top of page

JE USAFI WA MAKABURINI NI DHAMBI ?


Mch.Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Wapo waamini,watu waliookoka wenye maswali mengi yasiyokuwa na majibu mpaka leo. Maswali mengine wanaulizwa na watu,mengine hujiuliza wao wenyewe,na moja wapo ya maswali yanayoyendelea kuulizwa ndio hili la leo tunalojifunza,kwamba~Je kusafisha makaburi ni dhambi? Au Je usafi wa makaburini ni machukizo mbele za BWANA?

Awali ya yote,hatuna budi kujua kwamba makaburini ni eneo la ardhi lililotengwa kuzikia miili ya watu waliokufa.( Kumbuka;mwili hutokana na udogo,bali roho hutokana na Mungu,yaani mavumbi kuirudia ardhi na roho kumrudia Mungu – Mhubiri 12:7)

Hivyo kama mwili utairudia ardhi/udongo, hii ina maana- mtu afapo,basi atazikwa ili kukamilisha mchakato wa mwili kuurudia ardhi,na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa. Sasa,kama kuna “kuzika” basi ni lazima kuwepo na eneo la ardhi la kuzikia liitwalo “makaburini”. Na kwa kuwa eneo hilo ni eneo maalumu pa kulazia miili ya wafu,basi ni haki mbele za Mungu lisafishwe na kutunzwa vizuri. Na ndio maana serikali imeweka mamlaka zake za kupatunza mahali pa kuzikia kwa mujibu wa sheria.

Kibiblia suala la makaburi limeelezwa vizuri,kuonesha ni suala la kawaida na ni muhimu sana. Ibrahimu alipokufa,naye alizikwa kwenye shamba/makaburini lililokuwa likitunzwa,(Naye Sara mkewe  alizikwa hapo hapo kabla ya Ibrahimu). Na tangu kipindi hicho tunaona utaratibu wa kutunza maeneo ya kuzikia ukiendelea mpaka leo.  Kwa bahati mbaya leo kumezuka zana ya kupaona makaburini ni kama eneo la majini na mapepo,hivyo walokole wengine huogopa hata kukatisha huko,au kwenda kufanya usafi hali wakidhani kufanya usafi katika eneo hilo ni sawa na kujiungamanisha na wafu!!!! kitu ambacho si kweli. Usafi kama usafi wa makaburini haukuungamanishi na wafu,isipokuwa ibada ya wafu huko makaburini ndio imekatazwa na ni mbaya mbele za Mungu.

Kwa nini uogope makaburi?

Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya Wakristo ambao hawawezi kabisa kuchukua jukumu la kwenda kufanya usafi makaburini. Na kwa sababu hiyo maeneo ya kuzikia hubakia machafu. Sasa,Kwa neema tu,watu wasiookoka ndio wamekuwa kipaumbele ya kutunza maeneo ya kuzikia kwa kusafisha. Hivi unajua sisi walokole hatusafishagi kabisa makaburi,? Yaani ni tofauti kabisa na wengine ambao hawajaokoka! Unafikiri ni kwa nini?

Zinaweza kuwa sababu nyingi zinawafanya watu kuogopa au kushindwa kusafisha makaburi kama eneo la kuzikia,Moja ya sababu ni kwamba tumepokea mafundisho yasiyo sawa na tumeaminishwa vibaya nje kabisa na Neno la Mungu pamoja na ulokole wetu. Kwa maana hakuna shida yoyote kutunza maeneo ya kuzikia kwa lengo la kusafisha. Ikiwa wewe ni mtu wa Mungu,umeokoka na tena umejazwa Roho mtakatifu,hutakiwi kuzuiliwa na mitazamo ya kidunia kwa maana wewe sio wa dunia hii. Jifunze kwa mtu wa haki aitwaye Yusufu wa Arimathaya,biblia inasema;

Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe.Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi,akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.” Mathayo 27:57-59

Biblia inasema kwanza,Yusufu alikuwa ni “mwanafunzi wa Yesu” hiyo ndiyo sifa ya kwanza kubwa,tungelisema leo Yusufu alikuwa ameokoka na kuwa mwanafunzi wa Yesu,kama wewe ulivyookoka,lakini Je u mwanafunzi wa Yesu.( Yaani umekubali kuketi na kuukulia wokovu wako,kujifunza?). Pili Yusufu alikuwa muumini imara asiyeogopa,maana alimwendea Pilato na kumwomba mwili wa Yesu,kisha akauchukua. Ebu cheki jambo hili kwa leo, Wewe unaweza kubeba maiti? mbona unakimbiaga? Kwani kuna shida gani!!!! Jamaa akauchukua mwili wa Yesu kisha biblia inasema akaustili vizuri kwa nguo za gharama,kisha tena “akauweka katika kaburi’

Maana yake ni kama vile aliuzika. Je aliuzika hewani?lah! bali katika kaburi. Kaburi ambalo lilikuwa likitunzwa kwa muda mrefu,ni kaburi jipya ambalo halijawahi kuzikiwa. Lakini nataka uone hapo kwamba kutunza maeneo ya kuzikia sio dhambi!!!  Yusufu alifanya hivyo,na huyu alikuwa ni mwanafunzi wa Yesu. Hivyo Kusafisha makaburi sio dhambi wala sio mbaya,dhambi ni kuwafanyia ibada wafu!!! Unapofanya usafi makaburini,nia yako ni nini? hilo ndio la maana litakalo kuhukumu. Kama unafanya kwa nia ya kutunza maeneo kwa kuyaweka safi ili taratibu za kuzikia ziendelee hiyo sio mbaya,ila kama unasafisha kwa nia nyingine ya kiibada,au kuwakumbuka marehemu na mengineyo,hayo sasa ndio mabaya. Nia yako ni ipi katika kusafisha makaburi?

Kwa maombi na maombezi pamoja na ushauri,usisite kupiga kwa;+255 683 877 900

What’s app +255 746 446 446

Na Mch.Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comentarii


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page