FILIMBI YA MPIRA.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 25, 2016
- 3 min read

Na mchungaji Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Filimbi ya mpira au kwa lugha nyingine “kipenga cha mpira” Katika mechi ya mpira wa miguu kuna timu mpili zinazoshindana. Kila timu inajitahidi imshinde mwenzake,lakini kuna mtu mmoja yeye sio mchezaji wa timu iwayo yote,mara nyingi huyu mtu husimama katikati hapo mwanzo,kisha akizunguka huku na huku akikimbia kimbia kana kwamba anacheza lakini hachezi bali huchezesha mpira tu.
Mkononi mwake ana kipenga/filimbi aliyoivaa katika shingo yake huku amebeba na kadi nyekundu au njano. Huyu ni mwamuzi wa mpira,tunamwita refalii. Kipenga cha mpira bhana,kinanifuraisha sana.!! Ukiona kinalizwa ujue kuna kosa limetokea,kama lah! wala hakilii.
Mpiga kipenga hufuatilia ni nani kakosea,na kakosea kosea vipi,akigundua tu,basiii pale pale hupuliza filimbi;akiwafahamisha watu wote uwanjani ( hata wale wasiokuwepo uwajani lakini wanatazama katika TV) kwamba mchezaji fulani kakosea. Na watu wote watajua makosa.
Yaani,sijawahi kumuona mpiga kipenga katulia mahali pamoja,bali anahaha kutafuta makosa ili akipige kipenga chake!!! Nikajiuliza siku moja,hivi laiti kama kusingelikuwa na makosa kipenga cha kazi gani? Kisha nikajua kwamba kipo kwa sababu ya makosa yanayotendeka.
Kazi moja wapo kubwa ya kipenga ni kupulizwa kwenye makosa,chenyewe hakina shida na haki,shida yake kubwa ni kuona makosa. Nikimtazama mpiga kipenga awapo uwanjani najifunza kazi ya kipenga jinsi kinavyoangaika kumtafuta mkosa,na kikimpata basi ujue watu wote watajua kwamba fulani kakosea,au fulani kadondoka.
Tazama,mahali pa usahihi hakioni usahihi,hata kama mchezaji alikuja uwanjani akapendeza sana kwa jezi nzuri,lakini chenyewe hakioni,au mchezaji kapiga chenga sana,hata hapo chenyewe hakioni hilo,Lakini akikosea tu lah! Utajuta,nakuambia watu wote watajua. Nikiiangalia kipenga kinanikumbusha mbali enzi za shule ya msingi kwa mwalimu wetu wa hisabati.
Kipindi ticha anafundisha ubaoni,akaandika orodha ndefu ya table ya hesabu (hesabu za kuzidisha) Alianzia 9×1 mpaka 9×9 lakini kumbe kulikuwa na makosa madogo aliyofanya wakati wa kuzidisha,Lakini wanafunzi hawakuona yote aliyopatia wao waliona misteki ( makosa) tu.
Hesabu ya mwalimu ilikuwa hivi; 9×1=17,9×2=18,9×3=27,9×4=36,9×5=45,9×6=54,9×7=63,9×8=72 na 9×9=81 alipomaliza akawageukia wanafunzi wake,gafla wote wakacheka,akawauliza mnacheka nini? Wanafunzi wakamwambia“ mwalimu bhana,umechemsha kweli yaani 9×1=17!!! hahahahaa” kumbe!!!
Wanafunzi hawakumpongeza mwalimu kwa kazi kubwa yote alivyopatia mengine,wala hawakuona ni njema,bali walipiga kipenga kwa kosa moja tu. Nikajifunza kitu hapo,
Nimejifunza hili kwenye maisha yetu ya wokovu,leo wapo watu wapiga vipenga wazuri. Wenyewe wanaangalia ni wapi umedondoka,wakijua tu,basi ujue papo hapo watakipuliza ili watu wate wajue,au kanisa zima lijue fulani kakosea wapi. Tuangalie kisa kimoja katika biblia kinachofanana na haya nikuelezayo;
“ Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.” Yoh.9:1-3
Wanafunzi wa Yesu,wao walipomuona kipofu,moja kwa moja wakaanza kufikilia makosa, wao waliona dhambi ndio sababu kuu ya kipofu kuwa kipofu. Wakamuuliza mtu huyu ndio katenda dhambi? Au wazazi wake? Kwa lugha nyepesi ni kwamba walitaka kujua ni nani kakosea hata huyu awe kipofu? Ndivyo hali ilivyo leo makanisani kwa wapendwa; utakuta mtu anapitishwa eneo fulani,labda uogonjwa fulani hivi.
Gafla watasema kwambi ni dhambi katenda huyu ndio maana anaumwa,kwa hiyo filimbi itapigwa kiasi kwamba kanisa zima litajua fulani kadondoka dhambini hata akawa hivyo. Mfano mzuri; mchungaji anaweza naye akapita katika eneo gumu,lakini wapiga vipenga watapiga kusema mchungaji kaanguka. Lakini hata kama kweli kaanguka dhambini,je ni halali kupinga kipenga watu wajue kwamba mchjngaji wako kaanguka? Je si vibaya hivyo?
Kuna watu jamani wamebobea kupuliza kipenga cha habari mbaya pale tu wamuonapo mwenzao kadondoka. Hii ni mbaya,haipaswi kuwa wapiga vipenga kwa makosa ya wenzetu. Kabla hujapuliza kipenge chako,jiulize hivi; Je wewe huna makosa? Jifunze kwa habari ya yule mwanamke aliyefumaniwa. (Yoh.8:1-8) Waliibuka washtaki wake ambapo walitaka kumuhukumu lakini wao wenyewe ni wakosaji wakubwa!
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,na unahitaji maombi kwa eneo lolote unalopitia sasa,tafadhali nipigie sasa; ; +255 683 877 900
Mchungaji G.Madumla.
What’s app +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments