HUYU NDIYE YOSHUA
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 16, 2020
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Huyu ndiye Yoshua,mwanajeshi wa Bwana,na msukuma gurudumu la mafanikio ya Musa ! / The Joshua,Soldier of the Lord and Successor of Moses !
Neno “Yoshua” lina maana ya “mkombozi”,Yesu naye ni Yoshua,kwa maana ndiye mkombozi wa ulimwengu. Kuna mengi ya kujifunza katika maisha ya Yoshua msaidizi wa Musa. Ingawa Yoshua alikuwa ni mpambanaji wa zamani,lakini mpaka sasa tunajifunza upambanaji wake na unatuimarisha katika vita yetu ya sasa dhidi ya falme na mamlaka,wakuu wa giza hili, na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Ukweli ni kwamba simulizi ya Yoshua imeandikwa kwa makusudi ili kutoa picha halisi ya namna ya kupambana hadi mwisho pasipo kukata tamaa na hatimaye kushinda.
Biblia inaanza kumtaja Yoshua kwa mara ya kwanza“ katika vita ” ( Kati ya Amaleki na Israeli – Kutoka 17 :8-9,).Biblia inajaribu kutuonesha kwamba Yoshua alikuwa ni mtu mpambanaji kweli kweli,asiyekopesha mtu! Simulizi yake inaanzia katika vita! Bila shaka kuna mahali alianzia,lakini maandiko hayaelezi mwanzo wake,kwa maana kilichokusudiwa ni kueleza uhodari aliokuwa nao Yoshua.
Maisha yake ya kwanza.
Yoshua alikuwa ni mtoto wa Nuni wa kabila la Efraimu – Hesabu 13:8
Alikuwa akiitwa Hoshea,Musa alimbadilisha na kumwita Yoshua -Hesabu 13:16c (Soma nguvu ya majina)
Ni miongoni mwa wapelelezi 12,waliotumwa kuipeleleza nchi ya ahadi – Hesabu 13:1-2,8
Ni msaidizi wa Musa ( Alipanda naye Musa kwenye mlima Sinai,alimsaidia Musa kujenga hema ya kukutania – Kutoka 24:12-13,33:11)
Wasifu wake wa uongozi.
Aliteuliwa rasmi kwa kupakwa mafuta kama msukuma gurudumu la mafanikio ya Musa – Hesabu 27:18-23
Musa alimvika mamlaka ya kuwavukisha watu wa Mungu kwenda kwenye nchi ya ahadi – Kumb.31:1-8 ( Musa hakuweza kuingia Kanaani,na Yoshua ndiye aliyechukua jukumu la kuongoza watu wa Mungu)
Kwa namna ya kipekee kabisa,akasimama sehemu ya Musa baada ya Musa kufa – Yoshua 1:1-9
Mafuta ya ujasiri wa kuteka yalikuwa juu yake – Yoshua 1 :10-11
Bwana amtaka awe na moyo wa ushujaa na uhodari – Yoshua 1:6
Hata hivyo,Yoshua hakupambana yeye mwenyewe bali Bwana alikuwa pamoja naye. Aliwafundisha askari wenzake juu ya upambanaji,na hatimaye walifanikiwa kuipiga Ai- Yoshua 23-24. Katika upambanaji wake,pia alifanikiwa kuteka “wafalme 31,na ardhi kubwa alitiisha kuwa sehemu yake”. Na baadae katika kipindi chake alifanikiwa kugawanya ardhi miongoni mwa makabila – Yoshua 23:4. Hata hivyo,Mungu alimdhihilishia kwamba yupo pamoja naye katika matukio makubwa kama ifuatavyo;
Maji ya mto Yodani kutindika na kusimama kama chuguu ili kutengeneza njia ya makuhani na jeshi la Israeli kupita – Yoshua 3:14-17
Malaika wa Bwana akimtokea katika vazi la upambanaji – Yoshua 5:13-15
Kuangushwa kwa ukuta wa Yeriko na kusimamishwa kwa jua.
Machache kati ya mengi aliyonayo Yoshua ambayo leo hii ni fundisho ni kama ifuatavyo;
Mtazamo chanya pamoja na imani – Hesabu 14:6-8 ( Wakati watu wengine waliposema “ haiwezekani”,yeye alisema “inawezekana’‘,alikuwa na mtazamo chanya siku zote. Aliona kushinda kila siku)
Ujasiri – Yoshua 10:25 ( Alikuwa ni mpambanaji shujaa na jasiri,alikuwa na moyo wa upambanaji “the spirit of fighting”)
Msikivu na mnyenyekevu – Yoshua 11:15 (Alikubali kuchungwa na Musa,hakuna mahali kwenye biblia tunapoweza kusoma kwamba Yoshua alitofautiana na Musa. Yoshua alikubaliana na Musa katika yote,hali ya utii,usikivu,na unyenyekevu mkubwa sana ilikuwepo kwake.)
Mfanya maamuzi sahihii ya haraka – Yoshua 24:15 ( Hii ni sifa muhimu sana kwa kiongozi. Yeye alikuwa ni mfanya maamuzi yenye tija,kwa haraka pasipo kusitasita)
Hofu ya Mungu – Yoshua 5:14
n.k
Katika siku zake za mwisho.
Yoshua alihakikisha anawatahadharisha Israeli kwamba watembee na Bwana,pia anawaambia kwamba wasije wakachangamana na mataifa wenye kuabudu miungu. Maneno yake ya mwisho yalikuwa ni wosia wenye nguvu.- Yoshua 23-24. Ni viongozi wachache wanaoweza kuacha wosia kwa watu wao. Wengi wanapomaliza kazi zao,basi huondoka pasipo kutoa mwelekeo maalumu. Lakini hata hivyo,Yoshua hakuwa na mtu maalumu aliyemwanandaa kushika nafasi yake.
Hatuji kwa nini hakukuwa na mrithi wake. Baada ya miaka yake 110,Yoshua alikufa na kuzikwa katika mpaka wa urithi wake huko Timnath-sera ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu ( Yoshua 24:29-30)
Hivyo; Kupitia maisha ya Yoshua,naamini kuna kitu umekipata. Ukumbuke maneno yote ambayo Bwana alimwambia Yoshua,maneno hayo ni vile anakwambia wewe leo. Kumbuka ; moja ya nguzo kubwa ya ushindi kwa Yoshua ilikuwa ni “kutafakari neno,na kuliweka neno katika maisha yake halisi”-Yoshua 1:8.
Nguzo hii ni halisi hata sasa! Mafanikio yenye ushindi yapo katika Neno la Bwana katika kutufa na kufanya yale yote aliyokuamuru. Yoshua hakukwama popote kwa maana Neno aliliishi.
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Na kwa huduma ya MAOMBI ushauri na msaada zaidi,piga sasa +255 683 877 900
What’s app namba +255 746 446 446.
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios