top of page

IMARISHA NDOA YAKO (Building a great marriage)~ 03


03. Ambatana na mpenzi wako.

“Kuambatana ” ni hali ya kuwa pamoja na kwa umoja. Kitendo cha kufuatana fuatana kama kumbi kumbi, yaani kwenye mitoko yako pembeni anapaswa awepo mumeo / mkeo na kwenye kufanya maamuzi, mfanye pamoja, huko ndiko kunakoitwa “kuambatana na mwenzako ” unawajua “ kumbi kumbi ” haa! Labda huwajui, kumbi kumbi ni wadudu wanaopatikana pale mvua inaponyesha kwa muda labda mvua imenyesha kwa wiki sasa, hapo utawaona wadudu hawa ambao wana mabawa na hupenda taa hasa wakati wa jioni, unapowasha taa paa! Basi baada ya muda kwenye kipindi cha mvua utawaona wakiizunguka taa. Sasa hawa kumbi kumbi wanasifa ya kufuatana fuatana, ndio maana nimekutolea mfano wake.

Kitendo cha kuambatana na mkeo / mumeo kinaiweka ndoa imara na ndio chanzo kikubwa cha mpenzi wako kufanyika rafiki. Kuambatana ni jambo muhimu sana kwenye ndoa, kwa sababu lisipokuwepo jambo hili, tayari tunaona mwanya wa shetani kupenya na kuivuruga ndoa yako. Ebu fikiria wewe mume laiti kama ungeliambatana na mkeo katika mambo yako uyafanyayo, Je huyo mwanaume wa nje angelitokea wapi hata kumchombeza mkeo? Lakini kwa kuwa upo bize na mambo yako, na mkeo yupo yupo tu, basi watu wanamfuata wa kila aina na hapo adui utumia nafasi hiyo hiyo.

  1. Ukweli, wanaume wengi ni shida kuambatana na wake zao.

Ni wanaume wachache sana tunaoweza kuambatana na wake zetu, bali wengi wanashindwa. Ukichunguza sababu hasa ya wanaume kushindwa kuambatana na wake zao utakuta ni sababu za kijinga jinga, hazina hata maana. Mojawapo ya sababu ni kampani za marafiki zao ambao nao hawana wake zao, hivyo tu! Wakati mwingine wanaume huwadharau wake zao yaani ni hayo tu! Sasa hapo kuna sababu hata moja yenye mashiko? Utakuta baba kasoma soma angalau na marafiki zake wasomi hivi, sasa mke aliye naye hajasoma. Sababu hivyo tu, mwanaume eti hushindwa kutembea na mke wake anaogopa atamwaibisha pale zikianza zile za “ yes, no, offcouse,actually have…. ” basi hujikuta akimwacha nyumbani mkewe.

Moja ya hatari kubwa sana kwenye ndoa yako ni kushindwa kuwa pamoja na mwenzako katika yale uyafanyayo hata kama ikiwa ni huduma ni lazima uwe na mpenzi wako yeye pia ni sehemu ya huduma hiyo ingawa nk wewe ndio ulioitwa. Unawezaje kupanga mambo makubwa kama ya kujenga alafu mwenzako hajui?

Unawezaje kupokea mshahara alafu mwenzako hajui? Unawezaje kununua kiwanja kwa siri alafu mwenzako hajui? Unawezaje kuweka pesa benki alafu mwenzako hajui? Tena hajui hata kama una aacount hiyo benk? Hivi,wewe mtumishi wa Mungu ; unawezaje kwenda kuhudumu sehemu alafu mwenzako hajui? Au unawezaje kushughulika na mambo ya wanawake ikiwa wewe ni mwanaume, mume wa mtu na mwenzako hajui chochote, bali yeye anashangaa ukienda na kurudi kwa wamama, Mhhh!!!? Unawezaje kukopa pesa za vikoba / saccos / benki na umeweka mali mliochuma wote alafu mwenzako hajui? N. K

Lakini hayo ndio mambo uyafanyayo kila siku, Je huko ndiko kuambatana? Mimi nataka nikuambie kamwe ndoa yako haiwezi kuimarika ikiwa unayafanya hayo pasipo mwenzako. Nioneshe ndoa moja iliyokaa vizuri pasipo kuambatana nami nikuoneshe ndoa nzuri yenye muambatano, kisha utashangaa!!!

“Kumambatana” ni moja ya siri muhimu sana ya kuikuza ndoa na kuifanya ndoa kuwa na furaha wakati wote. Ukweli ni kwamba huwezi kufanya maamuzi yaliyo sahihi peke yako bila mwenzako. Na laiti ukifanya hivyo peke yako peke yako, nakwambia kuna siku utakwama tu, na hapo ndipo utaumbuka mtu mzima. Watoto wa mjini wanasema “utadondokea pua😇😇😇” yaani utachemka, Mungu anajua maana ya kukupa huyo mwenzako kwa sababu wewe mwenyewe huwezi.

Tumeshuhudia ndoa zilizovunjika kwa sababu tu ya mambo ya usiri, baadae yalipojulikana wanandoa waliachana, ni mbaya! Ebu jiulize hivi ; Kwa nini umfiche mwenzako? Unapata faida gani kufanya mambo kinyemela? Kwa nini usihitaji ushauri kwake hata kama hajasoma kama wewe, lakini si mwenzako jamani? Nakwambia hivi, katika upumbavu wake, lakini atakushauri jambo ambalo utalikumbuka kwamba ni kweli kabisa! Usimdharau mkeo,umchukulie alivyo naye anaweza sana kuliko wengine wote.

  1. Ukishindwa kuambatana na mkeo / mumeo ujue utawafaidisha watu wengine!! 🍉

Fikiria unamwacha nyuma nyuma mpenzi wako katika mambo yako. Kwa mfano wa moja kati ya hayo niliyokuandikia, labda unajenga kwa siri au una viwanja umenunua kwa siri na kila ukienda kwenye mali zako upo peke yako peke yako tu zaidi sana upo na watu wa nje ( upo na washkaji, majaa fulani hivi hata sio ndugu zako) .

Na bahati mbaya paa!! Umekufa!!!! 😭😭😭 Je mimali yako haijabebwa na wengine? Je hilo jumba ulilokuwa unaweka madirisha halijabebwa na wengine? Mbaya zaidi watoto wako wanakuja kuambiwa baadae sana wakati watu wameshaingia humo, ndio wanaambiwa “ umeona mjengo wenye akili huo? Ulikuwa wa baba yako, lakini sasa ni mali ya wengine!!! ” sasa hata mtoto hawezi tena kudai shauri yako mtu uliyeshindwa kuambatana na mwenzako. Haya mambo yapo, na Mungu hapa anasema nawe katika eneo hili kusudi kuanzia leo uchukue hatua ya kubadilika.

Ndoa imara imejengwa hapa, kwamba mambo yako wewe mume ni ya mkeo na ya mkeo ni yako. Uendako ubavuni yupo mpenzi wako labda isipokuwa ofisini kwako lakini sehemu nyingine yupo huyo kipenzi chako. Hivi unajua mpenzi wako akiwa pamoja nawe hata presha huna, maana unajua chochote kile kinachotokea tutakifanya pamoja, sasa wasi wasi utatokea wapi?

Anza leo kuwa karibu na mpenzi wako na utaona atakavyokupenda kuliko akupendavyo sasa. Unajua ndoa iko hivi, mkiwa ninyi wawili mmekuwa mwili mmoja maana yake wewe ukienda au ukitoka sehemu yoyote, maana yake mwili mmoja ndio unaoenda ah kurudi ni sawa na kuchukua chungwa kulikamua juisi yake kisha ukachanganya na maji, hapo huwezi tena kutenganisha maana vitu viwili vimechanganyika na kuwa kitu kimoja kisichotenganishwa. Na hapo popote juisi itakapopelekwa itakuwa kama kitu kimoja tu, ndivyo wewe na mwenzako mnapaswa kuwa kutembea pamoja, kushauriana pamoja, na mengineyo. Bado hujachelewa anza sasa kufanya hivyo.

Kwa msaada zaidi wa maombi ikiwa kwenye ndoa yako kuna changamoto katika hili, au yawezekana wewe upo tayari lakini tatizo ni mwenzako, nipigie tuombe pamoja na ushauri. Piga sasa kwa namba zilizopo hapo juu.

ITAENDELEA…

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page