top of page

DHAMBI ITUZINGAYO KWA UPESI.


sin

Na mchungaji G.Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Je dhambi ituzingayo kwa upesi ni uzinzi? Je ni ulevi?,Je ni utukanaji/usengenyaji?

Inawezekana ikawa ni moja kati ya hayo,unajua kila mmoja ana udhaifu wake. Wengine uzinzi ndio udhaifu wao,wengine ulevi. Udhaifu wote wa namna hiyo ni kazi ya ibilisi tu.

Lakini nilipoanza kumwangalia mzinzi niligundua kwamba kabla ya kuzini kuna dhambi aliifanya kwanza ndipo akazini baadae. Nilirudi kumwangalia mwivi au tapeli niligundua kabla ya kuiba au kutapeli kuna dhambi fulani iliyotangulia.

Lakini nikaenda kumchunguza mlevi,naye pia nikagundua kwamba kuna dhambi iliyotangulia kufanyika kabla ya ulevi,nikaona aitoshi nikamuangalia muuaji kuanzia yule aneyetoa mimba iwe ni mwanaume au mwanamke hadi yule mwenye kuua kama kuua nikagundua kitu kile kile kwamba kuna dhambi ilitangulia kufanywa

Bila shaka “nia mbaya ” ndio chanzo cha dhambi zote kwa maana huwezi kutenda dhambi ikiwa huna nia mbaya. Then baada ya kupelekeshwa na ile nia mbaya ndani yako,ndipo kitu cha pili kinafuata nacho ni kuwa na mawazo mabaya na hatimaye hatua ya kutenda inafuata. Sasa moja ya dhambi inayotumaliza watu wengi tena hata watumishi wa Mungu baadhi yake wamekamatwa katika dhambi hii ni dhambi ya “udanganyifu au uongo”

Kila mtenda dhambi hakosi kudanganya kwanza ndipo akamilishe dhambi yake. Mfano mzinzi ni lazima adanganye kwa wingi ndipo afanikishe kutenda uzinifu. Hali ipo hivyo hivyo kwa kila mtenda dhambi. Hivyo kama tungelisema dhambi inayotusonga kwa wepesi basi ingelikuwa ni ile nia ya ndani ipelekeayo kusema uongo au kupanga njama za udanganyifu!

Ebu angalia hata namna ile dhambi ilipoingia ulimwenguni kupitia mtu mmoja  (Adam). Maandiko yanasema shetani (baba wa uongo) alikwenda kumlaghai mwanamke  kwa lengo moja tu,kwamba mwanamke asimwamini tena Mungu. Alipofanikiwa kujaza uongo,uongo huo huo ulienda kwa mwanaume wake Adam,naye akamsikiliza mke wake kuliko Mungu,na mara wakaanguka dhambini kwa kutokutii sauti ya Mungu. Lakini dhambi ya kuasi au kutokutii ilitokana na nini? kama si udanganyifu kutoka kwa ibilisi! Biblia inasema ; “ Hawa alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa ”. (1 Timotheo 2:14).

Kuna siku moja nilisikia tangazo la mkutano wa injili hapa Dar es salaam kwetu pazuri,radio moja ya Kikristo iliyokuwa ikitangaza mkutano huo. Sasa, kilichonishangaza mimi ni tangazo hilo jinsi lilivyo,kwa maana walitangaza kwamba kutakuwepo na watumishi zaidi ya 100 mitume na manabii watakaosimama wote na kunena kwa siku moja,tena sio siku moja ni masaa machache mno katika siku moja.

Kitu ambacho hakiwezekani kwa idadi kubwa ya hao mitume na manabii kusimama mmoja mmoja kisha wakanena wote hata kama ingelikuwa ni kwa siku tatu! Niliposikia nikagundua kwamba walitangaza vile ili kuwashawishi tu watu waje kwa wingi ili watabiliwe mambo yao,lakini huu ni uongo wa wazi kwa maana

haiwezekani watumishi zaidi ya 100 kusimama kila mmoja na kutabiri kwa kipindi cha muda mfupi wa semina. Sasa umeona hapo!!! Hilo ni tangazo la watu wanaojitambulisha wameokoka! lakini bado uongo umewaganda! Hii ni mbaya, Kwani ukitangaza katika uhalisia wake kuna shida gani mpaka uingie katika uongo? Maana ni afadhali sana utangaze katika ukweli wake hata kama atakuja mtu mmoja tu basi huyo huyo ndiye atakuwa amekusudiwa na Bwana,na inatosha kabisa!

Angalia mfano mwingine ambao watumishi wa Mungu wanavyoangukia katika dhambi hii,Utakuta mchungaji ameandaa semina au ibada maalumu kisha anafikiria namna ya kuwatangazia waumini wake.Na baadae anagundua kwamba anataka semina yake ianze  saa tatu asubuhi,lakini anawajua waumini wake wakitangaziwa saa tatu kamili asubuhi watakuja saa nne asubuhi.

Kwa hiyo Mchungaji analazimika kudanganya kwa kuwatangazia waumini kwamba semina itaanza saa 2 asubuhi wakati hakijua kabisa muda huo wa saa 2 asubuhi yeye mwenyewe hawezi kuanza kwa muda huo. Huu ni udanganyifu unaofanyika madhabahuni,kwa nini usitangaze kwa muda ule ambao hakika utaanza muda huo huo ili kusudi uwazoeshe waumini wako kwamba wewe ni mtu ambaye ukitangaza jambo lazima ulifanye katika muda ule ulke uliotangaza?

Sasa kwa kuwadanganya waumini juu ya muda basi kunawafanya waumini nao kukusoma na kukuelewa kwamba wewe ni mdanganyifu katika muda wa Mungu nao wataendelea kuwa wadanganyifu. Soma Kutoka 23:1

Siku moja mchungaji aliwauliza waamini kwamba “ ikiwa mtu yeyote asiyesema uongo baada ya kuokoka na asimame juu” kanisa zima ziiiii! Hakuna hata mmoja aliyesalimika hali wameokoka. Kumbe kila mmoja ana sehemu yake alidanganya,lakini kikubwa ni je watu hawa walifanya toba baada ya dhambi ya uongo? Ikiwa hakukufanya toba hawatasamehewa. 

Ikumbukwe kwamba,hakuna dhambi kubwa wala dhambi ndogo, kwa maana dhambi ni dhambi tu. Lakini dhambi ya uongo inazinga kwa upesi sana kuliko dhambi nyingine ziwazo zote. Leo watu wengi wamekwama kuona udhihilisho wa Mungu kwa sababu ya dhambi ya uongo,wengine imefika wakati udanganya madhabahuni kwa BWANA hali wakijiua kabisa kwamba kile wakisemacho ni uongo lakini husema tu. Jamani tumuogope MUNGU sasa,Mungu hadhiakiwi!

Siku nyingine tena mnenaji wa semina alifanya changizo,akawaita watu watakao changa million mbili mbili. Watu baadhi wakaenda madhabahuni,katikati yao kulikuwepo na kijana mmoja naye akasimama akaenda. Nikawa nashaka kidogo kumuona yule kijana,lakini nikasema “ anyway you never now,inawezekana anazo bhana” kumbe bhana yeye alijiendea tu,sasa sikujua kwamba alikuwa hajaelewa au vipi? Ni vyema madhabahu ikaheshimiwa tukaelewa na kile kitamkwacho.

Biblia imeweka wazi kwamba waongo wote sehemu yao ni kwenye ziwa la moto (Ufunuo 21:8). Fikiria,kwa uongo tu,unakwenda motoni. Kwa takwimu zisizo hakikiwa ni kwamba;wengi hutupwa motoni kwa sababu walianguka katika uongo,inwezekana kweli wakawa waliokoka lakini uongo tu ukawaangusha.

Kumbuka hili;uongo ni roho kamili itendayo kazi kwa watu wengi. Mtu yeyote aliyevamiwa na roho hii,kumpenda Baba ni kwa kuigiza igiza. Kwa maana kwa sehemu huabudu kweli,na kwa sehemu bado ni mtoto wa ibilisi kwa kuwa ibilisi ndio baba wa huo uongo. Mungu atusaidie.

Jikague nafsi yako je uongo si sehemu inayokukwamisha maisha yako ya kiroho hata kushindwa kumuona BWANA. Ikiwa ni kweli,sasa chukua hatua kwa kutubu na kukataa hiyo roho. 

Waweza nipigia simu sasa tuombe pamoja; Kwa huduma ya maombezi piga sasa; +255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446

MchungajiG.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page