HABARI ZA WOKOVU
- Mch. Gasper Madumla
- May 30, 2018
- 5 min read

Na Mch. Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi…
“ Natamani kujua zaidi habari ya wokovu” Ni maneno ya mtu mmoja aliyeokoka juzi juzi tu. Alipopata Neema ya “kuokoka” ndugu zake wakamuuliza kwa nini umeingia kwenye dini mpya? Na kwa sababu hakulifahamu neno bado wala hakujua kuokoka sio dini mpya,hivyo hakuwa na majibu kwa habari ya maisha yake mapya ya kiroho aliyoyapokea. Akanikumbusha mbali kidogo kipindi nami nilipookoka; Maana nami sikuwa na majibu ya kutosha lakini nimeokoka,sasa nakumbuka nilikuwa na rafiki yangu mmoja tuliyekuwa pamoja kwenye dini zetu huko. Yeye mwenzangu alipata neema ya wokovu kabla yangu,sasa na mimi nikawa nikimshangaa vile vile kama wengine wanavyoshangaa maana nami sikuelewa mambo haya hapo mwanzo.
Kile tulichokijua ni kwamba “mwenzetu amepotea,kwa sababu tulifikiri kwamba kitendo cha yeye kuokoka ni kitendo cha kupotea na kuiacha imani ya dini ya baba na mama zetu”. Nami nikashangaa kumuona ameacha kunywa (pombe),ameacha mizunguko isiyokuwa na maana wakati sisi tupo vile vile na mambo ya kidunia hali tunaenda kanisani kila siku. Hapo ndipo nilipojiuliza kwamba “ hivi ni nani aliyepotea kati yetu sisi na yeye?”
Kwa sababu tulikuwa sote dhambini lakini mwenzetu kaacha dhambi hizo tulizokuwa tukizifanya pamoja,lakini cha ajabu sisi ndio tulimuona kapotea eti kwa sababu ameokoka,loh!kumbe sisi ndio tulikuwa tumepotea. Lakini hata hivyo alishindwa kueleza mabadiliko aliyoyapata yalitoka wapi,hakuwa na ufahamu juu ya wokovu lakini aliokoka.Kumbe ni muhimu sana kujifunza suala zima la wokovu,na ni nini hasa neno hili “kuokoka” Au kuna nini cha ajabu tunachokipata tukiokoka? Au kuokoka kuna uhusiano gani na maisha yetu?
Mtu mmoja mshika dini fulani hivi,akasema “nimeokoka katika dini yangu hii hii,wala siachi msimamo wangu. Kwa sababu dini yangu ndio ya ukweli,hata hivyo nikiokoka nikifa nitazikwa na nani?” Ooops! Inashangaza kusikia mtu asemaye maneno kama haya,lakini ni kwa sababu tu hajui wokovu ni nini hasa,na ndio maana leo ni vyema kujua habari ya wokovu zaidi.
Kuokoka ni nini hasa?
“ Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;“ Waefeso 2:8
Kwa mujibu wa andiko hilo tunapata maana ya kuokoka. Kuokoka ni kipawa cha Mungu cha kukutoa hukumuni na kukuungamina na Kristo kwa njia ya imani. Tafsiri hii ni ya kipekee yenye mambo makubwa matatu;
Kipawa cha Mungu.
Kuletolewa hukumuni.
Kuungamanishwa na Kristo kiimani.
• Kipawa cha Mungu
Ni zawadi ya Mungu ya bure “ a free gift of God” hii ikiwa na maana yeyote aliyeokoka hakuifanyia kazi kipawa cha Mungu bali ameipokea kwa neema tu,na hivyo asijisifu. Kipawa cha Mungu hakitokani / hakiji kwa matendo yako mema,wala hakiji kwa sababu umezaliwa kwenye familiya ya dini yako,bali ni neema tu. Neema ni upendeleo wa kiungu usiohustahili. Hivyo utagundua kwamba ikiwa umeokoka,umependwa sana na Mungu kwa maana umepewa zawadi au kipawa cha bure usichokifanyia kazi.
Nilipokuwa nikiwatazama watu wafanyao maovu,ilikuwa ikinishangaza sana. Lakini sasa sishangai hivyo! Maana najua watu hao hawajapewa neema ya wokovu. Ni kweli wengine walipata lakini wakaisukumia mbali,wakaikataa – lakini Mungu aliwapa bure neema. Ukweli ni kwamba kama Mungu angelihesabu matendo yetu ndipo tuokoke,sijui ni nani angeliokoka maana hata mimi nisingeliokoka! Bali ni kwa neema tu. Wakati mwingine “ kipawa cha Mungu “ huitwa “huruma ya Mungu” kwa maana ni huruma za Mungu tu hata kuokoka.
• Kutolewa hukumuni
Kwa sababu ya dhambi na makosa yako,ulikwisha hukumiwa tayari. Hukumu ilikuwa juu yako maana mshahara wa dhambi ni mauti ( Warumi 6:23). Hakuna aliyepona hata mmoja wetu,bali sote tulikuwa hukumuni. Lakini tunapookoka dhambi zetu zimeshughulikiwa na Bwana pale msalabani,na tunatakiwa kuenenda rohoni na wala si mwilini tena. Biblia inasema
“ Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.“ Yoh. 3:18
Ebu angalia kwa umakini neno hilo,linatisha sana. Kwa maana yeyote asiyemuamini Yesu amekwisha hukumiwa,hata kama anajitahidi kwa mambo ya kidhehebu ila asipookoka na kuiweka imani yake kwa Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake,ujue amekwisha hukumiwa. Hii ni hukumu ya kwanza na ni kubwa! Katika hukumu hii;matendo mema hayatakuwa na nafasi yoyote ya kukupa uzima wa milele.
• Kuungamanishwa na Kristo kiimani.
Kila aliyeokoka amepewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu ( Yoh.1:12). Hii ina maana kwamba kuna nguvu iliyoachiliwa na Mungu ya kufanyika mtoto wa Mungu baada tu ya kuokoka. Kazi yaKufanyika mtoto wa Mungu inafanywa na Roho mtakatifu. Na kwa sababu umezaliwa upya,wewe ni mali ya Mungu. Mungu anapokutazama anamuona Kristo ndani yako. Hivyo tunaposema “kuungamanishwa na Kristo kiimani ” tuna maana ya kuwa kuwa na Kristo pamoja,lakini yote hutegemea imani yako kwa Yesu. Na ndio maana huna budi kumuamini Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Kuokoka kunatambulika kwa majina tofauti,kama;
Kuzaliwa mara ya pili ( Yoh.3:3)
Kufanywa upya / Kumwamini Yesu / Kuweka imani yako kwa Yesu/ Kuwa kiumbe kipya ( 2 Wakorintho 5:7)
Hatua za wokovu.
Kuhesabiwa haki ( Justification)
Mchakato wa utakaso ( Santification)
Utakatifu (Glorification)
01. Kuhesabiwa haki.
Mtu mmoja alikuwa amehukumiwa kwa mujibu wa sheria ya jamuhuli ya muungano wa Tanzania. Siku hiyo ya hukumu kulikuwa na mambo mawili aliyotakiwa muhukumiwa alitakiwa kuyafanya; moja ni kulipa Tshs milioni 10 au pili aende jela miaka nane ikiwa kama atashindwa dhamana hiyo. Na yule mhukumiwa kwa kweli hakuwa na kiasi kikubwa cha pesa namna hiyo,hivyo kwa mujibu wa sheria anatakiwa aingie jela miaka nane. Lakini hakimu alipomtazama alimuhurumia sana,na kusema “Kwa huruma zangu nitamlipia deni / pesa hii ili asiingie Jela asije akafa maana mbona ni mzee sana”
Alichokifanya hakimu sio kufuta kosa la mhukumiwa bali ni kulipa deni lake ili adhabu kubwa yote aibebe hakimu. Hakimu hana uwezo wa kufuta kosa bali kubeba kosa. Hivyo kwa huruma,akamlipia deni kama dhamana kubwa ya kiasi cha pesa na yule mhukumiwa akatoka akishangilia. Si kana kwamba mhukumiwa alifanya jitihada yake ili alipiwe deni bali ilikuwa ni huruma tu ya hakimu! Mfano huu ninaufananisha na “kuhesabiwa haki”
Wewe mwenye dhambi ulikwisha hukumiwa tayari kama mshahara wa dhambi zako,lakini Yesu kwa huruma zake tu,akasimama kama hakimu na akakulipia deni lako. Lakini hakufuta kosa lako sababu hukumu lazima ifanyike sawa sawa na kosa,bali ghadhabu ya Mungu Yesu akaibeba yeye kana kwamba wewe hukutenda kosa!
Neno “ kuhesabiwa haki” ni msamiati wa lugha kisheria kwamba mwenye kesi amepewa haki ya kuwa huru dhidi ya kifungo kilichokuwa kikimsubiri. Msamiati huu hutumiwa mara nyingi kwenye mambo ya kimahakama,kusema kwamba kesi imekwisha amliwa na kumuweka huru mkosaji. Tangazo la kumuhesabia haki kwa mkosaji linafanywa na hakimu mwenye mamlaka husika baada ya mahakama kujiridhisha kwenye vigezo vyote na kuona ni haki kwa aliyekosa kuwa huru kwa mujibu wa sheria. Hivyo kuhesabiwa haki sio suala la mkosaji bali ni suala la hakimu.
Katika upande wa kiroho; “kuhesabiwa haki” ni kazi ya Mungu mwenyewe kutuhesabia haki bure pale tunapookoka. Ni huruma za Mungu tu,kukuhesabia haki bure si kwa matendo yako,bali kwa imani tu. Biblia inasema;
“ kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;“ Warumi 3:23-24
Kwa neema,kwa njia ya ukombozi,umehesabiwa haki. Hii ina maana gani kwako? Ikiwa umempokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wako,basi ujue dhambi zako hazikumbukwi na Mungu anapokuangalia anakuona ni mwenye haki,uliyenunuliwa kwa bei ya thamani ya damu ya mwana-kondoo wa Mungu. Si kazi yako ya kutangaza “kuhesabiwa haki” bali ni kazi ya Mungu mwenyewe….
ITAENDELEA
Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi piga sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios