JE MUNGU ANASEMA NAWE, KWA KIWANGO KIPI?
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 10, 2018
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.,
“ Je Mungu anasema nawe kwa kiwango kipi? Je kwa kiwango cha chini,? cha katikati? Au kiwango cha juu? Majibu unayo wew mwenyewe! Nakumbuka ;
Siku moja nilikuwa nipo nyumbani nikicheza na wanangu. Unajua ni hivi;Nikiwa ofisini ni mtu mwingine mchungaji na nikiwa nyumbani mimi ni baba, na nikiwa na watoto mimi ni kana kwamba ni mtoto mwenzao maana ninacheza nao na kufanana nao maana mimi na wao kama tutaendesha magari ya kitoto basi tutafanya pamoja, kama tukiamua kujipikilisha vyakula vya maji na michanga na watoto hapo chini basi wenyewe tunajipikilisha na kuendesha magari ya udongo.; na huo ndio uliokuwa utaratibu wangu.
Siku hiyo nilipokuwa na watoto wangu tukicheza kama ilivyo kawaida,nikaanza kusikia uchovu wa kulala. Nikajilazimisha niendelee kucheza nao, lakini usingizi ulizidi ndipo nikawaacha wenyewe wakicheza nami nikaenda kulala nika utii usingizi “ hahaha usingizi shikamoo 😁😀😁”
Nilipolala ilikuwa mida ya mchana kama saa saba kasoro hivi, gafla Roho mtakatifu akaanza kusema nami kwa namna ya ajabu. Roho akanichukua mpaka eneo la mapambano kisha akanionesha roho mbaya za adui zimepandwa ndani kwangu,nikaanza kupigana nazo, moja ilikuwa mfano wa bomu dogo la mkono lenye nyaya nyingi na ni la moto
kiasi kwamba nilipolishika nikahisi hali ya moto kwenye mikono yangu na nikapambana nalo mpaka nikalitoa nje nikalivunja vunja, nikayarudia na mengine. Wakati huo ndipo nikaona roho hizo mfano wa watu wakija mbio kutoka nje nikapambana nao na kuwashinda. Kisha nikashtuka na mwanangu ndipo aliponiamsha akaniambia “baba amka ukale, chakula tayari… “ nami, nikaamka nikajua ahaa! Kisha nikaomba.
Kitu gani nakueleza hapa! Ni kwamba jifunze kuhusu njia anazotumia Roho mtakatifu kusema na wewe na uzitii. Wakati mwingine Mungu anahitaji utulivu ili aseme na wewe mambo makubwa usiyoyajua! Maono na ndoto ni moja ya njia kubwa anayoitumia Mungu kusema nawe. Je Mungu anasema nawe kwa kiasi gani?.
Watu wengi wamepishana na sauti ya Mungu kwa sababu ya kukosa utulivu na kushindwa kujua namna ya kufanyia kazi sauti ya Mungu. Ukiwa ni mwombaji, jifunze kwamba “ ukimya kuwa ni mojawapo ya njia ya kusema na Mungu” Ukiwa unasikia kupumzika hali upo kwenye maombi usiache kupumzika maana kuna namna Mungu anatafuta aseme na wewe. Tunajifunza kwa Samweli ambaye Mungu alisema naye pale alitulia usingizini ( 1 Samweli 3:1-8)
Ebu angalia, wakati Mungu alipotaka kusema na Petro pia. Kuna wakati alimfanya Petro awe katika utulivu ili amsikilizishe sauti yake ( Soma Matendo 10:9-16). Wale waombaji wanaelewa nini ninazungumza hapa. Kumbuka, si kila wakati wa kuangaika huku na kule labda kimaombi n. k, bali kuna wakati utulivu wako baada ya kuomba sana kutamfanya Mungu akusikilizishe sauti / majibu yako kwa njia Roho wake.
Tangu siku hiyo nimejifunza kumpa nafasi Roho mtakatifu katika ukimya baada ya kuomba nimsikie Yeye anataka nini haswa. Ukimya huu unaweza ukawa katika kutafakari, kutulia kimya peke yako bila usumbufu wa aina yoyote au ukimya unaweza kulala ikiwa unasikia ndani yako kulala, fanya hivyo na Mungu atakushangaza.
Shida kubwa leo ni kwamba umekosa utulivu. Ni kweli unaomba, lakini hauna utulivu na kwa sababu hiyo mengine unayakosa ambayo ni muhimu sana kwako. Kumbuka ; Roho mtakatifu anaposema nawe anakupa agenda ya kuombea. Na ikiwa huna agenda ya kuombea basi mambo mawili yanaweza kutokea; moja unaweza usiombe kabisa , ukajikuta unakaa tu bila maombi lakini pili unaweza ukaomba kweli lakini ukaomba nje ya mapenzi ya Mungu. Ni hatari hii sana!
Ukikosa utulivu kamwe huwezi kuisikia sauti au maelekezo muhimu ya kuombea. Ebu fikiria kama mimi nisingetii na kwenda kulala kama sehemu ya utulivu. Je ningeyajuaje hayo yote yaliyofichika katika ulimwengu wa roho. Unajua Mungu ndiye afichuaye siri zote ( Danieli 2:28)
Bwana Mungu anasema nawe mara nyingi sana, akitumia njia nyingi kuhakikisha unaelewa kwamba ni Yeye ndiye anayesema nawe ili kusudi usiangamizwe. Lakini kwa kukosa kwako utulivu, au kwa kukosa kwako kutafakari kile kinachokutokea mara kwa mara basi unapuuzia!!! Kisha mambo yakitokea, hapo ndipo unastuka na kuanza maombi! Sasa kwa nini usingeliomba tangu mwanzo ili hayo yasitokee? Angalia shughuli zako, zikiwa nyingi kiasi kwamba huna muda wa kutulia na kutafuta kuisikia sauti ya Mungu, basi ujue huwezi kamwe kuisikia lah! Ukisikia ni kwa Neema tu!
Hivi unajua Mungu ni yule yule aliyekuwa akisema na akina Danieli, Ibrahimu, Nuhu? Ni yule yule asemaye sasa na wewe na sisi. Lakini unaweza ukadhani kana kwamba Mungu amebadilika, hapana Mungu hajabadilika bali watu ndio wamebadilika sana. Ebu fikiria watumishi pamoja na wewe mtumishi ambaye hutulii! Katika hali kama hiyo utawezaje kupokea yote kutoka kwa Roho mtakatifu? Ni kweli hali ya maisha sasa imebadilika na unahitajika kutafuta mkate kwa ajili ya familia. Lakini katika yote hayo, umetenga muda gani na Mungu katika faragha.
Unajua sijawahi kuona mafunuo mengi ya Mungu, ya ukweli kwa mtumishi ambaye amekosa utulivu na Bwana! Nataka leo ujiulize, Mungu anasema nawe kwa kiwango kipi? Utagundua anasikia au hausikii kabisa sauti ya Mungu. Lakini si kweli kama Mungu hasemi na wewe. Shida haipo kwa Mungu bali shida ipo kwako katika mkao ulikaa sasa! Sasa moja wapo ya mkao mbaya ni “ kukosa utulivu wa kiroho”
Jifunze machache yafuatayo, yatakuongezea kuisikia sauti ya Roho mtakatifu ;
Hakikisha neno la Kristo lijae kwa wingi ndani yako. Huku ukilitafakari neno hilo.
Jenga shauku ya kutamani kuisikia sauti ya Mungu wakati wote. Hapa ni lazima uwe mwombaji, na waweza kumwambia Roho mtakatifu aseme nawe wakati ulalapo, utembeapo.
Omba Roho mtakatifu akusaidie kufasiri kile asemacho na wewe ( ingawa hili ni somo jingine la Roho mtakatifu)
Epuka mazingira ya dhambi.
Ebu jiulize sasa, Je unampa nafasi ya ngapi Roho mtakatifu kwenye maisha yako? Je ni kweli unaweza ukalala bila kumwabudu Mungu au kuomba? N. K ni muhimu sasa kuitii sauti ya Roho ndani yako ili Mungu aseme nawe. Mimi nataka tusaidiane sana kwenye eneo hili, ebu kama umepata kitu na ndani yako unasikia kumuhitaji Mungu zaidi, basi ebu chukua hatua ya imani unipigie sasa ;
+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments