KAZI YA KILA ALIYEOKOKA.
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 15, 2017
- 4 min read

Na Mch.Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Ni vyema ukafahamu ya kwamba kila aliyeokoka ana kazi ya “kushuhudia matendo makuu ya Bwana” ili kusudi wasiookoka waokoke. Hivyo wewe una kazi ya kupeleka habari njema kwa watu wote. Hivyo;Kazi ya kiuinjilisti ni ya kila mmoja aliyeokoka/mkristo mfuasi wa Yesu. Kazi hii sio kwa ajili ya watu fulani tu,bali ni kwa kila amwaminiye Yesu na kumpokea. Ni vyema tena tukaelewa maswali yafuatayo;
Uinjilisti ni nini?
Je huduma ya uinjilisti ikoje?
Je pesa au mali zako zinaweza kuinjilisha?
Je nguvu ya kushuhudia inatoka wapi?
UINJILISTI NI NINI?
Leo kumeibuka hoja nyingi za michanganyo kiasi kwamba hoja hizo zimewafunga watu wengi washindwe kumzalia Bwana matunda yapasayo toba. Hii yote imetokana na kushindwa kuelewa maana halisi ya uinjilisti,au inawezekana watu wengine wanachanganya neno hili “uinjilisti” na huduma ya “uinjilisti” . Kwa kuanzia,tujifunze maana kamili ya uinjilisti kwa mujibu wa biblia;
Uinjilisti ni ushuhudiaji wa uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa watu wote. Paulo anasema “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” Warumi 1:16. Ushuhudiaji wa habari njema hufanywa na kila mkristo aliyeokoka,tena ni agizo kuu ( Mathayo 28:18-20)
“Kushuhudia uweza wa Mungu” ni neno lenye mapana katika maelezo kwa maana,uponyaji ni uweza wa Mungu,wokovu ni uweza wa Mungu,injili ni uweza wa Mungu,Karama zote nazo ni uweza wa Mungu katika Roho mtakatifu n.k.Hivyo vitu vyote hivyo vinaeleza ile nguvu na uweza wa Mungu wenye kuleta wokovu katika Kristo Yesu.
Hivyo mtu mmoja akishuhudia uponyaji alioupata katika jina la Yesu Kristo kwa kueleza sawa sawa na neno la uponyaji,mtu huyu tunasema “ameinjilisha“. Au mtu mmoja akisimuliza jinsi Mungu alivyomuokoa kutoka dhambini sawa sawa na neno,mtu huyu atakuwa ameinjilisha kwa wale waliokuwa wakimsikiliza. Hivyo utagundua uinjilisti ni zaidi ya kuhubiri madhabahuni na kipaza sauti. Ushuhuda wako katika jina la Yesu ni injili tosha hata kama haupo kwenye madhabahu.
Ukipata tafsiri hiyo ya uinjilisti katika sehemu ya kwanza,utagundua kwamba una kazi kubwa ya kufanya ili kuwaleta watu kwa Yesu sawa sawa na vile ulivyotendewa wewe. Na pili,utagundua kwamba huwezi kukwepa kazi hii hata kama wewe sio mchungaji,bali ikiwa tu umeokoka una kazi ya kuleta watu kwa Yesu yaani kuzaa matunda.Pale unapokaa yakupasa umuhubiri Yedu,pale unaposoma na rafiki zako yakupasa umuhubiri Yesu,pale unapofanya kazi unapaswa umuhubiri Yesu,pale unapokaa na mtu katika dala dala unapaswa umuhubiri Yesu,pale uendapo nyumbani kwenu kijijini huko unapaswa umuhubiri Yesu.N.K
Leo watu wengi wamesukumia mbali kazi ya kuvuna roho/kushuhudia kwa kisingizio kwamba wao sio wainjilisti. Biblia hakusema watu watapewa injili na watu wenye huduma ya uinjilisti,bai watu watapewa injili kupitia wewe na mimi na kila aliyeokoka,pamoja na wainjilisti wenyewe wale wenye huduma.. Angalia agizo kuu lisemavyo ( Mathayo 28:18-20),Yesu anasema na kila amwaminiye na kumpokea kwamba anakazi ya kupeleka injili kote.
02.JE HUDUMA YA UINJILISTI IKOJE?
Huduma ya uinjilisti ipo tofauti na ule uinjilisti wa kwanza ambao kila mmoja amepewa kuzaa matunda. Tunapozungumzia huduma ya uinjilisti tunazungumzia huduma mojawapo kati ya zile huduma tano alizozitoa Bwana “ Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;” Waefeso 4:11-12
Kwa sababu hii ni huduma kamili,basi ni lazima kuwepo na mzigo. Na lazima wachache ndio wafanye kazi hii kama sehemu ya huduma sawa sawa na vile walivyoitwa ( kwa maana hatuwezi kuitwa sote kuwa wainjilisti,lazima huduma nyingine ziwepo) Watu wenye huduma ya uinjilisti ndio wale tuwaonao wakihubiri popote pale,iwe stand ya basi,au mkutanoni,madhabahuni n.k Tofauti kubwa iliyopo katika uinjilisti wa kawaida kwa kila aliyeokoka na uinjilisti kama huduma ni kwamba;
Uinjilisti wa kawaida ni kwa watu wote waliookoka,wala hauna eneo maalumu mfano,popote pale mtu anaweza akamshuhudia Yesu,iwe ni kazini kwake,iwe ni shule au chuoni,iwe ni katika dala dala mahali apokaa na mtu mwenzake asiyeamini. Nk Bali uinjilisti katika sehemu ya huduma ni kwa wachache walioitwa,wenye mzigo;mara nyingi hutegemea eneo maalumu labda mkutanoni,kanisani,stand ya basi,ndani ya dala dala.
Uinjilisti wa kawaida huvuna wachache,bali uinjilisti wa kihuduma uwaleta watu wengi kwa Yesu/mavuno ni mengi. Kwa sababu uinjilisti wa kawaida mara nyingi hufanyika kwa watu wachache kama vile mtu mmoja aweza kumshuhudia ndugu/rafiki/jamaa yake. Lakini uijilisti kama sehemu ya huduma hufanyika kwa wengi na kuvuna wengi. Mfano Petro alipohubiri alivuna roho za wanaume 3000 ( Matendo 2:41)
03.JE PESA AU MALI ZAKO ZINAWEZA KUINJILISHA?
Ninafahamu ya kwamba wapo watu wenye kutumia pesa na mali zao kusapoti injili na hatimaye watu wakaokoka na wale wenye kuhubiri injili. Tena jambo hili ni jema sana,kwa maana biblia inasema “ watahubirije wasipopelekwa? “( Warumi 10:15) maana ni kweli tunawahitaji watu watakaotuwezesha ili tukahubiri injili. Inawezekana tukawezeshwa kwa pesa,mali n.k na vyote sio vibaya kwa maana vinatolewa kwa ajili ya kazi ya Bwana itendeke.
Lakini tuliangalie kwa makini swali hilo hapo juu, “Je pesa au mali zako zinaweza kuinjilisha?” Hivyo ni lazima tujue ni injili gani inayozungumziwa ambayo pesa au mali itakayoweza kuinjilisha.
Pesa na mali katika uinjilisti/ushuhudiaji wa kwanza.
Kumbuka; uinjilisti ni ushuhudiaji wa habari njema ziletazo wokovu. Ikiwa ni hivyo basi ni dhahiri katika uinjilisti wa kwanza pesa au mali haziwezi kuvuna roho za watu,sababu hazina kinywa cha kunena shuhuda za Bwana. Mfano huwezi kwenda kumuwekea burungutu la pesa mtu asiyeokoka kisha ukasubiri kwamba ataokoka na zile pesa bila kutamka neno. Jaribu leo nenda kwa mtu aliye wa mataifa alafu muwekee pesa mbele kisha uondoke alafu uone kama ataokoka au la!!! Sana sana atalichukua hilo burungutu la pesa na kwenda kufanya anasa,( atakwenda kunywa gongo,mabia n.k) Kumbe katika uinjilisti,ni lazima unene habari za Yesu zitakazomfanya asikiaye ahukumiwe na dhambi zake na mwishoe atubu.
Pesa na mali katika huduma ya uinjilisti
Kwa kuwa katika eneo hili,wale waendao katika kulitangaza neno la Mungu ni wachache waliochaguliwa,basi ni dhahiri wanahitaji kuwezeshwa kama sehemu ya huduma. Mawezesho haya yanaweza yakawa ni pesa,mali kama eneo,nyumba,usafiri,kurusha matangazo,vyombo,vyakula N.K Vyote hivi vina gharama zake,hivyo pesa inaweza ikatumika katika eneo hili ili kusudi kazi ya Bwana katika uinjilisti itendeke. Tunawaona wanawake kadhaa waliokuwa wakimuhudumia Yesu kwa mali zao ( Luka 8:3)
JE NGUVU YA KUSHUHUDIA INATOKA WAPI?
Ni vyema tena lazima kwa mshuhudiaji kuvikwa uwezo utokao juu ( Luka 24:49). Ubatizo katika Roho mtakatifu ndio jambo la msingi liletao nguvu ya kushuhudia kote kote bila haya,na kuwaeleza kwa usahihi habari za Yesu. Ndio maana wanafunzi wa Yesu walikatazwa wasiende kuhudumu nje mpaka wapokee nguvu ya ubatizo katika Roho mtakatifu ( Matendo 1:4-5,8 2:1-4) . Soma somo la ubatizo katika roho mtakatifu.
Kwa huduma ya msaada zaidi,na maombezi piga sasa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch.G.Madumla
UBARIKIWE.
Comments