KAZI YA NENO LA MUNGU.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 8, 2015
- 9 min read

Zipo faida nyingi sana za neno la Mungu maishani mwetu,faida hizi ni nyingi mno kiasi cha kushindwa kuzieleza zote hapa. Lakini tuangalie faida kumi na tano (15) tu ambazo nazo ni chache kati ya nyingi zilizopo. Faida hizi huitwa “thamani ya Neno”. Siku zote ukijua thamani ya kitu basi ni dhahili utakitafuta kitu hicho.
Ukijua thamani ya dhahabu basi uwe na uhakika utaitafuta kama tuonavyo leo watu wakitafuta dhahabu kwa muda mrefu katika kuchimba bila kukata tamaa. Na ndivyo ilivyo hata katika Neno,endapo utajua thamani ya Neno basi utalitafuta bila kukata tamaa.
Awali ya yote ikumbukwe kwamba neno la Mungu katika biblia ni sauti ya BWANA MUNGU iliyohifadhiwa kwenye maandishi. Ni MUNGU mwenyewe akizungumza na wote wenye mwili.Sauti hii ya Mungu imekusudiwa kwetu katika Kutufundisha,kutuonya makosa yetu,kutuongoza katika njia sahihi na kutuadabisha katika haki~ 2 Timotheo 3:16
Tunapaswa kujifunza na kulitii neno la Mungu kila siku iitwapo leo kwa maana katika neno la MUNGU ndipo tunazungumza na MUNGU na ndipo mahali ambapo tunakamilishwa ukristo wetu. Tuangalie umuhimu wa neno la MUNGU katika maisha yetu. Tunaposema “Thamani ya Neno ” tuna maana ya “kazi ya neno la Mungu katika maisha yetu” .
Kwanza ni ukweli usiopingika kwamba neno la Mungu ndio kila kitu katika maisha yetu,kwa maana sisi hatuwezi kufanya lolote nje ya neno la Mungu. Zifuatazo ni baadhi tu ya kazi zinazofanywa na neno la Mungu katika maisha ya mwamini.
01.Kujenga imani ya kweli.
Jiulize; Je lisingelikuwa Neno kuhubiriwa kwako,ungelikuwa na imani gani? Je ungemuamini Mungu kama jinsi unavyomuamini sasa? Au Je kama si Neno kulisikia ungeokokaje? Au Je kama Neno lisingelikuwepo ungeliwezaje kumjua Mungu wa kweli. Au Je kama Neno lisingelikuwepo ungewezaje kusamehe na kuachilia ? N.K
Maswali hayo yanaonesha kwamba unaamini kwa sababu ya Neno limekujenga katika kuamini. Unaweza kusamehe kwa sababu Neno limekufundisha kusamehe. Hivyo Ni neno tu liwezalo kukujenga katika misingi ya iamnai ya kweli. Emu angalia ni wapi ulipotoka na wapi ulipo sasa,angalia na kuaona kwamba Neno limekuleta katika kuamini katika usahihi. Lakini Ili uwe na imani iliyo ya kweli,ni lazima usikie habari sahihi za Kristo Yesu,
kwa maana chanzo cha imani ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17). Yeyote asiyekuwa na imani inamlazimu asikie habari za Yesu,ambazo kwa hizo hujenga imani ya kweli. Hakuna jambo kubwa la msingi katika imani kama kusikia neno la Kristo,kwa maana ili mtu aweze kuamini ni lazima asikie habari za Yesu.
Hapo ndipo mahali penye kuijenga na kuiimarisha imani yako,ni kwa njia ya neno la Mungu kwanza. Tunaweza kujifunza tukiangalia kwa yule towashi wa Kushi (Matendo 8:27-38)
02.Kutukuza kiroho.
Ukuaji ni kitendo cha kuongezeka katika kumjua Mungu wa kweli. Au ni kitendo cha kutoka katika hatua ya utoto wa kiroho na kuelekea katika hatua ya juu ya uwana. Hatua moja wapo ya msingi ya ukuaji wa kiroho ni Neno la Mungu.Kama ilivyo kawaida katika ukuaji wa jambo lolote lile linahitaji mambo muhimu ya ukuaji na jambo mojawapo la muhimu katika ukuaji wowote ni chakula.
Angalia mfano wa mtoto mchanga kile anachokihitaji ni maziwa halisi ya mama yake,maziwa ni chakula safi kwa mtoto na umfanya mtoto kukua vizuri akiwa imara,vivyo hivyo neno la Bwana ni chakula cha roho zetu. Ili tuweze kukua vizuri tunahitaji kiwango kizuri cha neno la Mungu. Neno lina kazi ya kutukuza kiroho, ( 1 Petro 2:2,Mathayo 4:4).
Sasa emu angalia tena, ikiwa mtoto atapewa maziwa yaliyochakachuliwa ujue ya kwamba ukuaji wake utakuwa wa kimashaka,hatakuwa vizuri na ndivyo ilivyo ikiwa mtu atakae kuwa akila neno lililochakachuliwa,neno lisilo na nguvu basi ujue hawezi kukua kiroho inavyotakiwa.
Pia kwa neno la Mungu ndipo mahali tunazaliwa mara ya pili kwa mbegu isiyoharibika kwa maana neno ni mbegu isiyoharibika “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.” 1 Petro 1:23
Ili uweze kukua hata kufikia cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo,unahitaji kiwango kikubwa cha Neno la Mungu. (Waefeso 4:13-15)
Neno linapofanya kazi hii ya ukuaji wa kiroho,mambo mawili hutokea;
Kupewa uwezo wa kushinda majaribu na dhambi (Yoh.8:31-32)
Roho yako kuwakwa katika mambo ya Mungu ( Matendo 19:25)
03.Kutakasa na kutunza usafi wa moyo.
Imeandikwa“Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.”Yoh.15:3. Andiko hilo linatuonesha ya kwamba usafi uliofanyika hapo umetokana na neno la Mungu. Kile kilichowasafisha hawa wanafunzi ni neno walilolisikia. Basi ikiwa ni hivyo neno linausika na utakado wa mioyo yetu.
Lakini pia imeandikwa “ Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;” Waefeso 5:25-26.
Soma pia katika Zab.119:11 ( moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije nikakutenda dhambi) Ahaa ! Kumbe,kile kilichomfanya huyu ndugu ashindwe kutenda dhambi ni kiwango cha neno la Mungu aliloliweka moyoni mwake.
Kwa lugha nyepesi neno linakuzuia usifanye dhambi,kwa maana kuna wakati unaisikia kabisa sauti ya Roho mtakatifu kupitia neno ikikukemea katika mipango yako ya dhambi uliyoipanga. Utakuta mtu alipanga kutenda jambo baya,gafla neno la Mungu linajifunua kwake na kueleza kwamba“ hiyo ni dhambi,hiyo ni dhambi,hiyo ni dhambi,acha,acha…”
Waweza ukajiuliza kwamba ni mara ngapi ulikuwa ukifanya dhambi hali umeokoka tena dhambi zenyewe ni zile za kupanga kwamba unapanga kabisa kesho nitakwenda kufanya hivi na hivi,kisha unafanya kweli. Lakini angalia vile ulivyoendelea kudumu katika neno la Mungu kila siku,unajikuta hata kiu ya kutenda dhambi hiyo huna tena. Je kitu gani kilichokata kiu yako? Jibu ni neno la Mungu limekutunza usitende dhambi hiyo tena.
04. Kuleta uzima wa sasa na wa milele.
Kwa kuwa neno la Mungu ni pumzi hai,halisi ya Mungu Baba pumzi hii ni uzima kwa roho,miili na nafsi zetu ( Yoh.6:63). Kuna wakati unaweza hukawa huwezi kwa sababu ya ugonjwa fulani hivi,umekuelemea na hujui hata hufanyeje lakini mimi nataka nikuambie Neno la Mungu ndio dawa ya kwanza yenye kuhuhisha mwili wako,
lenyewe unapolisoma na kutafakari laleta afya,na kutia uzima ndani yako hata ujapo kufa utakuwa unaishi ( Yoh.11:25-26). Jaribu leo kuwa msomaji na mtendaji wa neno kisha utashuhudia wepesi utakaoupata na afya yako pia na ndio maana roho yako ikifanikiwa ujue na afya yako itafanikiwa ( 3 Yoh.:2)
05.Roho mtakatifu hutenda kazi ndani ya neno la Mungu.
Hii ni siri kubwa ya utendaji kazi wa Roho mtakatifu. Roho mtakatifu hutenda kazi katika neno lake. Ukisoma hapo katika kitabu cha Mwanzo 1:1-3,utagundua kwamba neno lilipotamkwa ndipo Roho mtakatifu naye akaingia kazini kulitimiliza. Utendaji kazi wa Roho mtakatifu hutegemea uwepo wa neno la Mungu,na ndio maana utakuta Roho mtakatifu akitenda ishara na ajabu penye neno la Mungu,watu hupona,hufunguliwa n.k. Kazi hii ya neno la Mungu ni muhimu sana,kwa maana nje ya neno la Mungu hakuna miujiza sahihi.
06.Uumbaji
Bwana Mungu aliumba mbingu na nchi kwa neno lake,na vyote vikawa.Zab.33:6,9 soma pia Waebrania 11:3. Hata leo Bwana Mungu anaendelea na uumbaji wake kwa njia ya neno,na ametushirikisha uumbaji huo. Lupitia neno lake tunaweza kuumba baraka badala ya laana,tunaweza kuumba uzima badala ya mauti,tunaweza kuumba afya badala ya magonjwa,tunaweza kuumba ushindi badala ya kushindwa.
Je unalitumiaje neno la Mungu maishani mwako? Una umba nini leo? Je unaumba kufeli kabla ya kufeli kwenyewe? Au je unajiumbia magonjwa hata kama hukuna magonjwa?
07.Uponyaji wa kudumu.
Bwana Yesu alitamka neno kwa wadhaifu,nao wakapona. Sisi nasi leo,twataamka neno la Mungu kwa wadhaifu,wagonjwa nao hupona. Ukisoma katika Mathayo 8:7-8,13. Pia Matendo 14:8-10.
Maandiko hayo yote mawili yanaonesha kwamba neno la Mungu linaponya,ona~Yesu alitamka kisha mgojwa akaponywa pia Paulo naye alitamka neno kwa yule kiwete naye akaenda saa ile ile. Tumia sasa vifungu vya neno la Mungu katika biblia yako,kili uponyaji sasa katika Jina la Yesu Kristo nawe utapona.
Angali kama Zab.118:17- kili ya kwamba hutakufa utapona na utayasimulia matendo ya Bwana na itakuwa hivyo.
08.Ishara,miujiza na matendo makuu ya kweli yamebebwa na neno la Mungu.
Suala la miujiza lipo hata kwa shetani lakini ukweli ni kwamba miujiza ya Mungu ndio miujiza ya pekee yenye ukweli kwa sababu imejengwa katika misingi ya neno la Mungu,(tazama hili katika miujiza ya Musa na ya wale waganga, maana Musa alifanya nyoka,nao wakafanya nyoka lakini nyoka wa Musa akawameza nyoka wao.shetani anaweza akafanya ajabu fulani,lakini muujiza wa Mungu ni mkuu kuliko hiyo ya shetani.)Tazama neno la Mungu lilivyobeba miujiza na ishara~Marko 16:20
09.Neno la Mungu ni uweza wake Mungu.
