top of page

JIRANI YAKO NI NANI?

“ Ebu fikiri mara mbili” na Mch Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi…

Moja kati ya maswali magumu kwa watu wengi ni swali hili “jirani yako ni nani? ” hata leo akitokea mtu na kukuuliza swali hili sijui kama utakuwa na majibu sahihi, najua kujibu utaweza kujibu, lakini je utaweza kujibu kwa usahihi wake? Na hilo ndio jambo la muhimu. Kumbuka maneno haya “mpende jirani yako kama nafsi yako ” hiyo ni amri ya pili iliyokuu kuliko zote ( Marko 12:31). Lakini sasa jirani yako ni nani? Hivi yule unayeishi karibu nawe ndio jirani yako? Au mtu unayesali naye ndio jirani yako? Au hivi jirani yako ni yule rafiki yako? Siku moja niliulizwa swali hili, nami nikajibu hivi“jirani yangu ni mtu wa karibu nami” off course yes! Lakini kumbe nilitakiwa kujibu zaidi ya hapo. Anyway! katika agano la kale neno jirani lilitafsiriwa kama “rafiki wa karibu sana au ndugu ” hivyo ilikuwa ni marufuku ;

  1. Kumshuhudia uongo jirani yako wala kumsengenya ( Kutoka 20:16, Zab. 15:3)

  2. Kulala na mke wake ( Walawi 18:20)

  3. Wala kumtendea mabaya ya aina yoyote ( Walawi 6:2) n. k

Lakini Yesu anatoa tafsiri pana kwa kile kilichoandikwa kwenye sheria ya kumpenda jirani yako “Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.” Walawi 19:18 Yesu anaifafanusha kwenye mfano wa msamaria mwema (Luka 10:25-37 ).

Ukweli ni kwamba yeyote anayeishi Karibu nawe ni jirani yako, au yeyote unayekaa naye iwe kanisani, ofisini, shambani n. k huyo ni jirani yako lakini tafsiri hii haikidhi maana ya neno jirani. Ukisoma ule mfano wa msamaria mwema kwenye Luka 10:25-37,utagundua maana ya neno jirani imepanuka zaidi ya mtazamo wa kawaida.

Mwana-sheria mmoja alimjaribu Yesu kwa maswali, na ikafika wakati akamuuliza Bwana “jirani yangu ni nani? ” kwa kujibu swali hili, Bwana akamtolea mfano kumfahamisha jirani yake ni nani ( Soma Luka 10:25-37 yote). Mtu mmoja alishuka kutoka Yerusalem kwenda Yeriko, naye akaangukia kati ya wanyanganyi, kisha wakamtenda huyo mtu vibaya. Bila shaka mtu huyu alikuwa ni Myahudi maana alitoka Yerusalem, hivyo kama utatafsiri neno jirani kama “mtu yeyote aishie karibu nawe” bali ni dhahiri jirani yake mtu huyu angelikuwa kwanza ni “kuhani” maana Kuhani alikuwa Myahudi aliyeshuka toka Yerusalem. Tena jirani yake wa pili angelikuwa “mlawi” aliyekuwa ni Myahudi ambaye naye alitokea Yerusalem. Lakini hao wote wawili hawakuwa jirani ya yule ndugu Myahudi,! Kumbe, ukamilifu neno jirani sio ukaribu wa kuishi pamoja, kwa sababu ingelikuwa hivyo basi Kuhani pamoja na mlawi wangelikuwa jirani zake.

Msamaria mtu ambaye alikuwa hachangamani na Myahudi, aliyeshuka kutoka mbali, tena ni mgeni katika Israeli ndiye aliyekuwa jirani yake mtu yule aliyeangukia kati ya wanyanganyi. Basi, hapo lazima tujiulize, ni kitu gani kilichomfanya mgeni wa mbali awe jirani wa Myahudi huyo? Tukitafakari neno hili ( Luka 10:25-37) tutaweza kuja na majibu sahihi kwamba “jirani yako ni nani? ” umeona hapo! Ebu angalia kwa makini na utagundua ya kwamba kipimo cha mtu kuwa jirani hakipo katika ukaribu mnaoishi bali kipo katika “huruma na kutoa msaada“. Sababu yule msamaria mwema alimuhurumia na kumsaidia mtu ambaye kwanza yupo naye mbali hawachangamani kabisa lakini ndiye ameitwa jirani kwasababu tu ya matendo yake ya huruma na msaada alioutoa, na hapo akaitwa ni jirani.

Najua mimi nakaa mbali nawe, lakini naweza nikawa jirani yako. Au inawezekana mila zetu hazifanani na za kwako, tena labda hatuwezi kushirikiana baadhi ya mila lakini bado unaweza ukawa jirani kwangu. Ikiwa ndivyo, basi ni sawa na kusema majirani ni wachache tofauti na wale wanaokuzunguka. Hivyo neno “Jirani“ni mtu yeyote aliyekaribu nawe kimsaada zaidi pamoja na katika kuona huruma kama mfano wa msamaria mwema.

Sasa, jiulize ni mara ngapi umewapita watu wanaohitaji msaada wako? Ni mara ngapi hujawahurumia wale walio katika kuhitaji? Unajua wengi wanafanana na Kuhani au Mlawi watu waliomuona ndugu yao / mtu kutoka sehemu moja kisha wakapita kando wasimsaidie. Labda tunaweza kusema “Kuhani na Mlawi ” walikuwa wakiwahi ibada hekaluni alafu katikati ya njia wanamkuta mkristo mwenzao yupo hoi, hali ya kufa. Wanamuacha huyu wakikimbilia walio wazima kanisani, huku wakidhani wanaenda kwenye “ibada“hali hawajui “ibada” yao wameiacha nyuma maana mtu yule ni ibada kwao! Yamkini ndivyo ufanyavyo hata wewe!!

Ikiwa umepata kitu cha kujifunza, ebu niambie kwa namba zangu zilizopo hapo chini. Na kwa msaada zaidi pamoja na maombezi nipigie kwa namba hizi;

+255 655 111 149/683 877 900/762 414 446.

Namba ya What’sapp ni +255 655 111 149.

Mch. Gasper Madumla.

S.l.P 55051 DSM,TZ.

Beroya bible fellowship church( Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE. 

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page