top of page

HISTORIA YA ISRAELI TAIFA TEULE.

Yerusalemu na wikipedia


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi…

“Historia ya Israeli taifa teule” ni historia muhimu sana kuijua ili usomapo biblia yako uwe na ufahamu mzuri. Lengo muhimu la kujifunza historia ya taifa teule la Mungu ni kujua asili na chimbuko la ukombozi wa mwanadamu;maana biblia nzima uliyonayo inazungumzia“ukombozi,wokovu” juu ya watu wote kwa sababu Mungu hapendi hata mtu mmoja apotee,bali sote tufikirie toba ( 2 Petro 3:9,1 Timotheo 2:3-4)Hilo ndilo lengo mama,lakini lengo jingine ni kukufanya wewe mkristo kupata ufahamu sahihi juu ya taifa teule,kitu ambacho wengi leo hawana taarifa kamili juu ya taifa teule la Mungu.

Uchambuzi huu ninaokuandikia leo,haujaegama kuliangalia taifa la Israeli “kisiasa” wala katika mtazamo wa “ kiserikali“kama wengine wanavyochambua. Bali uchambuzi huu unaliangalia taifa hili kwa mtazamo wa Neno la Mungu na ndio maana neno “taifa teule“limetangulia likiashilia kile kinachozungumzwa kinahusiana na Mungu. 

Chanzo cha kila taifa kinaanzia na jamaa ndogo (familia),na chanzo cha jamaa ndogo ni mtu mmoja. Mtu huyu ndie baba au “founder“. Mfano tunauona mji wa kwanza baada ya gharika kipindi cha Nuhu,mji huu ni “Babeli” pia tunauona mji mwingine “Ninawi” ;vyanzo vya miji hii ni jamaa ya watu wachache,kizazi cha Nuhu. Mtu “Nimrodi” yeye ambaye ndiye chanzo kikuu cha miji hiyo ( Mwanzo 10:9-10) Kumbuka pia nchi yote ilienea kutokana na uzazi wa Nuhu baada ya gharika.

Kama ilivyo huko “ Ninawi na Babeli” ndivyo ilivyo kwa taifa la Israeli limeanzia kwa jamii ya watu wachache(familia). Abramu mwenye agano na Mungu ndiye kiini cha taifa la Israeli (Mwanzo 11:2,18:18).Mtu  huyu ambaye alikuwa akiishi katika nchi ya Uru ya Wakaldayo pamoja na Tera babaye na nduguze ali ni Nahori na Harani. Huko Uru ya Wakaldayo ndio Mesopotamia. Neno hili Mesopotamia lilichukua eneo kubwa kati ya mito mikubwa miwili mto Tigris na mto Frati ( maeneo ya Irani na Iraki ya sasa)

Kwa mujibu wa Neno la Mungu,ali ni Tera na nduguze Abramu walikuwa ni waabudu sanamu,isipokuwa Abramu( Yoshua 24:2-3). Mungu alimtwaa Abramu mpaka nchi ya Ahadi ili kusudi afanye naye agano maana kule kwenye nchi ya baba yake kulikuwa na ibada za miungu megeni.

Abramu sasa aitwa Ibrahimu “ baba wa mataifa mengi “.  Sarai aitwa Sara “mama wa mataifa mengi”. Nao wakapata mtoto wa agano Isaka,Isaka akamzaa Isau na Yakobo kwa Rebeka( Mwanzo 25:21-28). Yakobo akawazaa watoto 12 Mwanzo 35:22-26 ( walikuwa ni watoto 13 ikiwa kama Dina-Mwanzo 30:21,lakini kwa taratibu za Kiyahudi wanawake hawakuhesabiwa). Yakobo alipokutana na malaika wa Bwana huko Peniel,akashindana naye mweleka hata alfajiri,naye Yakobo akamshinda. Malaika wa Bwana akambariki,badala ya kuitwa Yakobo sasa anaitwa Israeli ( Mwanzo 32:24-30). Hivyo watoto wake wanaitwa wana wa Israeli.

Wana wa Israeli wakajipata utumwani Misri muda wa miaka 430. Hatimaye Mungu akamuinua Musa na msemaji wake Haruni,Musa ambaye alikuwa ni zaidi ya nabii aliyewatoa utumwani Misri. Lakini hata hivyo Yeye Musa hakufanikiwa kuwaingiza kwenye nchi ya Ahadi isipokuwa Yoshua mwana Nuni na Kalebu mwana wa Yefune kwa sababu ya makosa ya kuupiga mwamba huko Meriba pia kizazi chote hakikuingia kwenye nchi ya Ahadi Kizazi kipya na kina Yoshua na Kalebu ndio waliingia Kanaani (Hesabu 20:1-13,27:12-14)

Baada ya safari ndefu ya kutoka utumwani,hatimaye wana wa Israeli waingia Yeriko mji mkuu wa Kanaani chini ya uongozi wa Yoshua,lakini hata hivyo Yoshua hakufanikiwa kumuandaa mrithi wake kama yeye aligyoandaliwa. Kitendo hicho kilimlazimu Mungu awe ndio serikali kuu. Aina hii ya uongozi uliokosa mtu wa kudumu wa kuongoza hata Mungu mwenyewe kuongoza kunaitwa “Theocracy“. Wana wa Israeli walikengeuka na kusahau yote aliyoyatenda Bwana kwa ajili yao.

Kitendo hicho kiliwafanya kupigwa kila wakati na maadui zao ambao Mungu aliwaachilia kwao. Na hapo ndipo wakajikuta wakiongozwa na “ waamuzi“. Walipomlilia Bwana Mungu,Mungu aliwapatia Waamuzi. Na Waamuzi wapatao 12 ( sita kati yao walikuwa waamuzi wakubwa mfano Deborah,Gideon,Samsoni n.k,na wengine sita walikuwa waamuzi wadogo-Soma kitabu cha Waamuzi chote). Samweli anatajwa kuwa ndio mwamuzi wa mwisho wa Israeli lakini pia ni nabii pamoja na nabii Gadi na Nathani-1 Nyakati 29:29)

Baada ya hapo Sauli mfalme wa kwanza wa wana wa Israeli akipakwa mafuta na Samweli (1Samweli 10:1). Kisha Daudi mfalme,kisha Sulemani.Kwa sababu ya maovu yaliyokuwa yakiendelea,yaliwafanya wana wa Israeli waendelee kupigwa.(Daudi alikwenda vizuri na Mungu ingawa makosa yalikuwepo kwenye ufalme wake kama lile la kulala na mke wa Jemedari wake Uria 2 Samweli 11:1-27)

  1. Kugawanyika kwa Israeli

Sulemani mfalme aliyeiacha sauti ya Mungu na mwishowe akaoa wanawake wengi aliozuiliwa kuingia kwao ( 1 Wafalme 11:1-4). Lakini Sulemani akaingia kwao,nao hao wake wakamgeuza moyo na hapo ndipo BWANA “akamghadhibikia” Sulemani kwa sababu moyo wake umekengeuka. Bwana akaurarua ufalme wake na kumpa mwingine bali hakufanya hayo katika ufalme wake. Kwa sababu ya hadhi na utumishi wa Daudi,Mungu akambakizia makabila mawili yaani “kabila la Yuda na Benyamin” kisha makabila kumi akampa mwingine.

Yale makabila mawili ndio yakaanza kuongozwa na mwanaye Sulemani aitwae “Rehoboamu” baada ya Sulemani kufa ( 1 wafalme 11:29-43) ufalme huu ukakaa pande za chini ya Mesopotamia,ufalme huu unajulikana kuwa ni “ufalme wa kusini au ufalme wa Yuda ” kumbuka Wababeli nao walikuwa kusini mwa Mesopotamia ambapo ndio eneo la Iraki ya sasa.  Bali ya makabila kumi yakaongozwa na “Yeroboamu” yanajulikana kwa jina la “ ufalme wa kaskazini au Israeli“. Waashuru kipindi hicho walikuwa Kaskazini mwa Mesopotamia eneo ambalo sasa ndio Irani.

  1. Uhamisho wa Babeli.

Ni nini maana yake?

Uhamisho wa Babeli ni kipindi ambacho mfalme Nebukadreza II,mfalme wa Babeli aliwachukua mateka watu wa Yuda (Wayahudi)kwenda kuishi Babeli (uajemi) kwa kipindi cha miaka 70. ( 2 Wafalme 24:10-15)

Danieli naye alikuwa utumwani Babeli. Mnamo kama 722 kk Israeli (Ufalme wa kaskazini)uliangukia utumwani kwa Waashuru nao hawakurudi wala hakuna kumbukumbu ya kurejea kwao. Na mnamo 586 kk Watu wa Yuda(ufalme wa kusini)walilazimishwa kuishi Babeli nao wakakaa utumwani miaka 70.

Nabii Yeremia alitabiri haya,kisha akasema “Babeli utakapotimiziwa miaka sabini,nitawajilia na kulitimiza neno langu jema…” Yeremia 29:10 Soma pia Yeremia 20:6. Danieli alipokuwa utumwani huko Babeli,aliposoma nabii hii ya Yeremia akagundua kwamba muda wao umeisha wa kukaa utumwani Babeli.ilikuwa katika kipindi cha kwanza cha utawala wake mfalme Dario mkuu (Danieli 9:2). Hivi unajua umuhimu wa kusoma neno la Mungu? Ebu angalia hapo kwa Danieli aliposoma neno la Mungu akapata ufahamu ya kwamba hawatakiwi tena kukaa utumwani,na ndipo mchakato wa kurejea makwao ukaanza.

Katika kipindi hicho cha mfalme Dario,ndipo alipotoa amri ya kuwarejesha watu kutoka Yuda warudi kwao na waanze kujenga hekalu lao kwa mara ya pili na wayaangaliye mambo yao wenyewe ( Ezra 6:1-4). Wakarejea Yerusalemu kujenga nyumba ya Mungu katika awamu tatu,mojawapo ya awamu ilikuwa ni awamu ya uongozi wa Nehemiah. 

  1. Neno Wayahudi.

Wayahudi ni watu kutoka Yuda ambao wamerejea makwao. Ingawa hapo baadae maana ya neno hili ilipanuliwa lakini bado msingi upo pale pale kwamba ni watu kutoka Yuda. Mpaka habari ya Wayahudi kwenye agano la kale inapoishia,inaishia na watu waliokuwa chini ya utawala wa kiajemi. Malaki ambaye ndiye nabii wa mwisho kabla ya agano jipya,Yeye alitabiri ujio wa mwokozi kama alivyotabiri Isaya ( Malaki 3:1,4:1-6). 

Miaka takribani 400 baada ya agano la kale mpaka agano jipya,iliitwa miaka ya “ukimya“lakini hata hivyo unabii huo wa Malaki pamoja na nabii zilizotolewa kwa ujio wa Yesu zilitimia (Mathayo 1:2). Yesu naye ni uzao wa Daudi mwana wa Ibrahimu naye ni myahudi – Mathayo 1:1. ( maana ndio wale watu waliorudi kutoka Yuda ). Ikiwa Mungu amembariki Ibrahimu na uzao wake,basi ujue taifa hili limebarikiwa. Na ikiwa utaokoka leo,basi ujue nawe ni mmoja kati ya watu waliorudi Yuda yaani Myahudi,utakuwa mrithi wa uzao wa Ibrahimu sawa sawa na ahadi ( Wagalatia 3:29). Ukweli ni kwamba taifa hili limebeba zaidi ya historia.

Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page