhusiano mzuri na Mungu wao.
03.Kwa kumcha Bwana.
Kumcha Bwana ni mchakato wa maisha ya kiibada. Kumcha Bwana ni kitendo cha kuwa na roho ya kicho;Hivyo kumcha Bwana ni hatua ya msingi ya kuvikwa kibali cha Bwana. Kabla ya yote,ukimuamini Yesu na kumpokea awe Bwana na mwokozi wa maisha yako,
basi uwe na uhakika atakupa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu (Yoh.1:12)Kile kitendo cha kupewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu kinakupa nguvu ya Mungu katika yale uyatendayo.
04. Kuwa mwaminifu ~ Ukiwa mwaminifu katika nyanja zote za wokovu wako basi ujue kibali kitakuwa ni sehemu yako.
Tunaweza kujifunza kwa Yusufu mtoto wa Yakobo. Yusufu alikuwa amekaza kwa Bwana na mtu mwaminifu kiasi kwamba alipolazimishwa alale na mke wa Potifa alikataa akaona hawezi kumkosa Mungu kwa dhambi hiyo ya kutembea na mke wa boss wake ( Mwanzo 39:9). Tazama jinsi Yusufu alivyotembea katika kibali cha Mungu katika maisha yake. Kila alipoingia mahali,Bwana alikuwa pamoja naye;angalia kaingia katika nyumba ya Potifa,gafula nyumba nzima ikabarikiwa,
kaingia tena gerezani Bwana akamuinua kutoka huko mpaka akawa waziri mkuu wa nchi ya Misri.Haikuwa ni jambo la kawaida tu,bali Mkono wa Mungu ulimtangulia na ndio kibali chenyewe tunachojifunza leo. Unahitaji kibali kama hicho,basi ukubali kulipa gharama ya kuwa mwaminifu. Ifike wakati uikimbie dhambi ujitunze katika kifungo cha uaminifu.
05. Jaza Neno (Maarifa ya kiungu).
Ukiwa na neno kwa wingi ndani yako ni sawa na kusema umembeba Yesu ndani yako kwa maana Yeye Yesu ndio Neno mwenyewe. Na ikiwa utakuwa umekaa ndani ya Yesu na Yesu ndani yako, hapo uwe na uhakika utakuwa na kibali machoni pa Mungu kwa maana yale uyatendayo hayatakuwa yako bali yatakuwa yametoka kwa Mungu.
Labda jifunze kwa kumuangalia yule mwana-punda aliyembeba Yesu katika LUKA 19:33-37. Utaona kwamba mwana-punda akikubalika na kundi kubwa la watu kiasi kwamba ilimbidi atembee juu ya nguo na matawi waliyoyatandaza watu,kitu ambacho kilikuwa hakiwezekani kwake isipokuwa kwa kumbeba Yesu tu,naye akapata heshima ya juu.
Matokeo ya kibali.
01. Wepesi wa kushuhudia. – Mara nyingi ukiwa na kibali cha Mungu,utajisikia kumshuhudia Mungu kwa watu wengine,kwamba Bwana amekutendea mambo ya ajabu. Na utajikuta ukiwa na wepesi wa kushuhudia kokote utakakokwenda.
Matokeo ya kukosa kibali. – Dharahu haitakuacha,kwa maana utaweza kuwadharu wenye kibali,na kuona kwamba walinga! Lakini pili,kuteseka huku na huku pale unapoingia sehemu,watu hawakuoni,na unaweza ukafanya kitu kizuri lakini kisionekane kabisa. ! Wakati mwingine hasira inakuwa haikuachi.
Inawezekana ikawa ni kweli kabisa inapitia katika changamoto hii,na umejitahidi sana kushughulikia ili uweze kuwa na kibali lakini,bado hujafanikiwa. Basi leo naomba tuombe pamoja katika hili,waweza kunipigia simu yangu hizi;
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app ni+255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments