KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU~08
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 14, 2016
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…

Na Mchungaji Madumla.
Karibu tuendelee kujifunza pamoja…
07. NI NAMNA GANI UTACHOCHEA KARAMA YAKO?
Katika sehemu hii,ni lazima tujifunze njia maalumu za kuchochea karama zetu,ili zikapate kumzalia BWANA matunda. Kuchochea maana yake ni kuikuza,kuifanya ichanuke,au kuisimamisha ionekane katika utendaji wake wa kazi.
Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kuichochea karama yako,na kumbuka kwamba kama hautajua namna ya kuichochea karama yako basi ni dhahiri kabisa,karama yako itadumaa na hata kufichika kabisa.Hizi zifuatazo ni njia za kuchochea karama yako;
(i)Kwa kuwekewa mikono na mtumishi wa MUNGU.
Mtumishi wa Mungu anayo nafasi kubwa sana ya kuchochea karama yako kwa kukuwekea mikono yake sawa sawa na kiu,au hitaji lilopo ndani yako na msukumo wa Roho mtakatifu ndani ya mtumishi. “ Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.” 2 Timotheo 1:6
Karama iliyopo ndani yako,ni kama kuni iwakayo moto taratibu,kuni hii ikikutana na kuni nyingine iwakayo katika ukubwa,basi ni dhahili kuni iliyoafifu itachochewa moto na kuni ile yenye moto mkubwa. Maombi ya namna hii yana nguvu sana. Katika eneo hili,mimi ninaona karama iliyo ndani yako ni kama kisima kidogo kilichofukiwa fukiwa,hivyo mtumishi wa MUNGU anafanyika kama mfukua kisima.
▪Ni lazima uombewe na mtumishi wa Mungu ili kusudi aweze kuondoa roho za hofu na mashaka ndani yako. Maana wapo watu ambao wana karama lakini ni watu waliojawa na hofu sana kiasi kwamba wanashindwa hata kusimama mbele za watu wakijiona kana kwamba wanaweza wakakosea.
Kumbe hali hiyo ya woga,wasiwasi,mashaka ni roho kamili ya shetani iliyopangwa kukuangusha na wala usiinuke. Mungu Yeye hakutupa roho ya woga. “Maana Mungu hakutupa roho ya woga,…” 2 Timotheo 1:7
(ii)Jaribu mara kwa mara kufanya kile unachojisikia kufanya kwa ajili ya Bwana Mungu. Mfano inawezekana ndani yako unajikia kuimba,na ukiimba unasikia bubujiko la rohoni. Ukiona hivyo inawezekana kabisa uimbaji ikawa ndio karama yako.
Tena hapo,ujitahidi kutumia muda wako katika uimbaji. Au inawezekana ukawa ya kunena lugha mpya,vivyo hivyo tumia muda wako katika maombi. Shida kubwa ya leo ni hii;watu hawataki kujaribu kufanya yale yalipo ndani yao.
(iii) Ongeza bidii ya kutumika kwa BWANA MUNGU.
Bidii ni jambo kubwa na la maana sana linaloweza kuchochea karama iliyopo ndani yako. Tazama usipokuwa na bidii ya kupenda kutumika kwa Bwana basi ujue kwamba karama yako haitakuwa na nafasi ya kuonekana. Shida iliyopo kwako,hutaki kujitoa kwa dhati katika kazi ya BWANA yaani umejitoa nusu nusu tu.
Utakuta huna muda wa kutosha wa maombi,tena huna muda wa kutosha katika neno la Mungu~kwako kumejawa na pilika pilika za mitoko isiyokuwa na tija katika wokovu,kisha wajiuliza “Hivi mbona mimi sijui karama yangu?…” Sasa utaijuaje karama yako ikiwa hujitoi kwa bidii kwa Bwana? Tena huna muda mzuri na Mungu,uko bize na mambo yako.!!
▪Suala la bidii sio suala la maombi tu,bali ni sula linalohusisha utendaji wa kujitoa kidhabihu kufanya kazi ya Bwana. Mfano,ikiwa utajitoa kwa Bwana vizuri basi,nusu ya ratiba yako itakuwa ni MUNGU.
~Angalizo;
Sisemi uwe unabakia kanisani tu pasipo kufanya kazi, au sisemi ya kwamba muda wako wote uwe katika shughuli za kanisa na huku umeiacha kazi. Bali ujaribu kumtanguliza MUNGU kwanza,ubalansi mambo yako. Bwana Mungu awe sehemu ya ratiba yako kwa sehemu kubwa. Lakini ikiwa wewe umeitwa kutumika madhabahuni pa Bwana tu,basi hiyo ndio kazi yako na uifanye kwa bidii ili karama iliyopo ndani yako ichochewe.
Wako watu wengine,kweli wameokoka~wanapenda kutumika kwa BWANA lakini ni wavivu wa kutupwa. Watu wa namna hii hushindwa hata kufunga na kuomba,bali siku zote upenda mitelemko tu. Yaani kama ukimkuta mmoja wa sampuli hii,utamuona akiangalia saa kila dakika pindi awapo kanisani.
Yaani anaona anachelewa kutoka,na endapo ibada imeisha basi ujue dakika moja tu wala humuoni kanisani,yeye mbio!!!~mimi huwa sielewi wanakimbiliaga wapi!!! Yaani hata kusalimiana na wenzake yeye hataki hana muda,mtu mmoja huwa anasema “…nawahi katika kikao,Au nawahi watoto nyumbani…” kumbe si kweli bali yeye ana mambo yake ya siri huko nje ya kanisa ndio hayo anayoyawahi. Sasa kwa staili hii utawezaje kuichochea karama yako ikiwa huna muda na MUNGU?
Tunajifunza kwamba bidii inachangia sana kuikuza karama yako. Tazama hata mtu wa Mungu Eliya,ambaye alifanya kazi ya BWANA kwa bidii katika maombi na tunaona bidii yake ikizaa matunda; “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.” Yakobo 5:17
(iv) Dumu katika uwepo wa MUNGU.
Hili ni jambo kubwa na zuri sana linalowezesha kuikuza karama yako. Kudumu katika uwepo wa Mungu ni kuendelea kufanya mazoezi ya kiroho kila siku kila saa,huku ukimsii Roho mtakatifu akusaidie. Hapo sasa waweza kuona ile karama iliyopo ndani yako ikianza kukua taratibu.
Mfano waweza ukawa na karama ya uponyaji,karama hii itaongezeka na kukua zaidi endapo utadumu katika uwepo wa Mungu maana aponyaye si wewe bali ni Mungu. Kudumu uweponi si jambo la kujiita mlokole alafu ikaishia hapo,no!! Bali ni mchakato endelevu wa maisha ya utakatifu.
▪Kumbuka haya yafuatayo;
(a) Kudumu katika uwepo wa Mungu ni pamoja na kuwa na maisha ya unyenyekevu wa moyo,kufuata yote akuagizayo Mungu.
(b)Karama haichochewi katika muambatano wa marafiki wabaya,(marafiki wa kidunia,wasiokuwa na haja na Mungu). Ukiwa na karama yoyote ile na ukiambatana na marafiki zako wasiomjua Mungu na wala hawana shida naye,basi ujue kwamba wataiua karama yako na kufutilia mbali.
Kumbuka wewe ni mfano wa Mungu,wewe ni nuru,hivyo inakupasa uangaze,sasa anza kuambatana na nuru mwenzako kusudi kila mmoja akawe sababisho la kuchochea nuru ya mwenzake “Chuma hunoa chuma;…”Mithali 27:17a
(c)Huwezi kuchochea karama usiyokuwa nayo. Yaani mfano wewe umepewa karama ya imani~sasa huwezi kuenda kuichochea karama ya unabii,kwa sababu hukupewa unabii bali utachochea kile kilichopo ndani yako. Na hiyo ndio maana ya kuchochea,kuchochea maana yake kukikuza kitu kilichokuwepo. Kama hicho kitu hakipo kuwapi kuchochea?
(d)Mchungaji wako anasehemu ndogo ya kuchochea karama yako,bali sehemu kubwa ni yako mwenyewe na Roho mtakatifu. Na ndio maana mchungaji hata kama angelijitahidi vipi kuchochea karama iliyopo ndani yako lakini kama wewe hujajitoa kwa dhati,basi zoezi zima la kuchochea ni kazi bure. Mfano;
~Chukua kuni yenye moto mdogo ya kuchochewa kisha kabla ya kuanza kuchochea ile kuni inajizima,alafu wewe mchocheaji ukaanza kuchochea kwa kupuliza. Ukapulizaa wee,ukapuliza wee~Nakuambia ukiiangalia utagundua kwamba imeshazimika kitambo,hali hujui kama ilizimika…
ITAENDELEA…
~ Kwa huduma ya maombezi,usisite kunipigia kwa simu yangu hii;+255 683 877 900
What’s app number +255 746 446 446
Na Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments