top of page

GONGO LAKO NA FIMBO YAKO VYANIFARIJI.( Zab 23:4)

Mch.Madumla

Na Mch.Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

  1. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,Sitaogopa mabaya;Kwa maana Wewe upo pamoja nami,Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Zab.23:4

Najaribu kumuangalia mchungaji aongozapo kundi kwenye malisho au pale mchungaji anapolitoa kundi kutoka kwenye malisho,nikajifunza mambo kadha wa kadha. Na kwa sababu hiyo nikalikumbuka neno la Bwana katika zaburi ya 23 yenye kumzungumzia mchungaji mwema ambaye ndie Bwana Yesu. Kati ya mambo muhimu aliyokuwanayo mchungaji wa kundi lolote ni kuwa na “gongo” pamoja na“fimbo” kwa ajili ya kuliongoza kundi lake salama.

Gongo” ni aina ya fimbo pana yaani ni nene kwa muonekano. Mara nyingi gongo linakuwa halina shepu nzuri kwa sababu lenyewe ni kama limti fulani hivi. Wale wanaokaa na jamii ya wafugaji watakuwa wananielewa nisemapo “gongo“. Hivyo lifimbo hili ni lisilaha la mchungaji ambayo hutembea nayo pale anapokuwa akichunga. Kwa kuwa “gongo” ni silaha ya mchungaji basi ni dhahiri matumizi ya silaha hiyo si kwa kondoo wake bali ni kwa adui wa kondoo wake.

Kuna mambo mengi yatokeayo wakati wa kuchunga,mambo mengi huwa ni majanga ya kupambana na wanyama wakali wenye lengo la kula kondoo,au wenye lengo la kuwatawanya kondoo. Muangalie mchungaji hususani mchungaji wa kimasai jinsi anavyochunga kundi lake,katikati ya njia hukutana na wanyama wakali wenye uchu wa kula kondoo. Gongo kama silaha hutumika kushambulia adui ajaye kwa lengo la kuwadhuru kondoo wa mchungaji. 

Kupitia  ufahamu huo kuhusu “gongo” kama silaha ya mchungaji,tuangalie jambo hili katika imani yetu ndani ya  Kristo Yesu. Yesu Yeye ndie mchungaji mwema ( Yoh.10:11).  Mchungaji mwema anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Bwana Yesu alikubali kufa kwa ajili yetu,wala hakuna mwenye upendo mkuu kama huo wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake ( Yoh.15:13).  Kama jinsi ilivyo kwa mchungaji kuwa na gongo kama silaha kwa adui yeyote ajaye kwa kondoo zake,ndivyo ilivyo Yesu mchungaji mwema anavyotulinda usiku na mchana sisi ambaye ni kondoo wake. Jina lake na damu yake ni “gongo” dhidi ya adui ( Yoh.17:12,Ufunuo 12:11). 

Na ndio maana hata sasa tunayo amri ya kuwatandika mapepo kwa gongo la jina na damu ya Yesu na mapepo kutimka. Jina la Yesu ni dawa tosha kwa adui yoyote yule,litumie kufukuza adui ajae kwa lengo la kukuaribu wewe au ajaye kwa lengo la kuharibu kundi lako/kondoo zako. Lakini tujiulize; Fimbo Je,ni ya nini tena? Au kwa nini fimbo wakati gongo lipo?

Fimbo ni ya nini kwa mchungaji?

Kazi ya fimbo ni kuchapa kondoo anayechepuka. Kondoo wote wanatakiwa watembee in a one ship. Ni kwa ajili ya fimbo neno “fellowship” limezaliwa,ikiwa na maana tumfuate mchungaji mwema katika mwendo mmoja “follow him in a one ship“. Hivyo fimbo si kwa ajili ya adui bali kwa ajili ya kondoo.

Ukiwa ni mchungaji wa mifugo ya kawaida kabisa,utagundua kwamba mifugo yako mingine haiwezi kwenda mbele bila fimbo. Bila fimbo kondoo hawaendi kabisa,kwa sababu pale unapowataka wakufuate vizuri lakini unashangaa wemeiacha njia na kuchepukia kwengine. Kuna wakati kondoo hawamfuati mchungaji badala yake wanaenda katika njia zao wao wenyewe  na cha ajabu wanaendaga hadi kwenye mashamba ya watu na kuanza kupurura kuaribu mazao ya watu wengine. 

Sasa namna hii haiwezekani bila bakola! Na ndio maana hata sasa bakola zipo na zitaendelea kuwepo kwa kusudi la kutunyoosha ili tuweze kutembea pamoja katika imani ya kweli. Katika wokovu tukiwa kama kondoo wa Bwana,zipo bakola zile zile kama kondoo wa kawaida. Leo hii,wapo kondoo waliotandikwa bakola lakini ni bakola za upendo kusudi wanyooke katika njia ya kweli. 

Baba yoyote ampendae mwanaye na kumuongoza katika njia ya haki ni lazima amtandike bakola za kutosha mwanae ili aweze kunyooka katika kweli. Bakora za baba ni zile za upendo,haziui wala kuleta ulemavu bali ni kwa maumivu ya kitambo tu.

Hivi juzi juzi tu,nilikutana na mwalimu wangu aliyekuwa ananifundisha kusoma na kuandika pia alinifundisha Jiografia. Lakini mama huyu mwalimu alikuwa anachapaga jamani duh! Kwa kweli nilikuwa simpendi hata kidogo. Lakini leo kwa bakora zake zimenifanya niwe na juhudi,sasa ni mtu mzima  ninajua kusoma na kuandika,na ndio maana hata sasa nimekuandikia ujumbe huu. Nilikuwa najiuliza kama si kunyooshwa leo ingelikuwaje? Labda ningefeli vitu vingi sana. Biblia inasema;

Usimnyime mtoto wako mapigo;Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.” Mithali 23:13

Hivyo fimbo ni kwa ajili ya kutunyoosha tabia zetu sisi ambao ni kondoo. Fimbo haiui kwa maana fimbo ni tofauti na gongo. Sasa itakuwa ni ajabu kwamba baba yako akupige na gongo badala ya fimbo! Ukiona baba yako anakutandika na gongo ujue huyo hakupendi,ni adui yako na ana nia mbaya kwako nia yake ni kukuua kwa sababu gongo ni kwa ajili ya adui tu.Biblia inakumbusha kwamba ni lazima kuwepo na “marudia” ile hali ya kunyooshwa na Bwana ili tumpende Mungu kwa mioyo yetu yote,kwa akili zetu zote,kwa nguvu zetu zote na kwa roho zetu zote. Hivyo kwa kuwa Mungu anatupenda sana,na anataka sisi tusipotee basi inamlazimu aturudii,biblia inasema ;

Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi,Naye humpiga kila mwana amkubaliye.Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?” Waebrania 12:6-7

Ni ukweli kwamba si yote unayopitia yameletwa na shetani,mengine yameruhusiwa na Mungu mwenyewe kwa kusudi la kukuimarisha katika imani yako. Hayo yote yaliyoruhusiwa ni kama mitihani kwako,au ni kama marudia kwako,au kama fimbo kwako. Lakini ukumbeke ya kwamba kazi ya fimbo ni kumchapa aliyekosea. Kuna wakati tunakosea kwa kujijua kabisa na tunarudishwa kwa fimbo,pia kuna wakati tunakosea kutembea katika imani lakini pasipo kujijua pia tunarudishwa kwa fimbo.

Ndio maana mtunga Zaburi anazifurahia gongo na fimbo ya Bwana,anasema inamfariji. Kurudiwa na Bwana ni kuzuri. Angalia hapo,“tunarudiwa huku tukiwa katika ulinzi salama wa Bwana akiwafukuza adui kwa gongo lake” 

Kuna na mambo mengine hayatoki katika maombi isipokuwa Bwana ameyaruhusu. Yenyewe ni mfano wa mwiba usiotoka kwa maana Bwana mwenyewe ameruhusu ili tuzidi kushuka magotini mwake kila siku,tusimsahau Bwana. Mpendwa,gongo la Bwana na fimbo yake ni kwa ajili ya kuleta faraja kwako. 

Kwa msaada zaidi wa maombi, piga sasa +255 83 877 900

What’s app ni +255 746 446 446

Mch. Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comentários


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page