KANAANI.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 4, 2018
- 2 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi sana.
Unaposikia neno “Kanaani” unaelewa nini? Bila shaka utakuwa ukielewa Kanaani katika mtazamo mwingine. Hivyo ninakuandikia angalau upate na kuongeza maarifa.
Kanaani ni nini hasa?
Kanaani ilikuwa ni nchi iliyochukua jina la mtoto wa Hamu ( Mwanzo 9:18,10:6). Kanaani ndio palestina ( Kwa maana jina la Palestina hutumiwa kwa nchi ambayo hapo kale iliitwa Kanaani). Ni nchi hii hii ambayo Mungu aliwaahidi watu wake ( Waisraeli) kuwapa yaani Ibrahimu na kizazi chake (Mwanzo 12:5). Hivyo kwa waisraeli Kanaani ilikuwa ni nchi ya ahadi.
Watu wa nchi hii walikuwa ni waabudu miungu. Na palikuwa na makabila mengi pamoja na Wakanaani wazawa waliishi hapo. Makabila kama vile “ Mkeni,Mkenizi,Mkadmoni,Mhiti,Mperizi,Mrefai,Mwamori,Mkanaani,Mgirgashi na Myebusi ” ( Mwanzo 15:18) ( Kanaani ilikuwa karibu na bahari ya kati kutoka Sidoni mpaka Gaza ikihusisha milima ya Shamu/ Siria pamoja na bonde la mto Yordani ( Mwanzo 10:15-19)
Lakini hata hivyo makabila makubwa mawili ndio yalikuwa na nguvu kubwa sana kabila la “Waamori,na Wakanaani wazawa” kwa maana Waamori walikuwa wameenea na kuoana na Wakanaani. Kwa sababu Mungu alikwisha wapa watu wake Kanaani, basi Kanaani ilitekwa. Kipindi ambacho Waisraeli walipoingia Kanaani waliteka nchi iliyopakana na mto Yordani ( upande wa Mashariki) iliyokaliwa hasa na Waamori.
Ukumbuke Israeli ilikuwa na makabila 12,hivyo makabila 2 tu yakabakia nchi ya ng’ambo ya Yordani na makabila 10 yakakaa sehemu ya juu ya mto Yordani ( Soma historia ya Israeli kwenye blogu hii,tafuta hapo juu)
Hata hivyo mara nyingi tunaona kwamba kulikuwa na ukinzani mkubwa na Wafilisti. Wafilisti walikuwa kama Wakanaani kwa sababu waliishi muda mrefu na kujijenga huko Palestina ( Kanaani) wakitokea kwenye kisiwa cha Kaftor ( Mwanzo 10:14). Wafilisti wenyewe walikuwa na miji mitano mikubwa,nayo ni ;
“ Gaza,Ashdodi,Ashkeloni,Gathi na Ekroni” Viongozi wa miji hii walikuwa wakiitwa “ mashehe“,yaani viongozi wa juu. Neno hili “mashehe” limetafsiriwa kiingereza kuwa ni “kings” ikiwa na maana viongozi wa juu,hivyo neno hili halina maana ya shehe wa kiislamu. Bila shaka umekwisha lisoma kwenye biblia.
Maana ya neno “Kanaani” ilipanuka zaidi kwa vile tunavyoweza kuielezea leo. Kwa sababu Kanaani ya leo hufananishwa na mbinguni,kama nchi ya ahadi. Lakini haikuwa hivyo kwenye biblia,Kanaani ilikuwa ni nchi tu ambayo Mungu alimpa Ibrahimu na uzao wake. Jambo moja la kushangaza ni kwamba; ingawa Ibrahimu alihaidiwa Kanaani, lakini iliwapidi wapigane ndipo waipate hiyo Kanaani!! Umewahi kujiuliza kwamba kwa nini tena kunakupigana na kuwashinda maadui ndipo waingie Kanaani?
Kwa sababu Kanaani ilikuwa inakaliwa na makabila zaidi ya makabila matano. Sasa Mungu anawataka watu wake wakawaondoe hao watu waingie wao. Hapo ndipo utakapojifunza kwamba, maisha ya kuingia kwenye ufalme wa Mungu ni kupambana kila siku. Kanaani yako huwezi ukaingia kwa kula na kunywa na kulala bali ni kwa kukaza kwa Bwana kwa kupambana na roho chafu,na nia za dunia hii.
Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezi pia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 655 111 149 / 683 877 900 / 762 414 446.
WhatsApp ni +255 655 111 149.
Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios