top of page

HABARI YA APOLO,INATUFUNDISHA NINI?

Updated: Sep 30, 2022


Kila kilichoandikwa kwenye biblia kina maana na kusudi kwako. Hivyo,hakuna kisicho na maana ndani ya neno la Mungu. Leo,tujifunze kwa ufupi mambo manne katika habari ya Apolo kama ilivyoandikwa katika kitabu cha matendo ya mitume sura ya 18:25-26. Na andiko lilo ni hili;


Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.” Matendo 18:25-26


Hivyo,Apolo alikuwa ni mzaliwa wa Iskanderia nchini Misri,naye alikuwa ni mtu wa elimu (Matendo 18:24). Alikuwa ni mwinjilisti na muhudumu kama alivyo Paulo ( “ Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa.” 1 Wakorintho 3:5)


Pia biblia inamuelezea kuwa ni mtu aliyekuwa anajua hasa ubatizo wa Yohana,lakini hakujua ubatizo wa Yesu. Apolo alikuwa na shauku/roho yake ilimwaka hata akaanza kufundisha kwa usahihi habari za Yesu,ingawa alijua kwa sehemu tu. Apolo alifanikiwa katika mafundisho kwa sababu kwanza alifundishwa njia ya BWANA  pili alijitoa,akawa na kiu ya kufanya.  Hivyo tujifunze kidogo kwa Apolo mambo yafuatayo;


  1. Kufundishwa njia ya Bwana

  2. Kuwakwa na roho/roho ya shauku kwa ajili ya Bwana.

  3. Kunena kwa ujasiri.

  4. Kufundishika/kujishusha zaidi.


01.KUFUNDISHWA NJIA YA BWANA.


Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana;...” Matendo 18:25

Biblia haikumuelezea Apolo kwamba alikuwa akifundishwa na nani njia ya Bwana,lakini imeeleza kwamba alifundishwa njia ya Bwana,na ndilo tulijualo. Hii ni hatua ya kwanza na ni msingi wa utumishi mwema mahali ulipo wewe; kwa sababu huwezi ukafanya vyema kama hukufundishwa kufanya vyema. Tunapata picha katika habari ya Apolo kwamba alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi waliofundishwa njia ya Bwana.


Kuwa mwanafunzi wa njia ya Bwana” maana yake ni kukubali kuketi chini na ufundishwe ili uende nawe ukafanye kama ulivyofundishwa. Changamoto ilipo siku ya leo ni kwamba watu hawataki kuketi na kufanyika wanafunzi,bali wengi wanataka wafanye kwa sababu wamepewa neema ya kuokoka tu. Ikumbukwe kwamba;ukitaka kufanya vizuri kwa jombo lolote lile ukubali kujifunza kwanza. Yamkini Apolo asingeliweza kufundisha kama na yeye asingelifundishwa njia ya Bwana.


Kwako wewe,Je unajifunza kwa usahihi njia ya Bwana? Unajifunzaje? Je unafikiri neema uliyopewa ya kuitwa mkristo inatosha pasipo kujifunza njia ya Bwana? Je kanisa ulilopo sasa linakufunza vizuri njia ya Bwana? Je umechukua hatua gani uweze kukua kiroho? Hivi unajua kwamba tangu ulipookoka unapaswa uwe umekuwa zaidi ya hapo ulipo sasa? N.K


02.KUWAKWA NA ROHO ( SHAUKU)


“ …na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka,...” Matendo 18:25. Mojawapo ya siri kubwa ya kutumika na BWANA ni kuwa na roho hii ya kuwakwa ndani yako. Mfano mzuri wa roho ya namna hii ni pale unaposikia msukumo wa kujitoa kidhabihu kufundisha/kuhubiri/kusifu na kuabudu pasipo kulazimishwa wala kusukumwa na mwanadamu yeyote yule. Hakuna mafanikio ya kanisa lolote ulimwenguni ikiwa kama hakutakuwa na watu wenye roho ya namna hii.


Ukiwa na shauku hutaona haya kuhubiri popote pale,bali utahubiri tu. Roho yako ikikuwaka,utafanya mambo makubwa ya ajabu kwa sababu ya msukumo ulio ndani yako. Unajua biblia haisemi kwamba Apolo alilazimishwa kufundisha,bali alijikuta akisimama na kufundisha. roho ikikuwaka utajikuta unapokea neno saa ile ile la kusema( Marko 13:11).

Apolo alivyowakwa na roho,gafula alianza kufundisha kwa usahihi habari za Yesu ( naye alijua ubatizo wa Yohana tu).


Na ndivyo ilivyo hata sasa,ikiwa utawakwa na roho utafundisha hbari za Yesu kwa usahihi hata kama unayajua machache yanayomuhusu Yesu. Apolo alifanya hivyo,wewe je ? Ni eneo gani unaloweza katika Bwana kufanya kwa usahihi zaidi?. Suala sio kufanya tu bali suala ni kufanya kwa usahihi zaidi. Maana leo wengi wanatumika kwa Bwana,lakini si wengi wenye kutumika kwa usahihi zaidi.


03. KUNENA KWA UJASIRI

Mojawapo ya fundisho tunaloweza kujifunza katika habiri ya Apolo sawa sawa na andiko letu,ni ule ujasiri aliokuwa nao ingawa alikuwa anajua kwa sehemu tu.  Biblia inasema“… Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi;…” Matendo 18:26. Mungu hakutuumbia roho ya woga ( 2 Timotheo 1:6). Hivyo kila jambo la ufalme wa Mungu litende kwa ujasiri wote;usiogope ukiamini Bwana yupo nawe katika hayo yote. Ujasiri ni roho kamili ya Mungu,ambapo wewe nawe unapaswa uwe nayo.


Kila aliyefanikiwa katika kazi ya Mungu alikuwa ni jasiri/shupavu. Ukimuangalia Yoshua mtu aliyekuwa kiongozi kwa wanavwa Israeli,alikuwa jasiri na ndio maana Mungu alimwambia awe hodari na ushujaa mwingi (Yoshua 1:7). Apolo alifanikiwa kunena kwa ujasiri wote,na ndivyo nawe unatakiwa unene Neno katika ujasiri wote.


Ujasiri unaletwa na Roho mtakatifu,kukufanya uweze kunena kwa ujasiri katika hekima yote na nguvu zote. Hivyo hunabudi kuomba ujasiri kwa Roho mtakatifu. Unapowezeshwa na Roho,basi papo hapo fanyia kazi ukilinena neno la Bwana katika ujasiri kwa mtu yeyote,naye Bwana atakuongoza katika hilo hatimaye utaweza kumzalia Bwana matunda. Jifunze kwa Apolo mtu ambaye hukuyajua mengi kama unayoyajua wewe sasa,lakini Apolo alisimama kiujasiri na kukitamka anachokielewa yeye katika njia ya Bwana.


Jifunze pia kwa akina Yohana na Petro watu wasiokuwa na elimu na marifa ya kidunia. Lakini watu hawa walisimama kiujasiri kunena na kutenda kiasi kwamba watu wote walipoona ujasiri wao,wakatambua kwamba walikuwa na Yesu ( Matendo 4:13)


Jiulize;Unaogopa nini? Ni nani anayekutisha wakati wewe unaye Yesu? Je hofu yako yatoka wapi? Kwa nini unaogopa hata wakati pasipo-ogopesha? Je utafanikiwaje katika utumishi ukiwa bado una roho ya woga? N.k


Jifunze tena kwa akina Paulo na Sila jinsi walivyokuwa majasiri hata walithubutu kuimba na kuomba kwa sauti walipokuwa gerezani hatimaye milango ya gereza ikafunguka ( Matendo 16:25-26). Sasa jiulize;Wewe mbona unashindwa hata kujitambulisha kwamba ni mkristo na umeokoka? Kuna wakristo ambao hawawezi hata kubeba biblia katikati ya kusanyiko la watu,wengine hawawezi kusalimia “Bwana Yesu asifiwe..,” wakiwa katikati ya halaiki ya watu,wanaogopa kwamba wataonekanaje!!!


Sasa ikiwa ni hivyo tu,unafikiri watu hao watawezaje kuhubiri neno ? Maana kusalimia tu wameshindwa!!! Wewe Je unaweza kusalimia hivyo ukiwa katika halaiki ya watu mchanganyiko? Lakini leo ninakuambia jitie moyo,simama kijasiri maeneo yote hata katika maombi.


04.KUFUNDISHIKA/KUJISHUSHA NA KUKUBALI KUKOSOLEWA.


“…hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.” Matendo 18:26


Apolo alikubali kufundishwa na akina Prisila na Akila,ingawa alikuwa tayari anahudumu. Apolo angeliweza kukataa kuelezwa habari zaidi za Yesu,lakini biblia inatueleza alikubali kukaa chini ya Prisila na Akila afundishwe,akosolewe pia. Tazama roho aliyokuwa nayo Apolo ni roho ya namna yake tena ni roho ya kuigwa kwa kweli. Apolo alipochukuliwa na akina Prisila alijishusha na alikubali kutojua mambo mengine,akaruhusu aelekezwe kwa usahihi zaidi.


Lakini leo hali imebadilika kabisa! Watumishi wa Mungu wengi hawataki kufundishwa wala hawataki kukosolewa wakiamini sivyo ndivyo kwamba wanalijua neno zaidi ya watu wote. Ikumbukwe kwamba,sote bado tu wanafunzi wa Yesu na tutabaki wanafunzi maisha yetu yote;hivyo tu


Hata kwako wewe ndugu msomaji wangu,kubali kujishusha juu ya jambo/mambo usiyoyajua ili uketi chini ya anayejua kwa usahihi kisha akufundishe na kukuelekeza vizuri.kiwango chako unachoelewa jambo fulani katika ufalme wa Mungu kitaongezeka ikiwa utajishusha na kukubali kufundishika,kama ilivyokuwa kwa Apolo.


Tunayaona matokeo mazuri ya Apolo alipojishusha na kufundishika vizuri. Tokeo la kwanza aliwashinda Wayahudi kabisa kwa neno ls Mungu ( Matendo 18:28)

Emu jaribu leo kuomba kwa Roho mtakatifu akupe roho ya kujishusha hata mahali unapopajua,basi wewe kubali kushuka kwa lengo la kujifunza zaidi kisha utaona Mungu atakuinua wewe maana neno linasema ;


“ …kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” 1 Petro 5:5.


Hivyo ukijishusha ujue Mungu atakupandisha,na ukipandishwa na Mungu basi hakuna wakukushusha.

Yamkini mambo haya manne tunayojifunza kwa Apolo ni mambo magumu sana kuyaendea kwa sababu ya maisha fulani uliyonayo,basi naomba unipigie simu sasa kusudi tuombe pamoja na kwa kuwa Mungu ni mwema na mwaminifu,atakusaidia.


Nipigie kwa namba hizi sasa;

+255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446


Mch.Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page