top of page

HASIRA.

Hasira hasara! Ona sasa unataka hadi kunyofoa nywele zako! Duh


 Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Hasira ni nini?

Hasira ni hisia kali ndani ya moyo wa mtu zinazomfanya mtu kutenda mabaya. Ni ile namna ya uchungu uliokidhiri wenye kupasuka hata kufanya maamuzi,au kutenda mabaya . Waswahili husema “ hasira ni hasara“,kwa maana matokeo ya hasira ni kutenda mabaya ( Zab.37:8). Tena,hasira ni moja kati ya matendo ya mwilini ( Wagalatia 5:19). Hasira tunda la uharibifu wa shetani. Hasira inakaa moyoni,maandiko yanasema hasira hukuu kifuani mwa wapumbavu (Mhubiri7:9)

  1. Matokeo ya hasira.

01. Kulipa kisasi,pamoja na hasara.

Kila mwenye hasira hujikuta akilipa kisasi kwa kuanzia katika kuwaza kisha kutenda. Kulipa kisasi ni kitendo cha kurudisha ubaya uliotendewa. Mwenye kutawaliwa na hasira hujikuta akilipa mabaya. Unakumbuka wale wana wa wawili wa Yakobo akina Simeoni na Yuda waliolipa kisasi cha kuwauwa wanaume wa Shekemu baada ya kubakwa kwa ndugu yao Dina. Kwa sababu ya hasira iliyopo ndani yao,walijikuta wakilipa kisasi cha mauaji makubwa ( Mwanzo 34 yote,Mwanzo 49:6-7).

Kumbe mtu anayelipa kisasi ni yule ambaye mwenye hasira ulitengeneza uchungu. Hii inaitwa “ hasira iliyolipuka” Kumbe!!! Ebu jiulize sasa,ni mara ngapi umelipa kisasi? Ukiona hivyo ujue ndani yako hakuko sawa,kuna hasira kali. Leo tumeshuhudia mengi yakitendeka kwa kulipa kisasi kama tokeo la moyo wa hasira.

Siku moja nilipokuwa ninakaa na wazazi,nikiwa kijana mdogo tu. Tulishuhudia jirani yetu pale mtaani,akivunja vunja gari ya mumewe akiwa amejaa hasira kali. Inasemekana kuna tabia mume wake alikuwa na tabia mbaya ya kukosa uaminifu katika ndoa,kwa hiyo siku hiyo alikamata kipande cha mbao kama si nondo akapasua pasua vioo vya gari ya mume wake, likavunjika vunjika. Kwa sababu ya hasira tu iliyompelekea kulipa kisasi akidhani anamkomoa mume wake,pasipo kujua yatakayomkuta huko mbeleni.

02. Mauti.

Hasira hupelekea mauti,watu wanauana na wengine wanauwawa. Jifunze kwa Kaini mtu ambaye alikuwa hasira ndani ya moyo dhidi ya ndugu yake Habili. Na tunafahamu nini kilifuata katika hasira ya Kaini,mauti ilikuwa ni tokeo (Mwanzo 4:7-8). Ni vyema kujua kwamba kama upo na hasira basi mauti inakunyemelea,labda uue au uuwawe. Kwa kifupi mwenye hasira ni muuaji tu,kwa sababu uchungu unaompelekesha. Ebu fikiria tu,ikiwa kama mtu akikanyagwa kidogo kwenye daladala tena na kuombwa na msamaha lakini papo hapo bado akitukana na kukunja sura yake!!!! Jiulize mtu huyo,vipi kama akipigwa kidogo hataweza kuua kama ikiwa kakanyagwa kidogo tu anatukana kwa kukasirika. Ni vyema kuoliona hivyo.

  1. Hasira inatoka yao?

Tukumbuke ya kuwa kwa sababu ya dhambi,mwanadamu amejikuta akizaliwa pamoja na hisia kali za kutenda uovu pasipo kufundishwa na yeyote yule. Na ndio maana unaweza ukashangaa kumwona mtoto mchanga akiwa na hasira tena wakati wa kunyonya anang’ata nyonyo huku akiwa amekasilika !! Hapo ndipo utakapojiuliza,kulikoni? Kafundishwa na nani awe na hasira??? Hii ni kuonesha ya kwamba amezaliwa chini ya dhambi.

Biblia inaeleza namna ambavyo hutakiwi kabisa kuwa mwepesi wa hasira. Hata wale viongozi wa kanisani na wenyewe wasiwe wepesi wa hasira ( Tito 1:7). Lakini bahati mbaya leo,tuna viongozi ambao ni wepesi wa kukasirika kinyume kabisa na maelekezo ya neno la Mungu.“Kuna watu jamani wana hasira hao,kwa kununa basi weh! Ndio usiseme.!!!”Watu wa namna hii wanamwitaji Mungu kwa kweli ili watoke kwenye kifungo hicho.

Kumbuka; Hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu ( Yakobo 1:20). Hii ina maana mtu mwenye hasira si rahisi kutenda haki ya Mungu, ( si rahisi kutembea kwenye mapenzi ya Mungu). Hivyo ukimwona kiongozi kanisani mwenye hasira za haraka,ujue hawezi kutenda haki ya Mungu. Ebu jichungu.ze wewe mwenyewe sasa katika eneo hili,Je umekuwa na hasira hata unajuta yale uyafanyayo?

  1. Dawa ya hasira.

Kwa kuwa hasira ni tabia ya mwanadamu na ni tabia ya ndani nayo hujitokeza sana pale shetani anapoichochea,hivyo basi iko dawa yake. Yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu yanayoweza kushughulikia hasira;

01. Kuombewa.

Kuna utofauti kati ya “ kujiombea ” na “kuombewa” ingawa yote ni maombi. Hasira haishughulikiwi kwa kujiombea bali kwa kuombewa na mtumishi wa Mungu kwa sababu hasira na yenyewe ni roho. Hivyo ujapojiombea wewe mwenyewe lakini bado unahitaji mtu mwingine wa Mungu aing’oe hiyo roho. Jambo tumeshuhudia wengi ambao walikuwa wakisumbuliwa na hasira, lakini walipoombewa hasira aliwaachia na sasa wapo huru. Kumbuka; hasira ni kifungo pia.

02. Kutafakari na kuliishi ni Neno.

Ikiwa kama hujampa Yesu maisha yako ( hujaokoka) basi huna budi kuokoka sasa. Kisha ulitafakari neno na kujitahidi kuliweka kwenye maisha yako. Haya ndio mazoezi mazuri ya kiroho,yatakayogandamiza kabisa hasira zako zote.

03. Kabla ya kulipa,kutenda basi tulia kwanza kwa kumwomba Roho mtakatifu akusaidie.

Kuna wakati kama mwanadamu, unakutana na jambo linalokugusa moyo na gafla unajikuta umeumia. Hapo usiwe na haraka ya kurudisha au kutenda chochote,bali tulia na umwombe Roho mtakatifu akueleze ufanyeje. Na ukiona kimya basi endelea kutulia hata kama wenzako watakuona mjinga,ni sawa wakuone hivyo lakini ukawa salama na Yesu wako. Chukulia mwenzi wako wa ndoa,amekutenda na kwa kweli ukiyaangalia matendo yake yanaumiza,lakini hapo hapo weww tulia umlilie Mungu,ukimwomba akusaidue utende kwa hekima inayostahili.

04. Mwone mchungaji.

Kuna wakati mwingine unajaribu kuyafanya yote lakini bado unkosea tu. Basi hapo rudi tena kwa mchungaji na uombe msaada zaidi,maana pengine kuna laana ya kwenu kiasi kwamba jambo ni zito kwako. Ukiwa pamoja na mchungaji, yeye mchungaji atajua namna gani akusaidie.

Jihoji sasa,Je umekuwa mtu wa hasira hasira? Je yupo mtu wako wa karibu amekuwa na hasira? Kama ni ndio,chukua hatua leo,kwa maana ujumbe huu haukukujia kwa bahati mbaya bali unakusudi kwako. Inawezekana upo na mtu wa hasira sana nawe Bwana amekusimamisha kama daraja la kumwokoa huyo. Chukua hatua sasa ya kushughulikia tabia hii katika Jina la Yesu Kristo.

Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezi pia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 683 877 900 

WhatsApp ni .+255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page