Ipo tofauti kati neno uwezo,na neno uweza. Uwezo ni nguvu fulani ya kawaida ya utendaji kazi,lakini uweza ni nguvu ya ki~ungu,ambayo hakuna mwenye nayo isipokuwa MUNGU tu. Uweza huu upo pia katika neno lake MUNGU. Neno la Mungu linapotamkwa basi ujue ipo nguvu ya utofauti kabisa ifanyayo kazi na lile neno.( Mwanzo~Ufunuo)
10.Linatusaidia kuomba.
Neno la Mungu likikaa ndani yako,nawe ukikaa ndani yake basi omba lote nawe utatendewa (Yoh.15:7). Siku zote,hatujui kuomba itupasavyo bila msaada wa Roho mtakatifu ( Warumi 8:26). Na siku zote maombi yasiyokuwa na mwongozo wa neno la Mungu ni kelele tu kwa Mungu,kwa maana huwezi kuomba ikiwa hujui unaombea nini?
Ni neno pekee linaloweza kukuambia mambo ya kuombea kwa wakati ulio sahihi. Kwa mfano wakati wa huzuni neno litakuelekeza uombe nini hapo,wakati wa furaha pia neno litakuelekeza namna ikupasayo ya kuomba sawa sawa na kipindi ulichonacho. Hata Danieli alipata ufahamu mpya wa namna ya kuomba alipovisoma vitabu (Danieli 9:1-3)
11. Neno la Mungu ndio kweli yote.
Kama vile tulivyoona hapo juu ya kwamba neno la Mungu linatakasa,maana neno lake ndio kweli ~Yoh.17:17. Hakuna mahali pengine ambapo tutapata kweli yote isipokuwa ndani ya neno la Mungu tu.
12.Neno la Mungu linatupa nuru katika maisha yetu.
Ni hakika ya kwamba hatuyajui mbambo ya sirini,ni kana kwamba tunaishi kwenye usiku wa giza,lakini neno ndio taa yetu ya njia zetu ( Zab.119:105) Ili uweze kupata nuru ya kweli ikuongoze katika njia yako,unahitaji neno la Mungu.
13. Neno la Mungu linatueleza sisi ni akina nani (Asili yetu) ni wapi tulikotoka,tupo wapi,na tunaelekea wapi?
Chanzo,asili ya kila kitu duniani kimeelezwa ndani ya neno la Mungu. Leo tusingelijua mahali tulipotoka na wapi tunapoelekea kama tusingelikuwa na Neno katika maandiko matakatifu. Biblia inatueleza chanzo cha mwanadamu kwamba kimetokana na Mungu,Mungu alituumba kwa sura na mfano wake ( Mwanzo 2:26). Lakini Neno linazidi kutueleza kule tutakapoelekea wadnadamu wote,huko ni “ mahali pa umilele”
Na siri ipo hivi; kila mtu ataenda kuishi katika umilele lakini itategemea huo umilele upo katika eneo gani Je umilele katika uzima na Bwana au umilele katika moto? Haya yote tunapata kujua tukiliangalia neno la Mungu ambalo limeeleza kila kitu na wala halijaficha chochote katika maisha yaliyopita,ya sasa na maisha ya baadae ya umilele.
Ukisoma habari za yule Lazaro aliyekuwa maskini na kula makombo ya yule tajiri katika kitabu cha Luka 16:19. Utaona Neno limefafanusha jinsi wote wawili walivyoishi katika mwili na pia Neno limeeleza jinsi walivyoenda kuishi katika umilele wao. Na ndivyo ilivyo hata sasa. Hivyo utagundua Neno ni kama kioo cha maisha yako,lenye kukueleza wewe U nani ulitoka wapi,na utaelekea wapi? Mimi nakushauri uishi sawa sawa na mapenzi ya Mungu ili umalize salama na uingie katika umilele na Bwana.
14.Ni silaha,upanga wa Roho. (Waefeso 6:17).
Upanga ni mojawapo ya silaha ya kujiami na ya kushambulia. Tunaona silaha hii ikitumiwa hata leo kufanya kazi yake iliyokusudiwa. Lakini Biblia imeeleza kuwa “Neno ni upanga wa Roho”. Roho anayezungumziwa hapo ni Roho mtakatifu,angalia vyema biblia yako na utagundua Roho aliyezungumziwa hapo ni Roho mtakatifu akiandikwa kwa kuanzia herufu kubwa.
Ikiwa ndivyo,basi Neno linaelezwa kuwa ni upanga wa Roho mtakatifu. Neno ni moja ya silaha anayoitumia Roho mtakatifu kufanya kazi ya kukata,kugawanya,n.k.Neno likibadilika na kuwa upanga wa Roho linafanya kazi kubwa mbili;
Kuchoma,na kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo wako. (Waebrania 4:12,Matendo 2:37)
Kufanyika silaha ya Mungu katika vita vya kiroho (Ufunuo 12:11,Luka 4:1-2-Yesu aitumia silaha ya Neno katika kupambana na ibilisi akiwa nyikani)
Kumbuka; Neno likiwa upanga basi ujue unakata kuwili yaani upende wa nje kwa adui na kwa watu wale unaowahubiria kiasi kwamba watu hao wanasikia kuchomwa mioyo yao kama vile upanga unavyochoma. Pili upanga unakata upande wa ndani yako,kwamba kile unachokihubiri na wewe kinakuchoma na kukugeuze kwamba ufanye vivyo hivyo kama unavyohubiri.
Ukiona Neno halikuchomi moyo wako basi ujue halijafanyika upanga wa Roho kwa maana ni Roho ndiye achomaye katika neno,na mara moja muombe Roho mtakatifu ili neno lake liweze kukuchoma na uweze kubadilishwa na hilo neno maana siku zote Neno zuri ni lile lenye kuleta maumivu fulanai ili wewe uweze kubadilika.
15.Neno ni mbegu yenye kupandwa kwenye mioyo yetu.
“Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu.”Luka 8:11 Soma habari ya mpanzi yote~Mathayo 13:1-43 Tarajio kubwa kwa mbegu iliyopandwa ni kukua na kuongezeka. Kumbuka mbegu ili iweze kuota inahitaji;
Ipandwe katika udongo mzuri
Ipewe maji ya kutosha na kupata mwanga mzuri. ( Lakini sharti ioze kwanza)
Na ndivyo lilivyo Neno ambalo ndio mbegu ipandwayo katika mioyo yetu. Unawezaa ukajiuliza kwamba sasa Neno linapandwaje kwetu ;
JUBU; -Neno linapohubiriwa au kufundishwa katika usahihi,kitendo hicho ni kitendo cha upandwaji wa neno la Mungu. Mungu anamtumia mtumishi wake aliyempaka mafuta kusimama kama mpanzi kisha kuliachilia Neno nalo neno linaishia katika moyo,moyo ni shamba la Neno kama mbegu.
Na ndio maana usipoelewa nalo hilo Neno,biblia inasema adui huja na kulinyakua mahali lilipopandwa ( Mathayo 13:19). Ikiwa Neno lililopandwa ndani yako halimei,basi ni lazima ujiulize kwamba kwa nini? Na ukijiuliza hivyo kwa umakini utagundua tatizo halipo katika mbegu (Neno) bali tatizo lipo kwako ( mahali pa shamba)
Hayo ni machache kati ya mengi,nimeona nikuandikie hayo ili uyapate kuyajua. Lakini wapo watu ambao wana ugumu mkubwa sana wa kusoma neno la Mungu. Wengine wakianza kusoma tu,mara husinzia. Wengine wakisoma hawaelewi hata kidogo,uchovu gafla uwakamata.
Naomba ukiwa wewe ni mmoja wapo kati ya watu wa namna hiyo,naomba unipigie simu hii;+255 683 877 900
What’s app +255 746 446 446
Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários