top of page

HUKUJA NA KITU DUNIANI,TENA HUWEZI KUTOKA NA KITU.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Kuna siku moja niliona tukio moja kwenye tarevisheni / TV likanishangaza kidogo,lilikuwa ni tukio la mazishi ya mtu mmoja mwenye pesa nchini Nigeria. Mtu huyo katika mazishi yake,watu wa jamii yake wakaamua kumzika na baadhi ya mali zake mfano gari lake. Mimi Sikuelewa!!! Ilikuwa maigizo au ni kweli? Anyway! Wanajua wao. Lakini jambo hili likanipa picha kwamba kuna watu ambao wamewazika wapendwa wao na mali. Yaani wamezifukia mali pamoja na wapendwa wao,

mfano ; marehemu kuzikwa na baadhi ya fedha,au mikufu ya dhahabu n.k . Watu wafanyao hivi wanaamini kwamba marehemu kama amekufa basi aondoke na mali zake alizochuma duniani alipokuwa hai. Hii inatuonesha kwamba watu wa namna hii bila shaka hawajui walifanyalo,au wamesahau kile kilichoandikwa kwenye biblia. Biblia inasema;

“ Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.” 1 Timotheo 6:7-8

Ukweli ni kwamba “ kutokuridhika pamoja na kiburi ” ni tabia ya mwanadamu. Tabia ya namna hii,inakufanya usahau kwamba wewe hukuja na chochote hapa duniani tena utaviacha vyote hapa hapa duniani. Ni vyema ujue kuwa kama ikiwa vitu vyote ulivikuta na utaviacha siku moja upende usipende;basi ni sawa na kusema kwamba vitu vyote havina maana isipokuwa roho yako tu ambayo uko nayo na utaondoka nayo. Katika neno hili la leo,najaribu kukutazamisha mambo muhimu yakupasayo kuyatafuta / kuayaangaikia lakini pia ni kitu gani muhimu cha kukipata.

Laiti kama ungelipata neema ya kusikia kidogo juu ya mahitaji muhimu kutoka kwa mtu wa Mungu wa zama za kale,kwa mfano Paulo mtume aliyetuandikia hayo. Basi ungelishangaa na kile tunachokifanya leo hususani katika utumishi wa leo. Kwa maana ni kweli Paulo alikuwa na mahitaji muhimu na kwa kuwa alikuwa pia ni fundi wa mahema hivyo hakutaka kumwelemea mtu yoyote. Mtu huyu alijifunza kuwa radhi na hali yoyote,alifundishwa kushiba na kuona njaa,kuwa na vingi na kupungukiwa pia. ( Wafilipi 4:11)

Hivyo hakuona haja ya kutafuta mengi kwa ajili yake,bali ni afadhali awe na nguo na chakula tu,nayo yatosha kabisa. Lakini kumbuka; Paulo alikuwa hana maana ya watu wasitafute mali na wabakie makanisani bali maana kuu ilikuwa wakristo wanapaswa kuishi maisha ya kuridhika. Katika utumishi wako,ni heri utamani kupata chakula na mavazi tu na hayo uweze kuridhika nayo. Ukifikia wakati wa kutamani vitu vichache tu kama hivyo,basi uwe na uhakika kwamba Bwana atakupa na vingine usivyoomba,yaani atakuzidishia mara dufu. Lakini leo; hali imebadilika,watumishi hupenda kujilimbikizia mali, hupenda kufanana na wamataifa jinsi walivyo!

Hakuna jambo la utumwa kama kushindwa kulidhika na unachopata! Mtu mwenye tamaa ya kujilimbikizia mali,kamwe hawezi kuridhika. Lakini laiti kama utaelewa kwamba unapaswa kutosheka na unachopokea kamwe huwezi kuwa mtu mbaya. Na ndio maana tunawaona wafanyakazi wengi wa serikali wa kipindi cha Yohana mbatizaji,tena hawa walikuwa ni askari ambao hawakutosheka na mishahara yao

“Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.“ Luka 3:12-14

Shida hii,haikuishia zamani hizo bali ipo mpaka sasa. Kwa sababu wapo baadhi ya watoza ushuru waliokosa uaminifu,na wamejikuta wakitoza ushuru zaidi ya vile walivyoamriwa. Bila kujua kwamba, wizi huo wa kujipatia mali kwa njia isiyo ya halali watahukumiwa siku moja huku wakiziacha mali hizo hapa hapa duniani. Ebu tazama kile Yohana mbatizaji alichowaambia polisi,“ Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.“ Sasa jiulize je hali ipoje leo kwa polisi tulionao ulimwenguni? Bila shaka askari wa kirumi walikuwa wakiwadhulumu watu, walikuwa wala rushwa,watu wasiotosheka na mishahara yao. Lakini ndicho kinachofanyika pia leo kwa askari wa dunia hii!!!! Kumbuka, chchote ulichonacho utakiacha!

  1. Nini kifanyike?

01.Tambua kila ulichonacho utakiacha.

Hivyo hakuna sababu ya kupigania mali au pesa (kwa njia isiyo halali) kwa lengo la kujilimbikizia kwa maana hata ukizipata,utaziacha. Ni vyema umwache Bwana mwenyewe akupatie. Ambapo kama mali au pesa zitakuwa zimepatikana kwa msaada wa Mungu,zitakuwa baraka kwako na sio mwiba.

02. Lidhika na hicho hicho upatacho.

Jambo hili halina maana usitafute pesa bali unazozipata uwe na moyo wa kulidhika. Mfano; wewe ni mfanyakazi umeajiriwa,na mshahara wako ni tshs 500,000/=. Hapo unapaswa kulidhika na mshahara wako,na ufanye kazi kwa bidii. Lah! Sivyo kama hautalidhika,basi ni lazima utajikuta ukiiba,au ukifanya janja janja fulani hapo ofisini,na mwisho wa siku utafukuzwa kazi. Ukumbuke hata hiyo hiyo laki tano uipatayo kuna watu wangependa waipate,hivyo huna budi kutosheka nayo.

03.Ridhika na mambo manyonge,Bwana akupe makuu.

Kati ya vitu ambavyo watu hawataki hata kusikia ni kukubali kuyapokea mambo dhaifu,madogo dogo. Mfano,kukubali kuishi kwenye maisha ya chini,kukubali kupata kidogo. Bali wengi hutaka makuu kuu!!! Lakini hiyo siyo kanuni ya Kiungu. Kwa maana ni vyema kukubali kuishi kwenye maisha ya chini kuliko kutafuta uonekane na watu??? Sasa jiulize kwamba hao watu unaowatafuta wakuone,watakupeleka wapi? Kama si upotevuni ?.

Unajua hakuna raha kama kuishi kwenye maisha yako halisi ya kawaida kabisa,isipokuwa unakula na kuvaa kawaida kanisa. Kwa maana hautasumbuka kujikakamua huku huna pesa!!! Lakini hata kama unazo,bado hakuna raha bali ni fadhaa tu. Nenda kawaulize watu ambao wanajiachia kimaisha,angalia jinsi wanavyokosa hata amani ya kawaida kabisa. Maana wakitembea wanashtuka wakiisi kuna mtu atawadhuru,hivyo itawalazimu kutafuta ulinzi. Sasa hapo je kuna amani kweli? Maana utembeapo,unalindwa!!! Lakini angalia na maisha yao kwa ujumla uone kama wanafuraha ya mioyo yao. Ni vigumu kupata furaha kwa kuwa wengi huwasonga songa.

Kwani ukiwa na sketi na blauzi moja moja au ukiwa na suruali moja na shati moja tu,kuna shida gani? Hata kama nguo zako ni “kauka nikuvae“> yaani nguo ni chache kwa hiyo unafua na kuisubilia ikauke ili uivae,ni sawa kabisa! Ni vyema kutambua jambo muhimu kwamba sio mavazi wala nguo,bali roho yako kuokoka.

  1. Jambo moja ambalo ukifa lazima uondoke nalo.

Nalo ni roho yako, ndio lazima iondoke. Ikiwa ndivyo,basi si sawa kuyaita makabuli “nyumba za milele” kwa maana kinachohifadhiwa ndani ya kaburi ni mwili,ambao utaoza na kufutika. Lakini roho ikaayo milele haifungwi wala kuhifadhiwa kaburini,yenyewe yarudi ilikotoka kwa Mungu ( Mhubiri 12:7). Hivyo ni lazima utafute uhusiano mzuri kati yako wewe na Mungu kabla ya kifo,kwa maana ndicho kitu pekee chenye maana.

Ukiwa umebarikiwa na ujumbe huu basi nifahamishe. Pia ukiwa kama unahitaji msaada zaidi pamoja na maombi,piga sasa kwa : +255 683 877 900/655 111 149/762 414 446.

WhatsApp namba ni +255 655 111 149.

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page