JIFUNZE KWA JUMBE YAIRO.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 16, 2015
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Ipo miujiza mingi aliyoifanya Bwana Yesu ambayo laiti kama ingeliandikwa miujiza yote katika biblia basi ni dhahili kabisa biblia isingebebeka maana ingekuwa kubwa mno (Yoh 21:25 ). Muujiza mmoja kati ya mingi iliyotendeka,ni huu wa kufufuka kwa binti jumbe. Yapo mambo mengi ya kujifunza katika muujiza huu. Lakini kwa machache tu,tujifunze kwa huyu ndugu Jumbe aliyefufuliwa binti yake na Yesu,Jumbe analojambo la kutufundisha,Biblia inasema;
” Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. ” Mathayo 9:18-19Jumbe aliyemfuta Yesu,alikuwa ndiye yule mtu maarufu,mkuu wa Sinagogi,anayeitwaYairo kwa maana Luka na Marko wanamtaja hivyo. Huyu alikuwa ni kiongozi mkubwa tu,ambaye tunawezakujifunza mambo kadhaa yaliyo ndani yake.
Unyenyekevu
Ni ukweli kwamba ndani ya Jumbe huyu kulikuwa na hali ya unyenyekevu mkubwa wa kukubali kumsujudia Yesu mtu ambaye hakuwa anamjua vyema ingawa amemsikia sikia. Si hali ya kawaida ya kiongozi wa Sinagogi anayejulikana kwenda kumsujudia mgeni asiyemjua,bila unyenyekevu haliwezekani jambo hili. Jumbe alikuwa ni mnyenyekevu,labda kwa sababu alihitaji msaada wa kufufuliwa kwa binti yake. Na hata hapo anatoa picha ya nje kwamba mara nyingine watu wakinyenyekea sio kwa sababu wana moyo huo,bali kwa sababu tu wanataka watatuliwe shida zao,na hili tunaliona likiendelea hata leo. Pale tunapowaona watu wakiabudu si kwa sababu wanampenda na wana haja na Yesu bali kwa sababu wanashinda fulani tu! Wakitatuliwa shida zao huwezi kuwaona tena wakiendelea na ibada!
Imani.
Bila shaka jumbe alimsikia sana Yesu,kusikia kwake kukamjenge imani. Tunayaona maneno yake aliyomwambia Bwana kwa maana asema “ ….Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. ” maneno haya ni ya mtu mwenye imani iokoayo. Kwa maana jumbe Yairo aliamini kufufuka kwa binti yake kupitia Yesu. Ingawa yeye jumbe alikuwa kiongozi wa dini,lakini alitambua kwamba hawezi kufufua isipokuwa Yesu tu awezaye,kwa lugha ya kimaombi ni kwamba,Yairo/jumbe alimpeleka binti yake aliyekuwa amekufa kwa Yesu akijua atafufuka tu. Si jambo dogo hilo la kuipeleka maiti kwa Bwana huku ukiaamini kwamba atafufuka hali ukijua kwamba amekufa kiukweli kweli. Kumbe ni kweli hakuna jambo linaloshindikana kwake aaminiye (Marko 9:23) na hakuna jambo gumu kwa Mungu (Yeremia 32:27)
Ujasiri
Fikiri nafasi ya heshima aliyokuwa nayo jumbe kwenye jamii yake na kwenye Sinagogi zima. Kisha fikiri kukubali mara moja kumsujudia Bwana mbele za macho ya watu wengi. Ujasiri mkubwa ameuonesha,kumbe ujasiri hauogopi macho ya watu,ama watu watakuonaje – lakini jumbe hakikumsumbua hicho,alijivika moyo mkuu akashuka kwa Yesu moja kwa moja bila kushauriana na mtu maana angeliweza kushauliana na viongozi wenzake kwanza,lakini biblia haituambii hivyo,bali alijivika ujasiri wa ajabu. Na kwa ujasiri huo alifanikiwa hata kugeuza safari ya Yesu hatimaye Yesu akaamua kugeuka na kuanza safari ya kwenda nyumbani kwake. Ujasiri ni tendo la ajabu ambalo Yesu alipoliona alipendezwa nalo,wanafunzi wake wakashangaa kitendo hicho!
Kudharau aibu.
Jumbe hakuona aibu ya kushuka kwa Bwana mbele za watu. Nafasi aliyokuwa nayo ilimzuia ili kulinda hadhi yake,lakini aliidharau aibu. “Kama watu watasema basi waache waseme,acha nishuke kwa Yesu,nimwabudu hadharani…” Ni kama vile angelisema hivyo. Kudharau aibu ni jambo jepesi lakini ni gumu kama hujakubali kutoka moyoni. Wale wote walioidharau aibu kwa ajili ya Bwana hakika walipokea mara dufu upako juu ya upako. Leo hii,tunakwama hapo,kwenye aibu tu! hali bado tunashida.!!!! Kwani kitu gani bhana ikiwa utanidharau kwa sababu nimeshuka mbele za Bwana,kwa maana utasema leo lakini usiku utalala na maisha yataendelea mbele kama kawa! Dharau aibu mbele za Bwana,wala usijihesabie haki!
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
Jiunge sasa kwa What’s app group pendwa,tuma neno “ NIUNGE” kwa What’s app namba yetu; +255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments