top of page

JE KUNA TOFAUTI GANI KATI YA HEKALU,SINAGOGI NA KANISA?


1024px-Jerusalem_Modell_BW_2

Mfano wa hekalu la pili la Yerusalemu.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

“Hekalu,Sinagogi na kanisa” haya matatu,yanazungumzia eneo la ibada. Huu ndio mfanano wa hayo matatu,ingawa tofauti ipo kidogo. Tofauti iliyopo ni muda / wakati wa kila moja linapotumika. Mfano Hekalu kipindi cha agano la kale lina maana tofauti kidogo na hekalu la agano jipya,kwa maana hekalu katika agano la kale linazungumzia hasa jengo la ibada lililojengwa kwa mikono ya kibinadamu wakati katika agano jipya hekalu ni mtu yeyote aliye ndani ya Kristo (1 Wakorintho 3:16). Kwa mtazamo huo,labda tuangalie tofauti nyingine za “Hekalu,sinagogi na kanisa” kama ifuatavyo;

  1. Hekalu / Temple

Ilikuwa ni ukumbi uliojengwa kwa kadiri ya vipimo maalumu kwa ajili ya ibada, Hekalu lilikuwa ni takatifu kwa Bwana (1 Wafalme 6:3). Hekalu la Kiyahudi lilibeba maeneo matatu muhimu nayo ni,Ukumbi wa nje,Hekalu au patakatifu,Sehemu ya juu/patakatifu pa patakatifu. Kulikuwa na utofauti kati ya hekalu/patakatifu na sehemu ya patakatifu pa patakatifu,tofauti ya kwanza ni kwamba sehemu ya patakatifu pa patakatifu ilikuwa ni sehemu ya juu zaidi wakati katika hekalu palikuwa chini yake.

Tofauti nyingine ni kwamba patakatifu pa patakatifu ndio ilikuwa sehemu hasa ya kulihifadhi sanduku la agano,na palitenganishwa na pazia kati ya patakatifu na hekalu ( Soma 1 Wafalme sura ya 6 yote). Kuhani mkuu ndiye aliingia patakatifu pa patakatifu mara moja kwa mwaka ( Walawi 16:15-17)

Patakatifu pa patakatifu ni mahali ambapo panaaminika kuwa ndipo Bwana Mungu hushuka na kuigusa dunia. Panaaminika ndipo mahali ambapo Mungu huketi,hivyo kuhuni huingia mara moja kwa mwaka kwa ajili ya kupeleka mahitaji ya watu wake waliopo chini. Kwa sababu kuhani anakwenda kukutana na Mungu,hivyo ilimbidi kwanza ajitakase yeye kwanza kabla ya kuachilia utakaso kwa wengine ambapo watu wote wakimsubilia chini ( Luka 1:8-10 ).

Katika biblia yetu tuisomayo kila siku,inaeleza kuwa Hekalu   lilianzia tangu agano la kale. Mara ya kwanza tunasoma habari za hekalu kupitia kuhani Eli ambaye alikuwa akiketi hekaluni siku zote.( 1 Samweli 1:9 )

( i ) Hekalu katika Jerusalemu ( hekalu katika Uyahudi )

Kwa mujibu wa historia ya Waisraeli,kulipatwa kujengwa mahekalu matatu yaliyojengwa katika nyakati tofauti tofauti (Ingawa kulikuwa na hekalu kama vile Hekalu la Ezekiel,hekalu la Zerubabeli)

  1. Hekalu la Sulemani ~ Mwaka 950 kabla ya Kristo,ambapo hapo baadae hekalu hili liliteketezwa na Wababuloni katika mfalme wake Nebukadreza II mnamo 586 kabla ya Kristo.

  2. Hekalu lingine dogo ~ Hekalu hili lilijengwa mahali hapo hapo mnamo mwaka wa 515 kabla ya Kristo,katika kipindi cha Ezra ndani ya utawala wake mfalme Dario ( Ezra 6:15-16).

  3. Hekalu lililojengwa upya na Herode mkubwa ~ Lilijengwa mnamo kuanzia mwaka wa 19 kabla Kristo baada ya uhamisho wa Babeli

( Uhamisho wa Babeli ni kipindi ambacho Wayahudi walilazimishwa kuishi Babuloni. kwa lugha nyingine ni kwamba Wayahudi walilazimishwa kuishi Babeli,ambayo kwa sasa tunaweza kusema walipelekwa Iraq,sababu magofu ya Babeli yapo katika mji wa kisasa wa Al-Hillah,kando ya mto flati kama 90km kusini mwa Baghdadi).

Hekalu hili liliteketezwa (baada ya uvamizi ) na Warumi katika mwaka 70 baada ya Kristo. Hata hivyo baadhi ya Wayahudi wanaamini kuwa na hekalu jingine pale Yerusalemu kitu ambacho wataalamu wa mambo ya historia wametilia shaka kwamba inaweza kutokea mapigano makubwa baina ya wenye kutaka na wasiotaka hali hiyo sababu katika eneo ambapo hekalu lilipokuwapo kwanza,sasa wapo wenye imani tofauti na Kikristo.

( ii ) Hekalu katika ujio wa Kristo Yesu. – Ujio wa Bwana Yesu,ulihamisha hekalu la kujengwa kwa mikono hata kila aaminie anakuwa ni hekalu ambapo Roho mtakatifu hukaa ndani yake. ( 1 Wakorintho 6:19). Yeye Yesu Kristo ametununua kwa damu yake ya thamani,na sasa tu mahekalu ya Roho mtakatifu.

  1. Sinagogi

Neno hili limetoka katika lugha ya kigiriki ” Sinagoge “ lenye maana ya “ Mkutano” ni tafsiri ya kiebrania ni beit knesset lenye maana ‘“ Nyumba ya mkutano”. Tafsiri ya biblia tunazosoma imetafsiri kuwa Sinagogi ni msikiti,hii ni kutokana na tafsiri ya biblia katika lugha ya kiswahili iliyofanyika huko Zanzibari,ambapo hawakuwa na neno mbadala la nyumba ya ibada. { Katika lugha ya kiebrania neno “ beit “  linamaana “ nyumba” ndio maana hata ukisoma bethsaida “ Nyumba ya mvuvi” au bethsania-Nyumba ya masikini (Soma injili imetajwa sana majina haya )}.

Tofauti iliyopo kati ya Hekalu na Sinagogi ni kwamba,Hekalu lilipitia vipindi vingi na tofauti tofauti hata kuwepo na hekalu zaidi ya moja bali Sinagogi ni sinagogi tu,hatuna masinagogi mengi kama ilivyokuwa hekalu.Hekalu huwa ni jengo kubwa lenye sehemu mbali mbali za ibada,wakati sinagogi huwa ni mkutano tu wa watu katika jengo lisilokuwa na mgawanyo mkubwa. Tena tofauti nyininge ni kwamba;

Hekalu lilikuwa kuanzia agano la kale mpaka agano jipya mfano kuanzia kitabu cha 1 Samweli 1:9,mpaka Ufunuo 21:22- Wakati Sinagogi lenyewe halitajwi katika agano la kale bali agano jipya tu.Mara baada ya uhamisho wa Babeli na kuvunjwa kwa hekalu la pili mwaka 70 tunaona sinagogi likishamili sana.

  1. Kanisa / The Church

Kanisa ni nini?

Kwa mujibu wa neno la Mungu zifuatazo ni tafsiri tano,tafsiri sahihi za maana ya neno hili “kanisa“. Awali ya yote neno hili “kanisa” tunalolitumia leo,lenye chimbuko la lugha ya kiyunani kwa jina la “ Kuriakon” yenye maana ya “ mali ya Bwana ” ndio maana katika Mathayo 16:18 Yesu anasema “ nitalijenga kanisa langu,”  ikiwa na maana kanisa ni mali ya Bwana. Lakini ikumbukwe ya kwamba katika agano neno hili lilitafsiriwa kwa jina la Kiyahudi “ ekklesia” yaani “ watu fulani walioitwa na Bwana,au watu waliotengwa na Bwana”

Hivyo basi;

(i )Kanisa ni mwili wa Kristo – Waefeso 1:22-23

Biblia inaeleza ya kwamba Yeye Kristo ndie kichwa cha kanisa,lakini kanisa ni mwili wake. Neno “kichwa cha kanisa ” lina maana ya “ kiongozi mkuu wa kanisa” . Katika tafsiri hii ya kwanza ni vyema kufahamu kuwa tu viungo vya Kristo kwa kuwa tu mwili wa Kristo. Ni jambo la aibu ikiwa kanisa linaitwa kwa mwili wa Kristo lakini limekumbatia dhambi,Je mwili wa Kristo waweza ukashiriki dhambi? Hapana hauwezi kushiriki dhambi yoyote ile.

(ii) Kanisa ni kusanyiko la waaminio katika Kristo Yesu – (Yoh.10:16)

“  Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” Yoh.10:16 Ikumbukwe kwamba kusanyiko hili la waaminio limepewa jina kondoo waliokusanyika kama kundi pa moja na mchungaji wao. Kupitia andiko hili,Yesu anasema analo kundi jingine ambalo anapaswa kulileta pamoja na kwa kuwa ni mali ya Bwana basi,watamsikia.

(iii)Kanisa ni hekalu/jengo/nyumba ya kuabudia. (Waefeso 2:21-22

Tafsiri hii ni moja ya tafsiri ambayo watu wengi wameijua,kwa maana watu wanapotamka kuhusu kanisa humaanisha kwamba kanisa ni jengo fulani hivi. Kupitia fasiri hii;wanakuwa hawajakosea. Biblia inaeleza pia kwamba;20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 

(iv) Kanisa ni bibi harusi wa Kristo;Waefeso 5:31-32

Ikumbukwe kwamba katika ulimwengu wa roho,kila aliyeokoka na kumfuata Kristo Yesu amefanyika kama bibi harusi. Kwa lugha nyepesi tumefunga naye agano;na ndio maana mtu akimuacha Kristo Yesu kisha akaigeukia miungu mingine basi anaitwa ni mzinzi/amezini. Umewahi kujiuliza kwa nini uitwe mzinzi hali hujazini katika mwili?  ( ufunuo 2:14).

Hivyo tumuonapo bibi harusi basi ni dhahiri yupo bwana harusi na pia kuna harusi yao. Katika ulimwengu wa roho KristoYeye mwana-kondoo ndiye Bwana harusi kwa maana kuna harusi ya mwana-kondoo huko mbinguni ( soma Ufunuo 19:7)

(v) Kanisa ni hekalu la Roho mtakatifu – (1 Wakorintho 3:16)

Pia hekalu la pili ni katika madhabahu sehemu fulani ya kanisa iliyotengwa kwa ajili ya kazi ya Bwana. Madhabahuni pa Bwana,mahali ambapo dhabihu zinapotolewa. Hivyo tafsiri hii inamlenga mwamini mmoja mmoja kuwa ni kanisa ( mwamini ametengwa kwa ajili ya Bwana,huitwa pia ni sehemu ya kanisa kwa sababu moyo wake u madhabahu). Kigezo kikubwa cha kanisa ni uwepo wa madhabahu mahali ashukapo na akaapo Bwana Mungu.

Mkazo wa kanisa.

Kanisa linaweka mkazo kwamba,kanisa ni mali halisi ya Kristo. Kanisa ni la Mungu mwenyewe,mkazo huu unaleta tofauti na mkazo wa hekalu la agano la kale ambalo walilitazama kama mali ya Wayahudi pekee,isipokuwa sasa,Kanisa si mali ya mtu au watu isipokuwa ni mali ya Mungu mwenyewe. Wewe ni kanisa na mimi pia ni kanisa ikiwa kama sote tunamwamini Kristo Yesu na tumempokea,naye amekuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.,Naye Kristo ndiye hasa kichwa cha kanisa (Wakolosai 1:18).

Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900

Na.Mch. G.Madumla

Whatsapp namba+255 746 446 446 .

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page