JIPE MOYO UTAYASHINDA YOTE.
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 3, 2017
- 2 min read
Updated: Sep 5, 2022

“ Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.’’ Yoh.16:33
Siku ya leo Bwana akutaka uwe na amani ndani yake huku tukitambua ya kwamba Yeye Mungu ameushinda ulimwengu kwa kila jambo. Lakini katika hayo yote amekuachia neon moja “ jipe moyo” Neno hili “jipeni moyo” lina maana “ kaza kwa Bwana’’ au lina maana “ msikate tama,endelea kuamini’’Hivyo mimi sijui unapitia katika nini lakini leo napenda nikuambie “ jipe moyo mkuu’’ utayashinda yote.
Kumbuka jambo moja kwamba kila chenye mwanzo kina mwisho wake,yale unayoyaona sasa yana mwanzo wake lakini pia yana mwisho wake. Ninatiwa moyo na mtumshi wa Mungu Musa asemavyo;
“ Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.’’ Kutoka 14 :13-14
Neno “usiogope,simameni tu’’ ni sawa na kusema “jipeni moyo,mtashinda tu’’.Musa aliuona ushindi katika Bwana,ule ushindi wa kuwafutilia mbali wa Misri. Hata leo Bwana akuambia Jipe moyo,atakupigania hao wa Misri wako katika maisha yako wataangushwa nawe hutawaona tena. Mpango wa Mungu kwako ni kukupatia ushindi katika Kristo Yesu. Kumbuka hakuna lisilowezekana kwa Mungu,hata kwa hilo la kwako linawezekana kwa Mungu,ila ujipe moyo tu na utalishinda.
Tendo la kujipa moyo ni tendo linahitaji “uvumilivu’’ Ukiweza kuvumilia kwa Bwana katika hayo/hilo unalopitia basi ni hakika utashinda zaidi ya kushinda. Bwana amekuandalia mpango wa ushindi kwa kuwa Yeye ameushinda ulimwengu. Ulimwengu huu ni ulimwengu uliojaa kila aina ya anasa,lakini ni wakati wako sasa wa kuhitaji msaada wa Mungu ili uweze kutoka eneo hilo.
Hakuna mtu yeyote aliyemtegemea Mungu kisha akafeli. Mungu ameweka ushindi pale utakapojitoa kwake. Lakini siku ya leo ninakutia moyo katika changamoto unayopitia,Mungu yu pamoja nawe wala hajakuacha. Hutakiwi kujihesabia kuachwa na Bwana.
Kumbuka;pendo la Mungu ni kubwa sana katika maisha yako. Wapo watu wanaojikataa na kuona kwamba Bwana amewaacha,lakini leo mimi ninakuambia Bwana yu pamoja nawe. Anza kurejea na kumtegemea Yeye na utauona mkono wa Bwana utakushindia hata katika hilo unalopitia sasa.
Kwa msaada zaidi wa maombi, piga sasa +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments