KARAMA YAKO NI IPI?
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 10, 2018
- 4 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Kulikuwa na baba mmoja aliyekuwa akiishi na mtoto wake mmoja wa kiume,mtoto huyo umri wake yapata kama miaka 9 hivi ni mtoto mdogo hivi. Mara nyingi alikuwa akipelekewa mashitaka juu ya mwanae. Na mashitaka yalikuwa yakitoka kwa majirani wakimlalamikia mwanae kwamba anawasumbua kwa kelele za makopo aliyokuwa akiyapinga mara kwa mara! baba wa watu akawa anamuuliza mwanae kwamba kwa nini unasumbua watu kwa makelele yako? Lakini mtoto wake hakuwa na majibu wakati huo.
Tabia ya kupiga piga makopo iliendelea na sasa akawa akipiga piga meza ndani. Lakini baba yake hakumuelewa mwanae kwa nini yuko hivyo. Mtoto akiona waimbaji wakicheza mziki wa moja kwa moja ( live performance) basi akili zake huelekeza kwenye drums ( kwa mpiga ngoma)’. Baadaye kanisa fulani wakahitaji mpiga ngoma,basi yule baba akamwambia mtoto wake “ nenda kapige ngoma kanisani “ alipoanza kupiga ngoma,watu walipigwa na butwaa! “ Ahaaa jamani,mtoto mdogo anapiga ngoma hivi,aisee duh!!!” watu walisema hivyo.
Leo hii ni mpiga ngoma mzuri sana. Nilipomuona nami nikashangaa nikasema “What!!! Haaaa! Jamani huyu ni Bwana,mtoto kama huyu anapiga ngoma nyingi hivi alafu ni vizuri sana!!” Alinishangaza sana. Nini nataka niseme? Uwezo huu wa kutumika kwa Bwana pasipo kusomea popote,ni zawadi itokayo kwa Mungu. Sasa huu ni mfano wa kawaida ya moja ya zawadi itokayo kwa Mungu.
Tunapozungumzia neno “ Karama” ni zaidi ya huo mfano kwa sababu karama ni uwezo wa kiroho ( ndani ya mtu ) wa kutenda kazi ya Bwana. Au ni uwezo wa utendaji kazi wa Roho mtakatifu ndani ya mtu baada ya kuokoka. Zipo aina mbalimbali za karama lakini Roho ni yeye yule,pia zipo huduma tofauti tofauti na Bwana ni yeye yule.( 1 Wakorintho 12:4-5) kuna karama zile tisa ( Neno la hekima,neno la maarifa,imani,karama za kuponya,matendo ya miujiza,unabii,kupambanua roho,aina za lugha,na tafsiri za lugha. 1 Wakorintho 12:8-10.) Lakini pia kuna karama zile mbili (karama za masaidiano na maongozi -1 Wakorintho 12:28) lakini pia kuna zile karama saba – Warumi 12:6-11 “Karama hizi saba zitafundishwa hapa hapa,endelea kufuatilia mafundisho haya”)
Utagundua kwamba kila aliyeokoka ana karama yake,maana hakuna hata mmoja aliyeitwa kwa Bwana akaachwa vivi hivi. Hata wewe kuna karama yako. Ilimradi umeokoka,basi umeitwa kwenye eneo fulani utumike. Kumbuka ; karama sio kwa wasiookoka bali waliondani ya Yesu,waliookoka,kwa sababu karama ni uwezo au nguvu ya roho mtakatifu inayokuwezesha kufanya kazi ya Mungu. Sasa haiwezekani Roho mtakatifu akae ndani ya mtu aliyemkataa Yesu.
Kumbuka,karama ni tofauti na kipaji kwa sababu kipaji ni uwezo wa kimwili wa kufanya kazi fulani. Uwezo huu hautegemei kwamba umeokoka au hujaokoka,yeyote anaweza akazaliwa na kuwa na uwezo wa kufanya jambo fulani,mfano niliokutolea hapo juu wa kupiga drums / ngoma ni uwezo wa kiasili / kimwili lakini katika uwezo wa namna hii ikiwa mpigaji akiokoka na kukaa kwa Bwana,basi Roho mtakatifu anautumia uwezo huo huo kuuleta katika karama.
Lakini pili,karama inajitokeza wakati mwingine bila kutegemea uwezo wa kiasili wa kuzaliwa nao na hii ndio karama ninayoizungumzia,mfano mtu baada ya kuokoka anajikuta ana uwezo wa kiroho wa kutenda miujiza sawa sawa na neno,mwingine kufundisha,mwingine kushauri,mwingine imani thabiti n.k mambo ambayo hakuwa nayo hapo mwanzo!
Lakini swali la kujiiza lipo pale pale, “ Karama yako ni ipi? ” ni eneo gani ambalo Roho mtakatifu anakutumia vizuri katika kazi ya ufalme wa Mungu? Na ukiweza kujua karama yako hautakuwa na sababu ya kutaka kuwa kama fulani,wala hautakuwa na sababu ya kumuiga fulani. Na hilo ndilo tatizo ulilonalo,kwamba hujui karama yako ni ipi!!! Lakini si wewe tu,ni wengi leo tunafanya huduma kwenye viwango vya chini sana kwa sababu hatujui karama zetu ipasavyo. Kwa hiyo wengi tunajikuta tukiigiza sana!!! Hakuna kitu kibaya chini ya jua hili kama kuigiza kwenye kazi ya Mungu ni heri hata usifanye mpaka ujue wito wako hasa ni nini?
Hivi unalijua hilo? Maana kuna watu ni waalimu,lakini wanafanya kazi kwenye ofisi ambazo sio zao,utakuta wakijiita wainjilisti,wengine ni wana unabii lakini wapo kwenye kwenye uimbaji n.k sio vibaya,lakini ujue kama umekaa mahali ambapo si pako,ujue matokeo yake ya kazi hayatakuwa mazuri. Jiulize je unaijua karama yako?
Njia zifuatazo zinaweza kukusaidia kuitambua karama yako
01. Kwa kuombewa na kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu.
“ Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.” 2 Timotheo 1:6
Timotheo alikuwa na huduma ya kichungaji ndani yake,karama ya kuchunga ilikuwepo lakini haikujitokeza. Paulo anamkumbusha mwanae wa kiroho Timotheo aweze kuichochea hiyo karama kwa kuombewa naye. Hata wewe ambaye yamkini hujui karama yako,ukiombewa na mwenye nguvu eneo hilo basi ujue utaichochea karama yako iliyojificha.
02. Kitu gani unapenda kufanya bila kushurutishwa? Fanya kwa bidii na kitakupelekea uijue karama yako.
“ Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu.” 1 Samweli 17:15
Daudi alipenda kuchunga wanyama,kuhakikisha yupo karibu sana na kondoo zake. Hali hii aliipenda sana ingawa kondoo walikuwa wa babaye mzee Yese. Biblia haituoneshi mahali popote ambapo Daudi akilazimishwa kuchunga mifugo ya babaye,lakini tunaona Daudi akijitoa hata kukubali kupambana na wanyama wakali kama dubu na simba ili kulinda uhai wa kondoo zake za babaye. Hali hii Bwana aliiangalia akaangalia moyo wa mtu huyu na kuona ni moyo wa kumpendeza. Na ukisoma biblia yako utaona Daudi baadaye alikuwa mfalme aliyewaongoza watu wa Mungu,Bwana alimtia mafuta ya kichungaji.
Angalia kile unachokipenda kufanya mara kwa mara hapo kanisani kwenu. Mfano kuna watu fulani wao wanapenda kusimamia na kuratibu mambo yakae sawa ingawa hawawezi kufundisha wala kuhubiri. Kitendo au tabia hiyo inawapelekea kuitambua karama yao,; watu wa namna hii huwa wanakuwa na karama ya “ masaidiano na maongozo ” Je wewe upo wapi?
Leo hii ebu tafuta karama yako,ujue kwa usahihi upo wapi katika mwili wa Kristo. Waweza kunipigia simu sasa ili tuombe pamoja yamkini waweza kupata msaada zaidi,piga sasa;
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni+255 746 446 446 .
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments