JE WEWE NI MWENYE WIVU KIASI CHA KUUMIA MOYONI?
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 19, 2017
- 4 min read

Na Mch.G.Madumla
Wivu ni nini?
Wivu ni roho na ni moja ya sehemu ya matendo ya mwilini~ Wagalatia 5:19-20. Hivyo basi ikiwa wivu ni sehemu ya mojawapo ya tabia ya mwilini,tunaweza sasa kufasiri tabia hii kwamba imeletwa na shetani kwa sababu Mungu hakutuumbia wivu. Wivu ni tabia mbaya ya kuhisi uchungu au hasira ndani yako kwa sababu ya mafanikio ya mtu mwingine.
Ukiona unahisi uchungu ndani yako kwa sababu ya ndugu/rafiki/jamaa yako aliyefanikiwa ujue una wivu ndani yako. Watumishi wengi ingawa wameokoka lakini wamejikuta wakiishi ndani ya wimbi hili la wivu. Tena ukiona mwenzako ameinuliwa na Mungu hupaswi kusikia/kuhisi uchungu ndani moyo wako.
Ninamkumbuka mdada mmoja aliyekuwa ni mpendwa,alipoambiwa kwamba shoga yake/rafiki yake amenunua gari,basi akahisi uchungu ndani yake hata akatamka hadharani kwamba “hilo gari alilonunua Joyce najua tu litaharibika,…” Unajua alishindwa kujizuia hata kutamka mabaya juu ya gari ya rafiki yake! Sasa nikajiuliza swali moja kwamba suala la kuharibika limetokea wapi? Ndipo nilipogundua kwamba ni wivu tu ndio uliokuwa unamtafuna!
Kuna aina ngapi za wivu?
Zipo aina mbili za wivu;
Wivu mbaya
Wivu mwema
i) wivu mbaya
Huu ndio wivu unaonyesha wengi kiasi kwamba wengi wanakufa kwa sababu ya wivu. Aina hii ya wivu asili yake ni shetani. Ni hali kupata maangaiko ndani moyo kwa sababu ya fulani aliyefanikiwa. Siku zote wivu wa namna hiyo haumuachi mtu salama. Tunajifunza mifano mingi kwa watu mbalimbali walioangamizwa na roho ya wivu.
Kati ya hao waliteseka kwa sababu ya roho hizi ni Sauli aliyemuonea wivu Daudi biblia inasema, Daudi alipopakwa mafuta tu,roho wa Bwana akaambatana naye na roho mbaya ikamwingia Sauli. Alafu tunasoma; “ Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.” 1 Samweli 18:9
Na hata ukifuatilia maisha ya Sauli yaliishia pabaya kwa sababu ya kupelekeshwa na roho ya wivu. Maana Sauli mara nyingi alikuwa akitafuta kumuua Daudi kwa mkuki,kwa sababu ya ule uchungu aliokuwa akiusikia ndani ya moyo wake. Kumbe tokeo mojawapo la roho ya wivu ni mauti.
Tunaweza kuliona hili kwa ndugu zake Yusufu waliokuwa wamekamatwa na wivu kwa sababu ya ndoto za nduguyao Yusufu. Maana kile kilichopangwa ni mauti itokee kwa Yusufu sababu ya wivu wao (Soma Mwanzo 37 & 38 yote). Yupo tena mtu mmoja aitwae Kaini aliyemua nduguye kwa sababu ya wivu ( Mwanzo 4:5,8) Hivyo unaona kwamba Kaini alimuua Habili nduguye kwa sababu ya matendo yake yalikuwa mabaya ( 1 Yoh.3:12) N.K
Kila amchukiaye nduguye ana roho ya wivu naye ni muuaji ( 1 Yoh.3:15)
Ni lazima ujue kwamba ikiwa kama unamchukia ndugu yako wewe ni muuaji na kweli hapo ndani yako. Wivu ndio unaokusumbua maana yeye mwenye uchungu hata wa kulipa kisasi ni yule mwenye wivu tu. Na ndicho kinachoua watu wengi siku ya leo. Mara nyingi tumeshuhudia hata watumishi kwa watumishi wakiumana madhabahuni kwa maneno ya vijembe dhidi ya wakristo wengine kwa sababu tu ya wivu yaani wakiulizwa kwa mafanikio ya wengine. Tukijua ya kwamba sisi wapendwa kazi yetu ni moja tu ya kuishi katika upendo basi tutawajali na wengine.
ii) wivu mwema.
Huu ni wivu wa kutamani kufanya vizuri kama alivyofanya mwenzako. Siku zote wivu wa namna hii ufananishwa na “ shauku ya moyo” ya kutaka kujifunza kwake aliyefanikiwa zaidi kwa lengo zuri na hata kumuombea mema asingeweza mbele. Mungu wetu kwa kuwapa anatuwazia mawazo ya amani siku zote kutupa tumaini ( Yeremia 29:11),Yeye ni mwenye wivu (Kumb.4:24). Hata Bwana Yesu aliona wivu kwa ajili ya Bwana,akitamani watu wajitokeza zaidi kwa Bwana na sio katika mambo ya mwilini ( Yon. 2:16-17, Zab. 69:9, Eliya naye 1 Wafalme 19:14)
Si watu wengi wenye wivu wa namna hii kwa sababu wengi hawapo kwa Bwana ipasavyo. Yule ajaye kwa Bwana ipasavyo atakuwa na wivu wa namna hii kwa kutamani kufanya vyema kila siku na kutamani kuona kazi ya Bwana inasonga mbele.
Sasa jiulize,Je wewe ni mwenye wivu mwema au mbaya? Je ni mara ngapi unasikia uchungu kwa sababu ya kuona mafanikio ya mwenzako? Je unafikiri utaishia wapi na tabia hiyo?
Nini matokeo ya wivu mbaya?
Kwa mujibu wa neno,wivu mbaya umekuwa na matokeo mabaya sana kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii nzima. Unajua hata taifa linaweza kuingia katika majanga kwa sababu ya wivu wa mtu mmoja tu ambaye akawa kama chanzo cha uharibifu wote. Siku zote uharibifu wa halaiki unaanzia kwa mtu mmoja kisha roho hiyo inasambaa kwa wengine. Na ndio maana mimi sishangai ninapoona watu waligombana kwa sababu ya siasa kwa kuwapa ninajua chanzo chake ni roho iliyoanza kwa mtu mmoja na hatimaye kuenea. Matokeo ya wivu huu ni haya ( haya ni machache tu yale yaliyo makubwa)
Mauti ( wengi wamekua na kuuwawa kwa sababu ya wivu)
Kulipa kisasi ( ni tokeo la wivu)
Chuki na hasira kali ( mwenye wivu si rafiki wa karibu,siku zote ni mtu wa kukimbiwa maana hakuna apendaye chuki. Hasira kali uambatana naye mtu huyo)
Je ni nini dawa ya wivu?
Hapo zamani Mungu alijaribu kuwatengenezea watu wake sheria ya wivu. Lakini hata hivyo haikusaidia mpaka pale alipokuja Yesu kuleta neema. Maana torati ilitolewa kwa mkono wa Musa Bali neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo ( Yoh.1:17). Hivyo basi kwa kuwa Mungu wetu ni upendo basi yoyote mwenye pendo tena akasema katika pendo, hukaa ndani ya Mungu ~ 1 Yoh.5:16.
Hivyo,dawa kamili ya wivu ni upendo wa dhati ( kumbuka ili uweze kuwafikia na pendo una muhitaji Mungu sana kwanza kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako,na akufundishe namna ya kukaa ndani yake ili pendo halisi liumbike kwako.)
Kwa misaada zaidi na maombezi,piga sasa+255 683 877 900
Mch.Gasper Madumla.
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Kommentarer