HEKIMA NA UTAJIRI WA MFALME SULEMANI.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 8, 2018
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Nilikuwa nikitafakari namna ambavyo Mungu alivyompa Sulemani hekima pamoja na utajiri,nikagundua mambo muhimu machache ambayo nafikiri ni yanakuhusu sana na wewe kwa sababu ninajua unapenda kuinuliwa kwenye eneo la uchumi. Sidhani kama kuna mmoja wetu ambaye anaupenda umaskini,
Bali kila mtu anapenda utele wa mali na mapesa. Ukweli ni kwamba yafuatayo ni mtaji kwako wa kukuinua kiuchumi kipindi hiki maana kama umaskini basi jamani inatosha!!! Kha! Uwe maskini mpaka lini sasa, yatosha – lakini ebu jifunze mambo hayo matatu yaloyofanyika
“ Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.“ 1 Wafalme 3:4-5
Ufunuo muhimu uliopo juu ya moyo wa adili / hekima na utajiri wa mfalme Sulemani unapatikana katika maandiko hayo. Ufunuo huu ni njia au namna Sulemani alivyoinuliwa, ufunuo huo ni;
01. Ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kumbariki Sulemani.
Ilikuwa ni jambo la Mungu mwenyewe kumwinua Sulemani katika eneo la utajiri ndio maana ukisoma maandiko hayo sura yote ya tatu ya 1 Wafalme huwezi kuona kwamba Sulemani aliomba utajiri,lakini Bwana alimpatia baada ya Sulemani kuomba hekima. Hii inatuonesha wazi kabisa kwamba,
Ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kumbariki Sulemani kwa utajiri wa kiwango cha juu kwa maana hakuwahi kuwepo tajiri kama Sulemani wala hakutakuwepo tajiri kama Sulemani. Kumbe kuinua watu kutoka katika umaskini ni tabia ya Mungu mwenyewe. Hivyo,kumbe Mungu hakutuumbia kuwa maskini,bali ni mapenzi yake tuwe na ;
Maisha ya utele.
Utoshelevu,ili tuwasaidie wahitaji
Mali za kuisimamisha kazi ya Bwana, isonge mbele. Tena tuwategemeze watumishi pamoja na injili.
Ni mapenzi ya Mungu usiwe maskini,ndio maana tunasoma hivi “ Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.” 3 Yoh.1:2 Hii ikiwa na maana Mungu anakutaka ufanikiwe rohoni pamoja na afya yako na mambo yako yote,ni sawa na kusema “ Bwana Mungu anakukusudia ufanikiwe,usiwe maskini”.
Ni Mungu ndie aliyepanga kumbariki Sulemani na akambariki Sulemani akawa tajiri, na ni Mungu huyo huyo tunayemwabudu leo,ambaye amepanga kukubariki na wewe leo,Je unaamini hayo? Ufunuo huu ni wa kwanza, kwamba Sulemani alipewa utajiri kwa sababu yalikuwa mapenzi yake. Na ndiye Mungu tunayemtumika hata sasa,kamwe hawezi kubadilika.
02. Sulemani aliambiwa “ omba utakalo nikupe” . (Kuomba)
Ingawa Mungu alikwisha achilia neema ya kufanikiwa lakini bado anakutaka uombe. Hii ni ajabu,kwamba vitu vyote akupavyo Bwana huna budi kuomba ingawa vimekwisha achiliwa kwako. Na ndio maana Bwana alimtokea Sulemani akimwambia aombe ndipo apate hekima. Hekima haikuja kimya kimya,ilikuwa ni lazima Sulemani aombe. Ndivyo hali ilivyo hata sasa,usipoomba huwezi kupokea la ukipokea basi ujue ni neema tu,lakini sio kanuni ya kupokea.
Kumbuka maisha ya utele,utajiri ni sehemu yako ndio maana Yesu ingawa alikuwa maskini kwa ajili yako,ingawa alikuwa tajiri ili kwamba wewe upate kuwa tajiri kwa umaskini wake ( 2 Wakorintho 8:9). Lakini bado kanuni ipo pale pale “ kuomba ” . Kumbe unayo nafasi ukiwa “katika roho” kuomba, na hakika utapata hata kama si leo,lakini utapata tu. Unayo nafasi wewe kukataa umaskini na hatimaye umaskini utakuachia – omba,omba,omba … Kumbuka,Bwana anamwambia Sulemani “ omba” naye akaomba hekima, Bwana akampatia hii ina maana Mungu hujibu maombi ikiwa utamwomba.
03. Bwana alitumia “Neno ” nayo aliyoomba Sulemani yakawa.
Hii ni kuonesha kwamba neno linanafasi yake kubwa sana katika kile utakachoomba. Ni “neno la wakati” kwa mfano,unakataa umaskini, je neno la kipindi hicho linasemaje kuhusu hicho unachokikataa. Neno limefaulu kukidhi kila unachotaka kuomba,hivyo neno litakufunulia namna ya kuomba,nawe utaomba. Kumbuka pale Bwana alipomwambia Sulemani aombe atakalo,naye;
Sulemani aliomba hekima ndipo hapo hapo Bwana naye akatoa neno,ili kufanikisha kile alichoomba Sulemani. Kwa mfano unaomba maisha ya utele, kisha Bwana anasema papo hapo “iwe kama ulivyoomba” na ndivyo alivyofanya kwa Sulemani. Huu ni ufunuo hakika,kwa maana hakuna kitu cha Mungu kitakachofanyika nje ya neno lake. Yeye hueshimu,na ni mwaminifu katika neno lake..
Ikiwa fundisho hili limekubariki,basi ningependa kusikia kutoka kwako kwa kuniandikia msg au kunipigia kwa namba zangu zilizopo hapo juu. Pia kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,waweza kunipigia sasa.
Kwa mawasiliano + 255 683 877 900
Na mch. Gasper Madumla.
What’s app +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments