KANISA (THE CHURCH) ~ 03
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 5, 2019
- 5 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Nidhamu kanisani ( church discipline)
Ukifanikiwa kuabudu kwenye makanisa ya wenzetu wazungu utagundua mambo yafuatayo kama sehemu ya utamaduni wao; kuvaa mini sketi kwa wadada sio mbaya, kutoboa maskio na kusuka kwa wanaume sio mbaya, kuchora tatoo kwenye mwili sio mbaya maana hata mchungaji msela fulani hivi, kapigilia chini moka kali kisha kisuluali kimodo kilichombana tiii, kisha kapiga na hereni na nyweli kapiga panki kachumbali fulani hivi!! Sijui kama unanielewa hiki nikisemacho😁😁😁
, na kwa wenzetu hakuna ubaya wala sio makosa ili mradi wameokoka tu! Lakini pia hata ukipiga pombe kwa mbali mbali bila kulewa kwa wenzetu walio wengi hakuna mbaya, n. K Hizo ni baadhi ya mila za baadhi ya wazungu. Ukirudi kwenye makanisa makanisa yetu ya afrika hasa hasa Tanzania. Akionekana mchungaji kachora matatuu mikononi mwake, au mchungaji wa kiume kasuka. Dah! Hapo humpati mtu, kwa maana si mila zetu. Hivyo utagundua kila taifa/bara lina tamaduni zake tofauti na za taifa/bara jingine. Kile unachokiona kibaya wewe mtanzania mwenzako mzungu anaona kiko sawa tu na maisha yanasonga mbele.
Siku moja mtu nilimwona mtumishi wa Mungu mmoja wa kike, alikuwa ni mdada mrembo mmoja hivi. Ile kumcheki, nikawaza moyoni mwangu ``mmhh huyu,!! Hapa hakuna mtumishi, mtumishi gani wa namna hii,… Jamani tunaelekea wapi” mimi nilianza kumuhukumu kwa jinsi alivyokuwa amevaa. Alivaa utafikiri anakwenda disko tena disko lenyewe ni la usiku. Kisuruali fulani kinachombana na kumchora, na ndivyo alivyovaa.
Lakini nilipokuwa nikiongea naye, Aisee mdada alikuwa yupo vizuri rohoni kweli kweli! Yaani tofauti kabisa na anavyoonekana. Na akaniambia kwamba wao kanisa kwao hakuna shida yoyote kwa mambo madogo madogo ya mwilini, hata mchungaji wao ndivyo anavyovaa.! Basi, nikaona isiwe shida!!! Tuendelee tu na kila mtu alivyojengwa.
Lakini tunapozungumza kuhusu “nidhamu kanisani ” hatulengi tu suala moja la mavazi bali tunalenga mambo mengi kupangwa katika utaratibu ufaao. Hivyo kumbuka; Hakuna kanisa lenye watu wakamilifu isipokuwa kanisani ni mahali pa makimbilio. Utagundua katika kila kanisa kuna waovu pia wapo humo. Unaweza ukajiuliza kwa nini wakosaji wanapatikana pia kanisani? Lakini tambua tu, wakosaji wametokea duniani na wamekimbilia kanisani.
Hii haina maana mkosaji akiingia kanisani mara moja huwa mtakatifu. Suala la utakatifu ni mchakato, na ndio maana unaweza kuona kuna gharama kubwa ya utakatifu. Hivyo, kuna mambo muhimu matatu ndani ya kanisa nayo ni;
Mafundisho halisi ya imani katika injili ( faithful preaching of the gospel)
Kufanyia kazi maagizo ya Bwana, kama ubatizo na meza ya Bwana ( Practicing the ordinances like baptism and Lord’s supper)
Nidhamu ya kibiblia ( Biblical discipline)
Mambo hayo matatu ni mambo muhimu sana ndani ya kanisa la Bwana. Katika jambo la tatu“nidhamu ya kibiblia“ni moja ya jambo muhimu ambapo kama halijashughulikiwa ipasavyo, matokeo yake kanisa umeguka na watu gafla huama kanisa. Makanisa mengi yana taratibu zao za kushughulia suala zima la nidhamu ndani ya kanisa. Bahati mbaya sana wengi hutoa adhabu kwa wakosaji badala ya kutoa nidhamu. Na wengi hujikuta katika kushughulika na wakosaji ndio wakiwapoteza kabisaa! Yaani ni afadhali wasingelishughulikia nao. Tatizo sio wakosaji tena, bali tatizo ni kiongozi wa kanisa /huduma ametoa “adhabu” pasipo kujua kwamba alitakiwa kutoa “nidhamu ya kibiblia “ juu ya mkosaji ili kumfanya mkosaji aweze kurejea vyema.
Kanisa linatakiwa litoe nidhamu gani kwa mtenda dhambi na mkosaji asiyetaka kubadilika?
Swali hilo ni gumu kidogo lakini tunaweza kujibu vyema pale tunapoiangalia biblia inasema nini haswa. Katika biblia yalikuwepo makanisa ya awali kipindi cha mtume Paulo. Na makosa yalikuwepo kama tunavyoyaona makosa ya leo. Lakini je walifanyeje? Yesu naye amefundisha taratibu stahiki za kinidhamu ndani ya kanisa, nazo ni;
01. Mkosaji aonywe.
“ Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.” Mathayo 18:15. Bola shaka kama kiongozi wa kanisa, kuomba ni jambo la kwanza na muhimu sana. Na kwa sababu hiyo Yesu anajua kwamba unawajibu wa kuomba, ndio maana mkazo mkubwa ukaanzia kwenye maonyo. Biblia imewaka utaratibu mzuri wa kinidhamu ndani ya kanisa ambao ni ;
“ kuonywa kwa mkosaji” lakini maonyo haya ni kati ya watu wawili tu yaani wewe na huyo mkosaji. Na mkosaji akipata kukusikia basi umefaulu kazi yako ya kinidhamu. Changamoto ninayoiona leo kwenye makanisa mengi, ni pale mkosaji akionywa katikati ya kundi la watu halafu kama hiyo haitoshi, basi anayemwonya anaweza kupeleka makosa yake kwa wengine kwa kuwafunulia siri yote. Hii ni mbaya, na sio utaratibu wa kinidhamu ndani ya kanisa. Kuonywa ni lazima kuwe siri kubwa kati ya mwonyaji na mkosaji, ambapo shaidi wenu ni Mungu tu na si vinginevyo.
02. Kama hasikii, ongeza watu wawili au mmoja, mwonye tena.
“ La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.” (Mathayo 18:16.) Biblia ipo makini sana. Inaposema uchukue mtu mmoja au wawili haina maana uchukue mtu yeyote tu, bali ina maana mtu mwenye hekima ndiye achukuliwaye. Kisha mkiwa pamoja mtaketi chini na kuzungumza kwa upole kabisa, huku mkiwa na lengo moja tu la kumrejesha na sio kumhukumu. Nidhamu inalenga kumfanya kosaji asirudie kosa bali arejee kwa Bwana. Akiwa awasikii ninyi sasa hatua ya tatu inahitajika.
03. Kanisa lishirikishwe, asipolisikiliza kanisa awe kwako kama mtu wa mataifa.
“ Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.” (Mathayo 18:17).
Kanisa kama watu wa Mungu. Ndani yake wapo watu ambao wanaweza kushirikishwa katika kutoa mashauri. Watu wa namna hii ikiwa hawajafanikiwa kumrekebisha kwa kuwa mkosaji amekataa mashauri yao. Basi hapo ndipo ndugu huyo awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru. “ Wamataifa na watoza ushuru” walikuwa ni aina ya watu wasio na Mungu. Hivyo walihesabika kuwa ni watu wenye dhambi waliofarakana na Mungu.
Biblia inaposema kwamba huyo ndugu awe kama mmoja wa watu wenye dhambi kwako ina maana wewe ushughulike naye kama unavyoshughulika na mtu mwenye dhambi na asiyekuwa na Mungu. Ebu nikuulize, Unashughulika vipi na watu wa namna hii/wamataifa? Bila shaka utapenda kwenda nao pole pole ukitamani wampokee Yesu. Hivyo ukishughulika na mwenye kudumu dhambini mambo yafuatayo hufanyika;
Kumwonesha upendo/ na kumpenda – Yoh. 3:16
Kumfundisha Neno kwa taratibu – Neno la Kristo
Kumchukulia.
Lakini hiyo ni namna ya kwanza kabisa ya nidhamu ya ndugu aliyekosa. Wakati mwingine kumwondoa mtu kutoka kanisani ili afundishe ni moja ya nidhamu muhimu sana. Kwa mfano akiwepo ndugu aliyelala na mama yake tena akawa akiendelea, yafaa kumwondoa mtu wa namna hiyo. Paulo aliwaambia waamini wa kanisa la Wakorintho.
“ Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.” 1 Wakorintho 51-2
kanisa la Korintho lilikuwa na mvulugano wa mambo mengi sana. Ilifika wakati watu wa kanisa walikuwa wakifurahia dhambi ya uzinzi. Tena uzinzi uliokithili wa mtu kutembea na mke wa baba yake. Halafu kanisa limetulia na kujivuna kwa uzinzi. Zinaa ya namna hii haikuwako hata kwa mataifa lakini cha ajabu ipo katika nyumba ya Mungu.
Sasa adabu anayostahili kupewa ndugu huyo ni kuondolewa katika kundi, ili asije akalichafua kundi la Bwana. Kuna umuhimu mkubwa wa kumwondoa mtu katika nyumba ya Bwana ikiwa kama anariharibu kundi kwa yale ayafanyayo. Sio dhambi kumwondoa mtu kama analeta uharibifu mkubwa ndani ya nyumba ya Mungu ( Tafakari na maandiko haya;Tito 3:10-11,Warumi 16:17, 2 Wathesalonike 3:14-15)
Hivyo; kanisa ni lazima liwajibike katika kuadabisha watu wake ili pasiwepo na wapotoshaji ndani ya kanisa. Ikiwa kama kanisa haliwezi kuongoza watu wake katika nidhamu kanisa litakuwa na shida sana na kuna uwezekano wa kanisa kuwa uvuguuvugu kwamba Roho mtakatifu anaweza asiwepo hapo kabisa. Ni hatari kama nini kwa kanisa lisilokuwa na maonyo juu ya wanaodumu kutenda dhambi. Kila idara lazima ichekechwe kinidhamu ili hofu ya Mungu ionekane.
Hivi unafikiri kwa nini Mungu aliruhusu kifo kwa Anania na Safira ( Matendo 5:1-5)? Kwa sababu hawa jamaa walikuwa wakimchezea Mungu tena kwenye kipindi ambacho Mungu analitengeneza kanisa wao wakawa wanafanya masihara na hatimaye wajafa wote wawili. Hata leo, akiwepo mtu ndani ya kanisa na anafanya masihara ya dhambi hali akijua afanyalo, basi anaweza akapigwa na Mungu.
Na akiwepo mtu wa namna hiyo, na kanisa limekaa kimya hali likijua madhambi yote, basi kanisa litapigwa kwa bakola ( viongozi watapigwa kwa bakola na Mungu) Kanisa la Kristo si la kuchezewa chezewa, lazima nidhamu na adabu zote ziwepo…
Ikiwa kama umebarikiwa nifahamishe, pia Kwa maombi na msaada zaidi , piga +255 683 877 900
What’sapp namba .+255 746 446 446
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios