top of page

JENGA TABIA YA KUTAMKA MIBARAKA KWA WATOTO WAKO MARA KWA MARA.

Na .Mch Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe….

Kwa ufupi…

Ikiwa unaweza kuwalaani watu kwa maneno ya kinywa chako basi ujue unaweza kubariki pia kwa kinywa chako. Ni neno la kuamibiwa kwamba kinywa kina nguvu ya kubariki na hapo hapo kulaani,lakini leo sitaki nizungumze nguvu ya kinywa bali nataka nikufundishe kujenga tabia ya kuwatamkia watoto wako mibaraka hata kama watoto hao ni wachanga,lakini bado unaweza kuanza kuwatamkia mibaraka.

Mara nyingi wazazi wamekuwa wakitamka laana na mabaya kwa watoto wao badala ya baraka. Utakuta mzazi akimwambia mwanaye“lione kwanza,kichwa kama samaki” pasipo kujua kwamba mtoto huyo anaweza akakuwa kama samaki au kupata tabia za kile alichotamkiwa. Ukiwa mzazi ujue una nguvu sana ya kuumba au kubomoa ikitegemea unaachilia nini kwa mtoto au watoto wako. 

Nakumbuka mwanangu alipokuwa akiianza shule ya msingi,hapo mwanzo masomo mengi yalimsumbua kwa sababu ya lugha aliyoikuta hapo shuleni,maana yeye alikuwa akisoma shule za english medium,na nilipofanya uhamisho sasa badala ya kusoma masomo kwa lugha aliyoizoea ya kiingereza ikabidi aanze kusoma kwa kiswahili. Kiswahili kikawa kikimchanganya sana kiasi kwamba cha kufeli masomo yake ingawa alikuwa darasa la kwanza tu. 

Kwa jitihada za mama yake akamtafutia twisheni,akawa akijifunza mengi. Lakini papo hapo nikajijengea utaratibu au tabia ya kumtamkia kufanya vyema na kufaulu. Nikawa nikimwambia maneno haya kila tuombapo “ mwanangu wewe ni kichwa na wala hutakuwa mkia katika Jina la Yesu…” baada ya kufanya mitihani yake akawa mtoto kama wakatikati kati ya watoto mia na. Nikazidi kumtamkia mibaraka ya kufaulu kwenye viwango vya juu.

Hatimaye,katika mitihani yake ya kumalizia mwaka,akafanya vizuri na kuongoza darasa zima,akawa mtoto wa tatu kati ya watoto 175 ya darasa la kwanza. Fikiria kutoka mtoto wa katikati mpaka kuwa wa tatu si jambo dogo! Akawa mtoto wa tatu kwa sababu ya kufungana kimajina isingelikuwa kufungana kimajina yeye ni wa kwanza(maana watoto watatu wamepata alama sawa za kufaulu masomo yote mia kwa mia pamoja na mwanangu)

Nini nataka niseme na wewe sasa;ni kujijengea utaratibu wa kuwaombea watoto wako na “ kuwatamkia mibaraka kwenye masomo au kazi zao”. Ebu tujifunze jambo hili kwa kusoma neno la Mungu; 

“ Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana.Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA.” Mwanzo 5:28-29

Lameki anatufundisha kitu katika andiko hili,maana alipopata mtoto hakunyamaza bali alimsemea baraka akasema huyu mtoto(Nuhu) ndiye atakaye wafariji. Na maneno yale yalikaa mahali pake kwa maana tunaona Nuhu akipata neema machoni pa BWANA ( Mwanzo 6:8).Kile alichokitamka Lameki kama mzazi,kimetimia! Nuhu hakuwa mtu wa kawaida kawaida. Lakini ukimsoma Nuhu maisha yake utagundua kwamba alikuwa ni mtu mkamilifu,lakini haya yote yamekuwa na mwanzo,na huo mwanzo ulianzia kwa matamko ya kibaraka kutoka kwa Lameki mzazi wake.

  1. Sasa sijui kwako,unamtamkia nini mwanao au wanao? Je unawaza kwanza kabla ya kuwatamkia maneno ili ujue maana kamili ya matamko yako? Ebu angalia umejijengea tabia gani juu ya uzazi wako,watoto waliotoka tumboni mwako au kiunoni mwako. 

Jifunze kwa Lameki aliyefaulu kutamka baraka nazo baraka zikawa. Tena jifunze kwangu mimi niliyejijengea mazoea ya kuwaombea watoto wangu na kuwatamkia ushindi kwenye maeneo mbalimbali na hakika ndivyo inavyokuwa katika Jina la Yesu Kristo. Anza leo kuweka utaratibu wa kuwabariki wanao katika Jina la Yesu Kristo,kwa imani mibaraka inakuwa sehemu yao. Ni rahisi kabisa,fanya hivi;

  1. Kila uombapo usisahau kuwaombea watoto wako kwa kuwataja majina yao kamili.

  2. Tangaza kushinda na kufaulu mitihani yao,kuwa vichwa,kufanya vizuri. 

  3. Watolee sadaka ya shukrani kwenye madhabahu mahali unapoabudu,mtolee kila mmoja kwenye bahasha yake huku ukiamini kwamba yote uliyoyaomba umefanikiwa kuyapata.

  4. Watazame watoto wako kama washindi.

Hiki nilichokuandikia ni halisi katika Jina la Yesu Kristo. Lakini inawezekana watoto wako au mtoto wako amefungwa eneo fulani na kweli kabisa unahitaji msaada,basi usisite kunipigia kwa simu zangu zilizopo hapo chini;

Piga sasa kwa +255 683 877 900/655 111 149/762 414 446. 

Namba ya what’s app ni +255 655 111 149.

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page