IMANI KIASI CHA PUNJE YA HARADALI, NI IMANI YA NAMNA GANI?
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 1, 2017
- 3 min read

Haradali ( na Mch.G.Madumla)
Bwana Yesu asifiwe…
Awali ya yote ni vyema tukajua tafsiri halisi ya neno imani kwa mujibu wa biblia. Biblia imetupa tafsiri nyepesi na rahisi ya neno hili imani,kwamba imani ni kuwa na uhakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana- Waebrania 11:1
Neno “uhakika” ni neno muhimu sana katika maana kamili ya imani. Uhakika ni hali ya kutokuwa na shaka,ni hali ya kuthibitisha jambo ambalo kwa kweli halijaonekana katika macho ya damu na nyama isipokuwa katika roho.
Kawaida ya mtu yeyote ili aweze kuamini jambo anahitaji kuona kwanza,hii ni kawaida ya kibinadamu na ndio maana Tomaso mmoja wa mwanafunzi wa Yesu hakuweza kuamini kufufuka kwa Yesu mpaka apate kuona na kutia kidole chake katika makovu ya Yesu ndipo aweze kuamini ( Soma Yoh.20:25).
Huu ndio mtazamo wakibinadamu. Lakini neno halituambii tuamini kwa kuona kwa macho ya kawaida,bali kuamini katika Roho vitu visivyoonekana wala kushikika kwa macho ya kawaida.Ikumbukwe kwamba imani ni kanuni ya kupokea muujiza,kufunguliwa kwa neno na tena ndio daraja la kila kitu kitokacho kwa MUNGU. Kwa maana pasipo imani huwezi kumpendeza Mungu wako (Waebrania 11:6). Sasa siku ya leo tunahitaji kuyajua hayo;
Punje ya haradali.
Ni punje ndogo ya duara ( small round seed) inayotokana na mmea wa haradali ( mustard plants.) Na mbengu hii kawaida ni ndogo mno kama milimita 1 mpaka 2 katika kipimo cha ukuzaji ; Inataka ifanane fanane na mbegu ya mtama/mtama tunaotumia katika kula. Mbegu ya haradali ina rangi manjano nyeupe na zipo nyeusi hivi. Ipo kwa ajili ya chakula.
Yesu anaizungumzia imani akiifananisha na punje ya haladari,lakini ni nini maana yake? Tunasoma;
“Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.” Mathayo 17:20
Maana ya mfano huu;
Punje ya haradali ni mbegu ndogo kuliko mbegu zote, ambayo inapandwa na kupata samadi/mbolea na maji. Nayo ikipandwa uanza kukua na kuwa kubwa kuliko mboga zote;hatimaye huwa mti hapo badae,tena mti unaendelea kukua na kuwa limti likubwa kuliko zote hata ndege wa angani huja na kujenga katika matawi yake kwa sababu ya ukubwa wake. ( Soma Mathayo 13:31-32)
Imani imefananishwa na na mbegu ya haradali ambayo ni mbegu ndogo yenye kukua na kuongezeka kila siku,hatimaye kuwa kubwa kuliko mbegu zote. Hii ikiwa na maana kwamba,imani inayozungumziwa hapo ni imani ikuayo kila siku hata kufikia katika utimilifu.
Watu wengi wamechanganya maana halisi ya mfano huu alioutoa Yesu katika kuifananisha imani na mbegu ya haradali wakidhani ya kwamba Yesu anataka tuwe na imani kiduchu kama chembe ya haradali. Kumbe Yesu alikuwa akizungumzia imani ikuayo kila siku. Tazama asemavyo Yesu,akawaambia,
“ Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.”
Sasa imani ndogo haiwezi kuamisha mlima! Wala imani ndogo haina matokeo kabisa. Huwezi kuwa na kiwango kidogo cha imani kisha ukafanya mambo makubwa. Siku zote yule mwenye imani kubwa ndio afanyaye mambo makubwa. Jifunze kwa Yesu Yeye mwanzilishi wa imani yetu,alitenda makubwa kwa sababu ya ukubwa wa imani yake.
Jifunze tena mfano huu wa punje ya haradali katika ukuaji wake;
Mbengu ya haradali inatabia ya kukua kwa hatua hadi hatua atimaye mti mkubwa. Leo tungeweza kuifananisha na mti wa mbuyu ambao unaanza kukua kama mchicha,lakini ukiendelea kukua katika hatua zake baadae uwa ni mbuyu mti mkubwa sana kiasi kwamba uwezi kuamini jinsi ulivyoanza kumea maana ulionekana ni mdogo sana.
Imani na yenyewe ina hatua za msingi za ukuaji,kutoka katika udogo kama punje ya haradali hatimaye kuwa mti mkubwa. Si kila imani inaweza kutenda makuu,bali ni kwa ile imani ikuayo kila siku ndio itendayo makubwa. Tunaweza kujifunza jambo hili kwa upana kwa kumuangalia Petro mmoja kati ya mitume wa Yesu.
Imani ya Petro ilikuwa ni imani ikuayo siku hadi siku,maana Petro yule aliyekuwa mvuvi alibadilika taratibu katika imani yake. Ukiangalia imani ya Petro alivyokuwa na Yesu na imani yake baada ya kuondoka kwa Yesu,utagundua imani yake ilikuwa tofauti. Aliongezeka imani zaidi,na hiyo ndio imani mfano wa punje ya haradali.
Kwa maana ilifika wakati Petro aliponya watu kwa kivuli chake tu,Bwana alitumia hata kivuli cha Petro kuponya wagonjwa. Kwa nini? Imani ya Petro ilikuwa kubwa mno tofauti na hapo mwanzo~imani mfano wa punje ya haradali.
Inawezekana unahitaji kujifunza zaidi,au inawezekana unahitaji kuombewa. Basi usisite kunipigia kwa namba hizi +255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Komentáře