top of page

JARIBU NA MLANGO WAKE WA KUTOKEA.

Updated: Sep 5, 2022

Kila jaribu kwa mtoto (mpendwa) wa Mungu kuna mlango wake wa kutokea



Kwa ufupi…. ( Fundisho la Jumapili tar. 17.06.2018 at BBFC na mch. G. Madumla)

“ Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.“ 1 Wakorintho 10:13


Katika andiko hili, tunaona mambo muhimu yakitajwa pamoja “Jaribu, uwaminifu wa Mungu, mlango wa kutokea na kustahimili?”. Mambo haya manne ni muhimu kuyafahamu katika maisha yako. Jaribu kwamba ni lazima lije kwako, lakini Mungu ni Mwaminifu kutakuwepo na njia ya kutoka lakini ni sharti uwe mvumilivu ili uweze kustahimili. Lakini andiko hilo hapo juu, lina maana gani haswa? Ebu tujifunze ;-


Jaribu ulilonalo sasa ni la kawaida ya wanadamu, jaribu hilo lipo katika uwezo wako hii ni sawa na kusema jaribu limekupata kwa kadri ya kiwango chako cha imani, kwani unapoongezeka kiimani na jaribu huja kwenye kiwango chako cha imani. Lakini Mungu Ni Mwaminifu, biblia inaposema ya kwamba Mungu ni Mwaminifu ina maana Mungu anaziangalia ahadi zake juu yako kipindi unapopotia jaribu kama sasa unavyopitia. Mungu amekuahidi hatakuacha, Mungu amekuahidi hatakulinda uingiapo utokapo pia n. k Sasa anapoziangalia ahadi zake yeye huitwa ni mwaminifu, ujapojaribiwa yeye hubaki kuitwa ni Mwaminifu maana kuna ahadi zake juu yako.


Ni kweli mpendwa unapitia jaribu, ni kweli upo katika jaribu yamkini ni kubwa, lakini ebu leo ona wema wa Mungu kwamba Yeye ni Mwaminifu pamoja na hilo jaribu atafanya na mlango wa kutokea. Hivi unajua Mungu anajua kwamba unajaribiwa hata sasa, ikiwa ndivyo basi mimi nikutie moyo kwamba upo mlango wa kutoka katika hilo.


  • Ingawa Mungu hamjaribu mtu lakini anaweza akaruhusu ujaribiwe, sio kwa sababu umetenda dhambi, sio kwa sababu umemuacha yeye bali kwa sababu ya kuimarishwa vyema kwenye wokovu, kwa sababu ya kuchongwa vizuri ili baadae uwe mwalimu mzuri kwenye eneo hilo upate kumshuhudia Mungu na uweza wake.


Siku moja, mama mmoja na familia yake walikuwa wapo kwenye maombi. Ilikuwa ni desturi yao ya kuomba kabla ya kulala, siku hiyo wajitakasa wakaomba zaidi na walipomaliza wakaenda kulala. Ilipofika saa kumi usiku shetani, mjaribu akawajia. Na aliwajia kwa njia ya panya, hivyo pakawa na usumbufu wa panya wanaotembea kwenda kulia na kushoto ndani ya dari / paa.


Yule mama akafanikiwa kuamka akamwamsha na mumewe. Wakawa wanawasikilizia wafanye nini, gafla wakasikia sauti kali “ Eeeeh” ilikuwa ni sauti ya binti yao. Wakaenda haraka mpaka kwa binti yao, na walipomuangalia maskini! Alikuwa anaanza kukakamaa utafikili amepigwa na shoti ya umeme.


Sasa, wazo la kwanza walilokuwa nalo ni kumpigia mchungaji awasaidie kwa maombi, kumbuka ni usiku wa saa kumi! Walianza kutafuta namba ya mchungaji fulani hawakuiona, wakachukua simu nyingine ambayo ilikuwa ni simu ya baba napo hakufanikiwa kuona namba ya mchungaji yeyoto. Wakakumbuka kwamba kuna mahali walikuwa wameziandika namba za wachungaji, huko nako hawakufanikiwa kuona namba ya wachungaji. Sasa mtoto anazidi kujigeuza geuza na walipoona wamekosa msaada mahali pa wachungaji, wakajifunga “kibwebwe” / wakajitia nguvu na kuanza kuomba wao wenyewe!


Na kule kuomba kwao kwa imani kukamnyanyua yule binti. Wakamuuliza“ ulikuwa wapi ” binti hajui alikuwa wapi. Wakamuuliza tena,“ unajisikiaje sasa” naye binti akajibu “ vizuri “

Ebu angalia hapo; Mungu ameruhusu wazazi hawa wajaribiwe sio kwa sababu ya kufanya dhambi bali kwa sababu ya kuwafanya wawe waombaji wazuri. Mungu alificha namba za simu za wachungaji,


ili kusudi wao waingie kwenye kuomba na wamaanishe maana laiti kama wangelifanikiwa kupata namba ya mchungaji wasingeliomba wala wasingekaza vizuri.

Kumbe kwa mfano huu, tunajifunza pia kwamba Mungu haangalii wingi wa maneno yako wakati wa kuomba bali huangalia imani yako katika yale uombayo ambayo yanaweza yakawa ni maneno machache tu lakini ndio yakaleta muujiza mkubwa!


Ebu jifunze jambo jingine kupitia mfano huo. Kwamba hata wewe katika jaribu lako, kuna njia ya kutokea lakini Mungu anataka aone jinsi gani utakaza kwake kiimani. Jifunze kwamba kuna wakati Mungu anakuondolea watu fulani unaowategemea ili sasa umtegemee yeye tu, kama wale wazazi waliwategemea wachungaji ingawa kumbe wangeliweza kwenda moja kwa moja kwa Bwana kisha wachungaji waje kama msaada mwingine. Ukiona unaowategemea wakusaidie kwenye jaribu lako wamekimbia, basi ujue Mungu anakwambia umtegemee yeye ili utoke kwa mlango wake.


  • Wakati wa kujaribiwa sio wakati wa kumuacha Mungu wala kulikimbia kanisa.


Je kwa nini unapokuwa na jaribu unakimbia kanisa? Au unaiacha imani? Maana kuna watu ambao mambo yao yakiwabana, na kanisani huwaoni. Ukimpigia simu “ hallow mpendwa, upo wapi maana sijakuona mwezi sasa! “ naye atakujibu “… Yaani mpendwa, mambo yamenibana kweli kweli, yaani napitishwa kwenye majaribu… “ Sasa ikiwa ndivyo, kipi bora ukimbie kanisa au ubakie zaidi kanisani wakati wa mambo yako yanapokubana? Nakuambie ni heri uje tu kwa Bwana kanisani maana hapo ndipo penye mlango wako wa kutokea.


  • Kipindi cha kufurahi ni kipindi hiki kwenye hilo jaribu – Yakobo 1:2


Fikiri, una jaribu la kukaukiwa pesa / njaa. Kwamba nyumbani kwako hakuna hata senti ya kununua unga robo ule ugali bila mboga! Jiko limenuna, kisha watoto na wenyewe wanahitaji ada, mwl wa tuisheni anataka pesa yake maana amechoka kuzungushwa kwa malimbikizo ya madeni ya miezi kadhaa iliyopita na kila unayemwendea akukope, anakujibu “ sina pesa, mambo yangu na mimi ni magumu” watoto wa mjini Dar, Tanzania wanasema “pambana na hali yako” Sasa unafanya nini katika hali kama hiyo?


Biblia inasema nini kwenye Warumi 5:3 “tufurahi katika dhiki pia” najua sio rahisi kufurahi katika shida, dhiki lakini Bwana anasema hapo katika dhiki ndipo mahali Yeye anapatikana! Na ndio maana neno linakuambia ufurahi katika dhiki. Hivi, nikuulize swali; utamwonaje Bwana kwenye kipindi cha raha mahali ambapo hakuna kusumbuliwa? Jibu ni huwezi! Unahitaji dhiki, jaribu ili Bwana aonekane kwako.


  1. Kwenye biblia kuna majaribu makubwa mawili;

  2. Jaribu la shetani kwa Adamu na Hawa ( Mwanzo 3:1-6)

  3. Jaribu la shetani kwa Yesu ( Luka 4:1-13)


Kwa mujibu wa majaribu haya, yapo mambo ya kujifunza siku ya leo kwa sababu na wewe unalo jaribu lako. Kwanza kabisa;

Majaribu yote mawili, shetani amehusika kuonesha yeye ndie mjaribu. Kule kwa Adam nyoka alivaa uusika wa shetani, kwa Yesu pia tunamuona sasa shetani moja kwa moja akimjaribu Yesu. Pili kupitia majaribu haya, shetani ametumia mbinu moja tu ya kutaka kuwaangusha aliyewajaribu. Mbinu hiyo ni “uongo katika kuasi sauti ya Bwana Mungu ” maana kwa Adamu shetani alimwambia Hawa “ mkila matunda, hakika hamtakufa” na neno lilikuwa lisema “ukila utafuka hakika”


Na kwa Yesu kulikuwa na uongo wa kumtaka Yesu aliasi neno la Mungu.

Adamu alipojaribiwa alifeli, Yesu alifaulu. Mojawapo ya sababu kubwa ya kufeli kwa Adamu ni kuruhusu tamaa ingie ndani yake. Sababu katika Mwanzo 3:6. Utaona mwanamke alipoona ule mti wafaa, alitamani kisha akachuma na kumpelekea mumewe nao wakala wote.

Kumbe, unapojaribiwa usije ukaruhusu tamaa kwa namna yoyote kwa maana tamaa ni nguvu mbaya ya kukutumbukiza kwenye shimo wakati wa jaribu.


Nguvu ya tamaa ikichukua nafasi kipindi cha kujaribiwa kwako, ni lazima uanguke! Ukijaribiwa kwenye eneo la mahusiano na mwanamke au mwanaume, ukiruhusu tu kutamani, basi ujue utaanguka na kesho tutakuokotea pabaya! Lakini Yesu ameshinda tamaa, shetani hakumuweza.


  • Mlango wa kutokea kwenye jaribu lako.


Kabla ya kuangalia mlango wa kutokea nisema kwamba,kuna utofauti wa yeye anayejaribiwa akiwa ndani ya Yesu (Ameokoka) na yule anayejaribiwa akiwa nje ya Yesu. Tofauti kubwa ni katika namna ya kustahimili na kutoka kwenye hilo jaribu. Kuna namna ya Kiuungu kwa watu ambao wapo ndani ya Yesu ya kushinda zaidi ya kushinda maana Yesu naye alishinda yote ya ulimwengu huu (Yoh.16:33) Hivyo unapojifunza njia hizi za kutoka kwenye jaribu lako,zitakusaidia ikiwa umempa Yesu maisha yako,umeokoka. Na bado hujachelewa hata sasa milango ipo wazi kwa ijili yako,waweza ungana nami kwa namba hapo chini. Ebu tuangalie mlango wa kutokea katika hilo jaribu lako ;


01.Imani na uvumilivu


– Ukikosa kuweka imani yako kwa Yesu ipasavyo itakuwa ni shida kutoka kwenye jaribu lako. Lakini uvumilivu unahitajika sana, kwa sababu jaribu hilo ni la kitambo tu na linamwisho wake kumbuka “ hakuna jambo lisilo na mwisho”. Hivyo hata katika hilo lina mwisho. Ijapokuwa wewe huoni mwisho wake ni lini, lakini amini kwamba lina mwisho. Hivyo ni lazima ujifunze kuvumilia ukitazamia kuisha kunakuja. Ukikosa kuvumilia utajikuta umeangukia maamuzi yasiyo sahihi! Hata kama umevumilia kwa muda, lakini mimi nakuambia bado, ongeza tena muda mwingine leo!


02. Maombi


Luka 22:40 “ ombeni kwamba msiingie majaribuni” kumbe kuomba kwako ni mlango mzuri wa kutokea. Kwa sababu wakati mwingine ukiomba ni kulikwepa jaribu, yako majaribu yakujiayo kwako kwa sababu hauombi. Lakini ukiomba mengine hayataweza kukujia. Mfano ; chukulia wewe ni muombaji umesimama vyema na Bwana, alafu pakawepo mtu anayetaka akuangushe kimapenzi. Mtu huyo anapokuangalia msimamo wako na Mungu, hukosa nafasi ya kukujia ila ukiacha kuomba tu anapata nafasi na mara anakualika chakula kwenye muda ambao yamkini ungeliomba hata usingelitoka nae out kwenye chakula ambapo atakutega huko!!!


03. Neno / uwe mtu wa neno.-


Neno ndio kila kitu, na ni mlango mzuri sana wa kutokea kwenye jaribu lako. Katika neno utapata maelekezo yote ya namna gani utoke.

Kumbuka,


Mungu yupo pamoja nawe, hajakuacha. Napenda nikutie moyo kwamba hata katika hilo bado kuna wema wa Bwana, naye atakufanyia njia pasipo njia ili utoke maana Mungu ni Mwaminifu sana. Hivyo vyema sana, upate mchungaji ambaye utamshirikisha hayo magumu unayopitia ili aweze kuomba na wewe. Mimi natamani nisikie kutoka kwako ili tuombe pamoja katika majaribu hayo. Unaweza ukanipigia kwa

+255 683 877 900


Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446


Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE. 

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page