top of page

JUU YA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA LANGU

Na mch.G.Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mathayo 16:18

Sasa emu ondoa jina la Petro hapo wakati wa kusoma,kisha weka jina lako; na sentensi hiyo itasomeka hivi : “ Nami nakuambia, Wewe ndiwe _____ na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Neno hili latoka kwa Yesu mwenyewe,na kama ni Yesu mwenyewe ndiye asemaye basi ukweli ni kwamba kanisa la kweli si la mtu au kikundi cha watu bali ni la Bwana mwenyewe anasema “…nitalijenga kanisa langu;…” 

Katika fundisho hili tutajifunza mambo yafuatayo sawa sawa na neno letu la msingi~ Mathayo 16:18. Yafuatayo ni haya;

  1. Kanisa ni nini?

  2. Kanisa la Kristo “ nitalijenga kanisa langu”

  3. Kusudi la kanisa

  4. Milango ya kuzimu haitalishinda kanisa la Bwana.

01. KANISA NI NINI?

Kwa mujibu wa neno la Mungu zifuatazo ni tafsiri tano tafsiri sahihi za maana ya neno hili “kanisa“. Awali ya yote neno hili “kanisa” tunalolitumia leo,lenye chimbuko la lugha ya kiyunani kwa jina la “ Kuriakon” yenye maana ya “ mali ya Bwana “ ndio maana katika andiko letu la msingi Mathayo 16:18 Yesu anasema “ nitalijenga kanisa langu,ikiwa na maana kanisa ni mali ya Bwana. Lakini ikumbukwe ya kwamba katika agano neno hili lilitafsiriwa kwa jina la Kiyahudi “ ekklesia” yaani “ watu fulani walioitwa na Bwana,au watu waliotengwa na Bwana

Hivyo basi;

(i )Kanisa ni mwili wa Kristo 

akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.” Waefeso 1:22-23 

Biblia inaeleza ya kwamba Yeye Kristo ndie kichwa cha kanisa,lakini kanisa ni mwili wake. Neno “kichwa cha kanisa ” lina maana ya “ kiongozi mkuu wa kanisa” . Katika tafsiri hii ya kwanza ni vyema kufahamu kuwa tu viungo vya Kristo kwa kuwa tu mwili wa Kristo. Ni jambo la aibu ikiwa kanisa linaitwa kwa mwili wa Kristo lakini limekumbatia dhambi,Je mwili wa Kristo waweza ukashiriki dhambi? Hapana hauwezi kushiriki dhambi yoyote ile.

(ii) Kanisa ni kusanyiko la waaminio katika Kristo Yesu.

 Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” Yoh.10:16 Ikumbukwe kwamba kusanyiko hili la waaminio limepewa jina kondoo waliokusanyika kama kundi pa moja na mchungaji wao. Kupitia andiko hili,Yesu anasema analo kundi jingine ambalo anapaswa kulileta pamoja na kwa kuwa ni mali ya Bwana basi,watamsikia.

(iii)Kanisa ni hekalu/jengo/nyumba ya kuabudia.

Tafsiri hii ni moja ya tafsiri ambayo watu wengi wameijua,kwa maana watu wanapotamka kuhusu kanisa humaanisha kwamba kanisa ni jengo fulani hivi. Kupitia fasiri hii;wanakuwa hawajakosea. Biblia inaeleza pia kwamba;20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.

“  Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.” Waefeso 2:21-22.

(iv) Kanisa ni bibi harusi wa Kristo;

“  Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.” Waefeso 5:31-32 

Ikumbukwe kwamba katika ulimwengu wa roho,kila aliyeokoka na kumfuata Kristo Yesu amefanyika kama bibi harusi. Kwa lugha nyepesi tumefunga naye agano;na ndio maana mtu akimuacha Kristo Yesu kisha akaigeukia miungu mingine basi anaitwa ni mzinzi/amezini. Umewahi kujiuliza kwa nini uitwe mzinzi hali hujazini katika mwili?  ( ufunuo 2:14). Hivyo tumuonapo bibi harusi basi ni dhahiri yupo bwana harusi na pia kuna harusi yao. Katika ulimwengu wa roho KristoYeye mwana-kondoo ndiye Bwana harusi kwa maana kuna harusi ya mwana-kondoo huko mbinguni ( soma Ufunuo 19:7)

(v) Kanisa ni hekalu la Roho mtakatifu.

Tafsiri hii inalenga hekalu za namna mbili. Hekalu la kwanza ambapo Roho mtakatifu anapokaa ni ndani yako ya moyo na hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza ya mwamini ( 1 Wakorintho 3:16). Pia hekalu la pili ni katika madhabahu sehemu fulani ya kanisa iliyotengwa kwa ajili ya kazi ya Bwana. Madhabahuni pa Bwana,mahali ambapo dhabihu zinapotolewa. Hivyo tafsiri hii inamlenga mwamini mmoja mmoja kuwa ni kanisa ( mwamini ametengwa kwa ajili ya Bwana,huitwa pia ni sehemu ya kanisa kwa sababu moyo wake u madhabahu). Kigezo kikubwa cha kanisa ni uwepo wa madhabahu mahali ashukapo na akaapo Bwana Mungu.

02.KANISA LA KRISTO.

Kanisa la Kristo si mali ya mchungaji bali ni mali ya Kristo ( Mathayo 16:18). Lakini hata hivyo leo si kila kanisa ni la Kristo kwa sababu kuna kanisa la Kristo na kuna makanisa ya watu binafsi walio nje ya Yesu hali wakidanganya kwamba wapo ndani ya Yesu. Kristo hana makanisa bali ana kanisa moja tu na ndio maana imeandikwa “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.” Waefeso 4:5. Hivyo hakuna Roho mtakatifu wengi,wala batizo nyingi wala Mabwana wengi. 

Swali la kwanza la kujiuliza;“Je kanisa la Kristo Yesu likoje sasa? 

JIBU; Kanisa la Bwana ni lile linalosimama katika karama ya Roho mtakatifu ya  maongozo na neno sahihi la Kristo ( lenye ushirika na Roho mtakatifu). Kanisa la na namna hii siku zote linamuinua Bwana sawa sawa na neno la Mungu,tena linafanya yale yote aliyoyaagiza Bwana. Hivyo utagundua kwamba kanisa la Bwana lipo moja tu,hata kama yapo mengi yenye kusimama vyema basi kwa pamoja linaitwa ni kanisa moja. Kanisa la Kristo haliwezi kufanya mambo nje ya kuongozwa na Roho mtakatifu. Angalia unaabudu katika kanisa gani? Je Roho mtakatifu anapewa nafasi,? Je neno la Mungu linahubiriwa kwa usahihi? 

Baadhi ya mambo ambayo kanisa la Kristo haliwezi kufanya;

  1.  Kumnyima nafasi Roho mtakatifu na vipawa vyake.

  2. Kuipa kipaumbele miujiza pasipo neno sahihi la Kristo.

  3. Kuyasema vibaya makanisa mengine ( hata kama makanisa hayo yana udhaifu,haitakiwi kuyasema katika madhabahu bali kuyaombea kwa maana maneno si dawa,bali dawa ni maombi)

  4. Kulea dhambi hali dhambi zinaonekana.

  5. Kuenda kinyume na neno la Mungu ( Mfano neno la Mungu linahubiri wokovu,lakini kuna makanisa yanakataa wokovu. Au neno la Mungu linafundisha juu ya ubatizo wa maji mengi,lakini kanisa linakataa)

  6. Kukaa bila ushuhudiaji na uinjilisti.( Kanisa la Kristo limebeba lengo moja tu,nalo ni kuhakikisha roho za watu zinaokolewa kwa hali na mali. Ni vyema washirika wafundishwe namna ya kuvuna roho za watu na jinsi ya kuzisimamia)

  7. Kupenda sifa/kunia zaidi ya Mungu. ( Yako makanisa yanayosimamiwa na watumishi waliojipa majina mengi tena majina ya ajabu ajabu yenye kuonesha wao ni bora zaidi,au kuonesha wana nguvu zaidi ya wengine)N.K

03.KUSUDI LA KANISA.

Kanisa la Kristo limebeba kusudi moja kubwa,kusudi hili ni kuvuna roho na kuzifanya roho hizo zifikie katika “uwana”. Leo kwa bahati mbaya makanisa yanayojitambulisha kwa jina la Kristo yamepoteza jambo hili muhimu kwa maana watu wanaokolewa kweli lakini hawafanywi wana-funzi. Kuokoka si kuwa mwana-funzi wa Yesu;kwa sababu kuwa mwana ni mchakato wa kudumu katika fundisho kiasi kwamba unakuwa kama Kristo alivyo ( Christ-like)

Kusudi hili la kufanyika “ mwana” ndilo linalozaa “ umoja katika Roho“. Haiwezekani umoja katika Roho ikiwa watu waliokolewa wapo katika utoto kwamba hawajafanywa wana. Labda sasa nitumie muda mfupi nikueleze japo kwa ufupi juu ya mchakato wa kufanyika mwana-funzi wa Kristo.

Neno hili “ mwana-funzi” limetoholewa kutoka katika neno “disciple” likiwa na maana ya mtu ajifunzaye kuwa kama mwalimu wake alivyo.Hivyo mwana-funzi wa Yesu ni tofauti mwanafunzi wa kawaida. ( mfano wa mwana-funzi anayezungumziwa ni kama wale wanafunzi waliopo VETA wanaojifunza ufundi na baada ya muda mfupi wanakuwa ni mafundi kama walivyo walimu wao).

Hivyo “ kufanyika mwana wa Mungu” ni baada ya kuokoka,kisha unaendelea kudumu katika mchakato wa kufundishwa (kama mtu wa VETA)na kufanya yote unayofundishwa. (Ukimpokea Yesu unapewa uwezo tu wa kufanyika mtoto ( child) wa Mungu. Uwezo huu unaopewa ni kuwa mtoto( child not son)-Yoh.1:12…

ITAENDELEA…

What’s app number ni +255 746 446 446

Mch.G.Madumla

Mawasiliano zaidi  +255 6877 900

UBARIKIWE.

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page