top of page

IBRAHIMU ALISEMA UONGO ?

Updated: Sep 30, 2022

Mch.G.Madumla.

Na Mch.Gasper Madumla.



Umeshawahi kusoma katika biblia yako hivyo? Wewe unafikirije? kwamba Ibrahimu alikuwa akisema uongo? Lakini tunamuangalia pia Isaka akisema maneno kama hayo kwa mkewe Rebeka,na Je Isaka naye alikuwa muongo kumtambulisha mkewe kuwa ni ndugu yake?( Mwanzo 26:6)


Awali ya yote tufahamu maswala ya “malango” itakusaidia. Kwa mujibu ya masuala ya malango,Abramu alitangulizwa kutajwa kama mzaliwa wa kwanza kwa sababu ya kuwa lango la agano,ingawa yeye Abramu ni wa pili kuzaliwa kwa sababu Nahori ndio kaka mkubwa wa Abramu,( Mwanzo 22:20 – Biblia ya kiswahili imemueleza Nahori kama ndugu yake Abramu,lakini biblia ya kiingereza mfano NIV imemueleza Nahori ni “ brother of Abram“)

Swali letu la msingi linatokea hapa;


“,…Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso;basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai.Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.” Mwanzo 12:11-13


Maelezo hayo aliyoyatoa Abramu kwa Sarai mkewe yalikuwa yalikuwa maelezo ya kulinda uhai wake,kwamba Abramu asije kufa. Abramu anajaribu kujilinda kwa kuukataa ukweli juu ya mahusiano yake na mkewe Sarai. Lakini Abramu amesahau kwamba hata angelisema ukweli bado Mungu angelimlinda kwa sababu Mungu alikwisha kumuambia kwamba “Abramu atafanywa kuwa taifa kubwa,na Mungu atalikuza jina lake” ( Mwanzo 12:2). 


Hivyo isingeliwezekana mtu huyu auwawe akiwa yupo pamoja na Bwana,mwenye kubeba ahadi hizo. Ukweli ni kwamba Sarai ni ndugu yake lakini pia ni mke wake. Hivyo katika mazingira ya utambulisho juu ya Sarai,ilipaswa neno mke litumike dhidi ya neno ndugu. Ikiwa ni hivyo basi ni dhahiri kabisa Abramu alidanganya katika utambulisho wa Sara huko Misri.

Lakini swali la kujiuliza ni hili; “kwa nini mtu wa imani kama huyu kufikia wakati kusema uongo?Je Imani yake ilishuka? Je undugu uliopo kati yake Abramu na Sarai ulikuwaje? N.k Unaweza ukajiuliza maswali mengi katika eneo hili,na inawezekana pia ukakosa majibu yake yote.


Katika maswali kama hayo,ni lazima ujue kwamba Abramu hakuwa Mungu hata asikosee. Katika hali ya kawaida ya ubinadamu aliokuwa nao Abramu,alijikuta akikosea katika eneo hili. Maana ukifuatilia kwa ukaribu utagundua chanzo chake nacho ni “njaa ya mwilini la kabisa pamoja na hofu ya kuuwawa”. Matakwa ya mwili yalimsukuma Abramu kumwambia Sarai aseme uongo;


Hofu aliyokuwa nayo Abramu ilikuwa ni hofu kubwa sana maana alianza kuwa na picha ya kuuwawa na wamisri ikiwa kama atasema ukweli juu ya mkewe Sarai. Kumbe wakati mwingine hofu inakufanya udanganye au kumkosa Mungu wako,hivyo ni vyema ufanyie kazi eneo hili kusudi usitawaliwe na hofu ya aina yoyote ile. Labda sasa tuangalie undugu aliokuwa nao Abramu na Sarai mkewe


01.Undugu wa Abramu na Sarai.


-Kwa upande wa Abramu ambaye aliitwa Ibrahimu ( Ibrahimu  maana yake baba wa mataifa mengi Mwanzo 17:5). Inaonekana wazi kabisa mzee Tera(babaye Ibrahimu) alikuwa na watoto wengine ambao hawakutajwa sababu kulikuwa na desturi za kutowatawahesabu watoto wa kike au wanawake (Jambo hili linaonekana likiendelea hata kwa Yakobo,maana Yakobo alizaa watoto kumi na watatu akiwemo na Dina ambaye ni mtoto wa kike -Soma Mwanzo 30:20,lakini Dina hakuesabika bali wale 12 tu nao wakawa makabila kumi na mbili ya Israeli)


Hivyo Sarai miongoni mwa watoto wa mzee Tera hakuhesabika lakini alikuwa ni mtoto wa mzee Tera. Katika taratibu za Kiyahudi za zamani zile ilikuwa inaruhusiwa kumuoa ndugu yako asipokuwa isipokuwa asiwe ndugu yako wa tumbo moja. Waliluhusu kushiriki baba lakini sio mama. Hivyo inaonekana Sarai alikuwa mtoto wa mzee Tera kwa mama mwingine.

 Kwa hiyo kile kilichokuwa na uzito mkubwa ni “tumbo la mama aliyezaa” .


Na ndio maana hata ukiangalia vile ambayo Mungu aliruhusu kufanya agano imara na Isaka na sio Ishmaeli ingawa wote walikuwa ni watoto wa Ibrahimu ( Mwanzo 17:19-20). Mungu aliangalia agano lake kwamba litapitia katika tumbo la Sara na sio tumbo la Hajiri ingawa mwanaume ni yule yule. Ibrahimu anasema hapa kule alipoenda katika nchi ya Gerari.

Naye kweli ni ndugu yangu, binti wa baba yangu ila siye mwana wa mama yangu, ndipo akawa mke wangu.” Mwanzo 20:12


Ni sawa na kusema Ibrahimu awe anasema hivi“...huyu Sara, ni ndugu yangu kweli sijakudanganya,ni mtoto wa baba yangu aliyezaa na mwanamke ambaye sio mama yangu mzazi. Lakini sasa amekuwa ni mke wangu,ila kusema ukweli ni ndugu yangu pia...”. Huo ndio undugu aliokuwa nao Abramu na Sarai ambaye sasa si ndugu tu ni zaidi ya ndugu maana ni mkewe!

Hata mwanaye wa agano Isaka,naye alioa mdogo wake,ebu angalia hapa;


01.Undugu wa Isaka na Rebeka ;


Abramu na ndugu yake wakajitwalia wake,Jina la mke wa Abramu aliitwa Sarai na jina la mke wa Nahori aliitwa Milka  mtoto wa (binti wa) Harani (Mwanzo 11:29). Biblia inatueleza kwamba mke wa Nahori alikwa ni mtoto wa Harani ndugu yake( Mwanzo 11:26),hii ni sawa na kusema Nahori alimuoa mtoto wa mdogo wake aitwae Harani ambaye alikufa mapema,Harani alimzaa Lutu. Na hapo baadae Nahori alifanikiwa kupata watoto kwa mkewe Milka binti Harani,na mmoja wapo wa watoto wake Nahori ni Bethueli ambaye huyu Bethueli alimzaa Rebeka ( Mwanzo 22:20-23). 


Ibrahimu alipata mtoto kwa Sara akaitwa Isaka. Isaka akamuoa  Rebeka kuwa mke wake,sasa jiulize kwamba Je si kweli Rebeka ni ndugu yake Isaka ingawa pia alikuwa ni mke wake? ( Kwa sababu Isaka alimuoa mtoto wa ndugu yake,angalia hapo ) Ndiposa tunamuona Isaka akimtambulisha Rebeka mkewe kuwa ni umbu lake maana ni kweli ni umbu lake. Hivyo Isaka hakudanganya katika utambulisho huo.


Hapo zamani watu walikuwa wakioana ndugu kwa ndugu tena mara nyingi Bwana Mungu aliwaagiza watu wake wasiende kuoa mbali kwa mataifa bali warudi mpaka nyumbani kwenye asili ile ile kwa kujitwalia mke.( 1 Wafalme 11:1-2,Mwanzo 24:36-38)

Hivyo, ni kweli Sarai alikuwa ni ndugu yake Abramu. Lakini kwa mazingira walioyokuwa nayo,


Abramu alidanganya kusema kwamba Sarai ni ndugu yake maana kwa kusema kule kukamfanya Farao amtwae Sarai awe mkewe,lakini kabla ya kukaribiana Mungu hakuruhusu hayo mazingira na kwa sababu hiyo akampiga Farao na nyumba yake kwa mapigo makuu ( Mwanzo 12:17). Kuashiria kwamba huyo mwanamke ni mke wa mtu.

Je ni nini tunalojifunza? Je tunajifunza tuseme japo kauongo kidogo hivi?


01.Uongo ni roho ya kishetani inayoweza kusambaa. 


Ibilisi yeye ni baba wa huo uongo ( Yohana 8:44). Abramu kama lango alipopitisha uongo huo,ulisababisha na wanawe kutembea katika roho hiyo hiyo Isaka naye alisema uongo kwa Rebeka,alikadhalika Yokobo kwa Isaka. Ifike wakati tusiogope mazingira na tuseme kweli yote ili roho hii tuishinde.


02. Usikubali utawaliwe na hofu


Hofu ndio mlango wa shetani,maana ukiwa na hofu ni lazima utaangukia dhambini na kumkosa Mungu aliyekuumba. Abramu kilichompeleka kumtambulisha Sarai hivyo ni hofu tu! Maana alifikiri kwamba akimtambulisha vyema atauwawa. Uonapo upo chini ya hofu,basi hakikisha unapambana kimaombi ili hofu ikuachie


Na Mch.G.Madumla.

Kwa huduma ya maombezi piga +255 683 877 900.

Kwa namba ya What’sapp ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page