top of page

IKIMBIE ZINAA ~ 01.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Ikimbie zinaa / flee from sexual immorality.

Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” 1 Wakorintho 6:18.

Dawa ya uponyaji katika zinaa ni “kukimbia“,Paulo hakuwa mjinga hata aandike hivyo,yeye anajua nini dawa ya zinaa. Lakini vyema ukajihoji kwamba, kwa nini dawa ya zinaa au usalama wa zinaa ni kuikimbia? Na kwa namna gani mtu aweza kuikimbia zinaa? Au kwa nini mkazo wa “kukimbia” umeelekezwa kwenye zinaa tu,na sio kwenye dhambi nyingine? Je hii ina maana zinaa / uzinzi ndio dhambi kubwa kuliko dhambi nyingine? N.k. Ukweli ni kwamba kuna maswali mengi sana ambayo unaweza ukajiuliza hapa,lakini bado jibu litabaki pale pale “ikimbie zinaa” !!!. Dhambi ya zinaa inapelekea / imebeba uharibifu mkubwa sana ukilinganisha na dhambi nyingine,ingawa dhambi zote hukumu yake ni moja tu,kwenye ziwa la moto. Ni vyema ukajua kwamba kama ukizini na mtu,basi hapo utakuwa umejishambulia wewe mwenyewe juu ya mwili wako.

  1. “Mauti” ni moja ya zao la zinaa.

Mauti ni hali ya kifo / hali ya kupoteza uhai. Pale mtu napozini anakuwa amefungua lango la mauti ( inaweza ikawa mauti ya kimwili au kiroho),kwa maana ibilisi hupata nafasi ya moja kwa moja ya kuangamiza chochote akitakacho. Daudi alipozini,kile kilichofuata kama zao / tokeo lilikuwa ni “ mauti” . Maana kwanza,aliua (alimuua Uria mume wa mwanamke aliyezini naye). Na ili kuthibitisha kuwa “mauti” ni zao la uzinzi,nabii Nathani anamwambia Daudi ;

“… BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.” 2 Samweli 11:13. Neno “ hutakufa” linaonesha kwamba Daudi alistahili apatwe na mauti,yaani afe. Lakini kwa neema ya tu ya Bwana hakufa yeye,lakini bado “ mauti” haikumwacha kwa maana mtoto aliyezaliwa katika zinaa alikufa! Hata leo,zinaa / uzinzi umebeba “mauti” ile ile,kama vile Daudi aliua mume wa mtu kwa sababu ya zinaa,ndivyo tunavyoona mauaji yanayoendelea sasa katika uzinzi, lakini mauti inatawala hata katika miamba,tumeona wengi wakiua watoto kwa kutoa mimba maskini,!!!kiumbe kinauwawa bila makosa,maana kiumbe hicho hakijafanya kosa lolote! Lakini mauti haiishii hapo tu bali wakati mwingine“mauti” hutambaa mpaka kwa muhusika mwenyewe. Kwa maana kama aliyezini ni mwanandoa,basi ujue ndoa yake itapigwa na mauti!!!

  1. Kusamehewa utasamehewa ukiomba toba,lakini msamaha wako hautaondoa maovu juu yako.

Daudi alisamehewa,maana Bwana alimwambia “ Bwana ameiondoa dhambi yako…” 1 Samweli 12:13 lakini, bado alipokea malipo ya kazi ya uzinzi alioufanya. Uovu,haukuondoka kwake,wake zake nao waliingiliwa mchana kweupe kama sehemu ya uovu ambao alistahili aupate. Ni kweli inawezekana umeokoka kabisa na hata umeomba toba mbele za Mungu baada ya uzinzi na hakika umesamehewa lakini kupata uharibifu ni fungu lako,kwa kuwa ndio vuno lako la lile ulilolipanda. Kwani hujawahi kuona mtu ambaye ametumia vibaya mwili wake kwa zinaa alipokuwa kijana,na sasa ameolewa au kuoa lakini ndani ya ndoa hakuna mtoto! ( labda Kizazi kimetoka,au kipo lakini hapati tu mtoto kwa miaka na miaka!,na amekwisha samehewa na Mungu). Kumbuka, utavuna ulichopanda ( Wagalatia 6:7)

  1. Uzinzi ni lango la kupigwa na adui zako.

Moja ya nafasi tamu anayoitumia ibilisi kupiga watu ni katika eneo la zinaa / uzinzi. Daudi alianguka ,neno la Bwana linasema “umewapa adui nafasi…” 2 Samweli 12:14. Sasa utaelewa kwa nini wengi wanapigwa na ibilisi, ibilisi anaweza akapiga uchumi,akapiga watoto wako,au akapiga huduma yako. Ni kweli unaweza kumshinda ibilisi,lakini jasho litakutoka mpaka umshinde kwa sababu yeye adui yako anakupiga kwa haki kabisa! Unajua pale unapokosea tu,ndipo unapofungua mlango kwa adui,naye kukupiga atakupiga,sasa mbaya zaidi ikiwa bado unaendelea kuzini,nataka nikwambie kwamba kipigo chake kitakuwa ni kikubwa!!!

  1. Zinaa / uzinzi hupiga kelele

“Kupiga kelele” ni zao la zinaa, kwa maana zinaa ina sauti kuliko unavyoelewa! Hii ina maana popote penye zinaa basi lazima watu wataelewa tu. Uzinzi haufichiki,hata kama mzinzi akijaribu kujificha kwenye nyumba za wageni hali yeye si mgeni,ujue atajulikana tu siku moja na wala hatachukua muda mrefu. Jaribu kufuatilia hili kwa watu ambao wanazini kisha utaona kwamba zinaa hanyamazi,bali itapiga kelele kuwashtua watu kwamba kuna mjamaa anazini!

Daudi alijifungia ndani tena ni mfalme mtu ambaye huwezi kumwona kiurahisi,lakini bado alionekana kutoka kwenye chumba chake cha siri kwa maana Mungu alimwona. Hujawahi kuona mtu anajificha mno akizini,lakini baada ya muda mfupi sana siri zake zinakuja kujulikana? Ndio,Kwa maana huwezi kumficha Mungu, kwa maana kama utazini basi ujue hata hapo utakapoingia ndani ya nyumba ya wageni,jicho la Mungu lipo hata huko likikuona vizuri tu!

Lakini kwa nini zinaa inasumbua sana watu? Kwa nini unazini? Shida ipo wapi? Biblia inasema nini kuhusu zinaa? Unaposoma 1 Wakorintho 6:18 andiko letu la msingi,wewe unaelewa nini? Je, hivi katika madhara yote haya yatokanayo na zinaa,bado unazini? Umewahi kutafakari mwisho wa zinaa ni nini? Ni vyema ukajifunza haya ili uikimbie zinaa!!!

ITAENDELEA…

Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900

Na.Mch. G.Madumla

Whatsapp namba +255  746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page