top of page

HATUA 11 ZA TOBA HALISI.


Mch.Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Awali ya yote,toba haina kanuni maalumu bali kanuni maalumu ni kile kitokacho ndani ya moyo,yaani ikiwa kama unahitaji kuomba toba basi huna budi maombi yako yatoke kwenye moyo na umaanishe kuacha dhambi,uovu,makosa na uasi. Ukimaanisha kwa kuomba ujue,Roho mtakatifu atakusaidia nawe utakuwa mbali na mambo hayo,na inawezekana. Hatua 11 za toba halisi ni hatua ninazozifikiria mimi kama zikifuatwa zinaweza kukusaidia katika toba yako,lakini haufungwi kwenda hatua nyingi zaidi kama ukiweza,kwa maana sio sheria.Hata hivyo ni vyema kujiuliza swali hili;

  1. Nini hasa maana ya kutubu?

Kutubu ni kugeuka au kuacha kile ulichokuwa ukikifanya. Neno kutubu limetokana na neno “toba”  lenye asili ya lugha ya Kiebrania,lenye maana ile ile ya kugeuka. Hivyo unapotubu,ni sawa na kusema unaamua kuacha kosa,dhambi na kuelekea kwenye njia sahihi ambayo ni Mungu. Lakini ikiwa mtu anatubu kisha anarudia yale yale,mtu huyo anakuwa yupo nje na maana halisi ya neno “toba”

“ Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu ” Matendo 2:37-38 ( Soma pia Matendo 26:20)

Angalia kile alichokisema Petro hapo,anasema “tubuni” akiwa na maana “geukeni” sasa na kuiamini injili. Hivyo hii jamii ya watu iliwalazimu waungame/wakiri dhambi zao kwa Bwana na kuomba msamaha kisha waelekee njia nyingine yaani waiamini injili nao watapata ondoleo la dhambi. Ukiuchunguza mstari huo kwa ukaribu,utagundua mambo yafuatayo;

  1. Maarifa ya Neno yalihitajika kabla ya toba,( Neno hata likawachoma mioyo yao)

  2. Waliomba msaada kwa Petro,nini sasa wafanye? (Leo unaomba msaada kwa Roho mtakatifu kabla ya toba yako)

  3. Lipo ondoleo la dhambi ikiwa mtu atatubu kwake Mungu.

.

▪Hivyo basi toba ni tendo la imani la kusamehewa dhambi kupitia damu ya Yesu ( Mathayo 26:28). Kutubu ni kuungama/kukiri dhambi,makosa yako kwa kuomba msamaha kutoka kwa Bwana.

Je neno kuungama ni kutubu?

Kuungama si kutubu kwa maana kuungama ni kukiri dhambi zako. Iko tofauti kati ya kukiri na kutubu,kwa maana anayekiri dhambi anapaswa aombe msamaha katika yale aliyoyakiri,“kuomba asamehewe” huitwa kutubu. Kwa hivyo kama mtu anakiri/anaungama/anafichua uasi wake,dhambi anapaswa aombe toba. Ukiri ni muhimu ili kutambua kwamba kweli kabisa umetenda dhambi,tena bila kujitetea kwa lolote,kama umezini,sema mbele za Bwana mimi nimezini,ili uweze kuomba msamaha. Ukificha ujue unajificha wewe mwenyewe kwa maana Mungu hujua yote ( Yeremia 23:23-24)

Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;” Danieli 9:4-5

Kumbuka;Toba ya kweli ni lazima imuhusishe Roho mtakatifu. Kwa maana Yeye ndie msaada wa kweli,Yeye ndie akukumbushae dhambi zako zote ulizozitenda. Kwa maana ziko dhambi nyingine huwezi kuzikumbuka kwa akili zako za kibinadamu,unamuhitaji Roho wa Bwana akukumbushe na kukupa wepesi wakati wa toba yako.

  1. Kwa nini tunatubu?

Kuna mtazamo ambao hauko sawa siku za leo. Mtazamo wa kufikiria kwamba kama umeokoka basi kamwe huitaji kutubu kwa maana wewe U kiumbe kipya,ya kale yalikwishakupita,na Bwana ameshakulipia deni lote la dhambi zako,huo mtazamo ni sahihi kabisa lakini ni lazima ujue pale unapotenda dhambi ni lazima utubu ndipo usamehewe. Hivyo tunatubu kwa sababu;

01. Mara nyingi,tunadondoka dhambini.

Toba ni njia ya kurejea kwa Bwana. Ikiwa hujaokoka,huna njia nyingine ya kwenda kwa Bwana isipokuwa kwa njia ya toba hasa ile utakayoongozwa. Lakini pia ikiwa kama umekwishaokoka,kuna hali ya kujisahau na kujikuta umetenda dhambi. Hapo unahitaji tena kurejea upya kwa Bwana. Hivyo mazingira yote mawili yanatuhusu sana.

02.Kwa sababu ya kuandaa mioyo yetu. / Kutafuta uhusiano mzuri na Mungu.

Tunapokuwa katika wokovu,tunahitaji mioyo kuwa safi kila siku. Hivyo unapogundua hujakaa sawa katika moyo wako,unapaswa kutubu ili utengeneze na Bwana. Hata kama wewe ni mhudumu wa madhabahu,ni mwiko kupanda madhabahuni ikiwa ndani yako unashuhudiwa dhambi uliyotenda ni sharti uitubie dhambi hiyo kwanza ndipo upande madhabahuni . Kwa maana unapokuwa madhabahuni unakwenda kusema na watu,basi ni vyema ukajitakasa kwanza wewe mwenyewe.

Je ni hatua gani za toba;

01.  Kushukuru.

Ni neno jema kumshukuru Mungu ( Zab.92:1a). Mshukuru Mungu kwa neema aliyokupa ya kutengeneza na Yeye,kwa maana ni Neema tu,kwa sababu wapo waliokufa katika dhambi zao bila kupata neema ya toba. Katika kushukuru,mwambie Bwana asante kwa kunihurumia maana hajakuua katika dhambi zako kwa maana ulipaswa ufe,ila kwa upendo wake amekuacha hai na amekupa nafasi ya kutubu. (Warumi 6:23)

02.Sifa kwa Bwana. (Zab.92:2)

Unapokuwa na muda kabla ya kukimbilia kuomba toba (maana Mungu anajua nia yako) basi tumia muda wako na utangaze fadhili za Bwana. – Itakulazimu usome somo la “ Tabia za Mungu ” fundisho hili lipo hapa hapa kwenye blog hii,litafute hapo juu. Kisha tangaza uweza wa Bwana kwamba Yeye anasamehe,ni mwingi wa huruma,si mwepesi wa hasira n.k ( Yoeli 2 :13). Mara nyingi nyimbo za sifa na kuabudu zinakusogeza karibu uweponi na kukuandaa kwa kutubu.

03.Omba msaada wa Roho mtakatifu.

Ni lazima ujue kwamba wewe pasipo Roho mtakatifu hauwezi kabisa. Maombi yoyote yale yanahitaji Roho mtakatifu ayaongoze,kadhalika hata maombi ya toba yanamuhitaji Roho sana ili ayatawale na kuyaongoza. Kwa maana wewe mwenyewe huwezi kwa kuwa una udhaifu, biblia inasema ;“ Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”Warumi 8:26 Soma pia Yohana14:26

04. Samehe wote waliokuudhi/waliokukosa.

Kumbuka; huwezi kusamehewa dhambi zako ikiwa wewe hujawasamehe wakosa wako. Kipimo cha msamaha kwako ni kuwasamehe waliokukosa ;“Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” Mathayo 6:14-15.

Katika hili ; Tangaza msamaha kwa wote waliokukosa,Kwa njia ya maombi. Ni kweli kimwili watu hao wapo mbali lakini kiroho wapo karibu. Na ikiwa kama unaweza kuwafikia basi jaribu kuzungumza nao kwa kadiri unavyosukumwa moyoni. Waachilie watoke moyoni mwako na wala usiwe na uchungu maana uchungu ni ukuta katika toba yako. Fanya hivyo kwa kumaanisha kabisa,kabla hujaanza kuomba toba katika haja zako binafsi.

05. Ungama /kiri dhambi zako.

Hiki ndio kiini cha maombi yako, biblia inasema“Nalikujulisha dhambi yangu,Wala sikuuficha upotovu wangu.Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.” Zab.32:5. Kama umeiba sema Baba ni kweli nimeiba,ukiua sema nimeua n.k Ni vyema usimfiche Mungu kwa maana Yeye anajua kila kitu,hivyo fungua moyo wako na  kusema kutoka moyoni mwako. La kama hukumbuki dhambi nyingine sema na Roho mtakatifu akukumbushe naye atakusaidia.

06.Tubu sasa na kujutia.

Baada ya kukiri,Sasa Omba msamaha kutoka kwa Mungu,ili Mungu akusamehe kwa yote uliyoyafanya kwa kujua au kwa kutokujua,kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Kwangua dhambi zako zote bila kudharau dhambi yoyote ile. Huku ukijutia dhambi zako kwa kumaanisha. Kujutia ni kuumia moyo wako kwamba kwa nini ulifanya,ili moyo wako uhusike. (soma pia  Zab.38:18,Mathayo 26:75 Petro akijutia dhambi zake) Tumia Zab.51 isome vizuri.

07.Omba rehema mbele za Mungu.Kuomba rehema ni kumsihi Mungu asamehe dhambi,ni tofauti na kuungama,hapa unaomba mapenzi ya Mungu yasamehe dhambi zako.

08.Ialike damu ya YESU,ikaoshe dhambi zako.-Toba yoyote ile ya kweli ni lazima ihusishe damu ya Yesu,kwa maana damu ndio itakasayo dhambi. Damu ni ya muhimu sana katika toba;“kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” Mathayo 26:28,Waefeso 1:7

09. Hakikisha unapata amani ya msamaha kwa kila dhambi unayotubu.

Mfano; unataka kutubia dhambi za aina tatu,chukulia ya kwanza ni dhambi ya wizi,dhambi ya uzinzi,na dhambi ya kiburi. Sasa, unapoanza kutubia dhambi ya wizi,basi hakikisha umeimaliza yote na kupata amani ya msamaha kwa dhambi hiyo ndiposa uingie kutubia dhambi nyingine ya uzinzi nayo ni vivyo hivyo,kisha umalizie dhambi ya kiburi.Haitakiwi kuruka ruka,kwamba umetubia kidogo tu mara umeingia kutubia nyinge tena gafla ukaanza na nyingine, hapana sio hivyo!

10.Weka azimio la kutokurudia dhambi zote ulizotubu kwa kumaanisha.

Ukimaliza kutubu,na upo vizuri kwamba amani ya Kristo Yesu imepatikana basi usisahau kuweka adhimio kwamba“sitarudia tena dhambi hii,Ee Roho mtakatifu unisaidie”“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.“Mithali 28:13

11.Mshukuru Mungu kwa kuamini yote uliyoomba umeyapokea.Kumbuka,ukiomba jambo lolote lile usisahau kumalizia na shukrani kwa Bwana Mungu ukiamini lile uliloliomba limekuwa lako.“Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Mathayo 21:22

  1. Matokeo ya toba halisi.

01.Kuponywa magonjwa. – Toba halisi huleta uponyaji, kwa sababu magonjwa mengi husababishwa na uwepo wa dhambi. Hivyo ikiwa dhambi itaondolewa basi afya urejea.“Akusamehe maovu yako yote,Akuponya magonjwa yako yote,”Zab. 103:3

02. Kuwa na uhakika na uzima wa milele.-Mtu aliyesamehewa dhambi huwa na uhakika na kuupata uzima wa milele kwa sababu sasa amehuishwa tena,kwamba alikuwa amepotea sasa amepatikana.

03.Kupata kibali. –Fikiri ukiwa rafiki wa Mungu,je hutapata kibali? Au fikiria mtu aliyesamehewa dhambi hatakubalika mbele za Mungu. Na akikubalika mbele za Mungu,basi ujue hata kwa wanadamu hukubalika katika kibali kikuu.“ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Mithali 28:13.  Angalia; yule atakaye zificha dhambi zake hatafanikiwa,kinyume chake ni sawa na kusema atakayeziungama dhambi zake atafanikiwa.  

Matokeo mabaya ya mtu asiyetubu.

Ikiwa kama kuna mtu hajatubu iwe ni kwa kutokujua umuhimu au kwa kudharau,yafuatayo yanaweza yakawa ni matokeo mabaya kwake. 

01. Kuwa mbali na uwepo wa Mungu – Ingawa Mungu bado atampenda na kumhurumia,lakini mtu huyo anakuwa mbali na ushirika na Mungu. Hatari yake akifia kwenye dhambi na hajaokoka mbinguni itakuwa ni hadithi kwake,atazuiliwa.

02.Magonjwa na balaa za maisha.- Si kila anaye umwa ametenda dhambi,au si kila ugonjwa ni kwa sababu ya dhambi,lakini magonjwa mengi huletwa na dhambi. Hata ukichunguza asili ya magonjwa ni dhambi maana kabla ya dhambi hakukuwa na magonjwa,ila dhambi ilipoingia na magonjwa,vifo,balaa za kila namna zikaingia. Hivyo kunauwezekano mkubwa kupitia magonjwa. Lakini pia maisha ya mwenye dhambi yamejawa na misukosuko kweli kweli.

03.Kutembea katika laana na kuosa tumaini la uzima wa milele.

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900

What’s app namba +255 746 446 446

Na Mch. G. Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page