KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU~03
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 15, 2016
- 2 min read

Karama ya Imani (1 Wakorintho 12:9)
Kuamini kuna viwango vyake. Kuna kule kuamini kwa kawaida ambapo ni fungu la wote yaani kila mmoja anaamini kitu fulani katika ufalme wa Mungu. Lakini kuna daraja la juu la kuamini kwa “uhakika” tena kuamini bila ya kufundishwa na mtu. Mfano wa karama hii ni kumtazama baba yetu wa imani Ibrahimu mtu ambaye aliishi kwa kumtegemea Mungu tu katika maisha yake yote. Ibrahimu hakwenda kusoma shule ya mwanadamu yeyote kuhusu imani isipokuwa Mungu alimfundisha mwenyewe.
Ndani ya Ibrahimu kulikuwa na nguvu ya Mungu ya kuamini iitwayo “karama ya kuamini” mfano wa kuelewa karama hii ni kumwangalia mkulima apandae mbegu,Kisha uenda zake kulala,na kesho huja tena shambani kumwagilia maji mbegu aliyoipanda ardhini,kisha huondoka tena na baadae hufanya hivyo hivyo kumwagia maji,kuiwekea mbolea huku moyoni mwake akiwa na uhakika kwamba mbegu itaota.
Anawezaje kuamini hivyo kwa maana mbegu hiyo ameizika ardhini? Kinachomwezesha kuamini ni kwa sababu alipoipanda gafla ndani yake “akaona zao la mbegu hiyo” yaani anaona zao kabla hata kuona kwa macho. Mfano huo wa mkulima unaeleza uhakika juu ya kinachotarajiwa kuja, ambacho kwa macho ya damu na nyama hakionekani, lakini mkulima anakiona ndani,ni sawa na karama ya imani.
Kazi hii ni ya Roho mtakatifu ndani ya mwamini. Tena kwa kuwa Yeye Roho huwapa awapendao basi si wote wenye karama ya namna hii. Ndio maana kuna watu wachache ambao wana daraja la juu la kuamini na inawezekana wakawa sio wachungaji au viongozi kanisani,lakini ni watu hatari katika imani. Yesu ni mfano mzuri sana wa mtu mwenye karama ya imani.
Angalia mfano huu tena, fikiria pale mchungaji anapofundisha kanisani halafu baada ya neno utakuta wengine hawakuamini neno walilolisikia hivyo hawakupokea kabisa, lakini kuna wengine wachache wamelipokea na kuliamini neno. Sasa hapo unajiuliza kwamba mnenaji alikuwa mmoja aliyenena na wote,wote wamesikia, lakini wachache mno wamepokea. Kwa nini wengine hawakupokea na kuamini? Moja ya sababu ni kwamba walitofautiana “uwezo wa imani”
ITAENDELEA…
Kwa msaada zaidi;+255 683 877 900
What’s app number +255 746 446 446
Na mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments