DAUDI,KIPENZI CHA MUNGU.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 8, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Daudi mtu aupendezaye moyo wa Mungu / A man after my own heart
Maneno aliyoyasema Bwana Mungu kwa Daudi yanafanana na maneno yale aliyoyasema kwa Yesu ( Mathayo 3:17 linganisha na Matendo 13:22) Kipindi Yesu cha ubatizo wa Yesu,Mungu alimwambia Yesu “ huyu ni mwanangu ninayempenda” kisha akamwambia pia Daudi “Daudi,mtu anaupendeza moyo wangu” maneno haya yanafanana katika neno moja “ pendo la Mungu ” alilolifunua kwa Daudi mtumishi wake pamoja na Yesu mkombozi.
Lakini hii yote ni kudhihilisha kuwa Daudi, alikuwa ni kipenzi cha Mungu. Tambua neno hili kwamba, kama mtu amekuwa ni kipenzi cha Mungu, basi ni dhahili kwamba, moyo wa mtu huyo ni wa ajabu,ni moyo wenye roho ya kicho. Daudi alikuwa na roho ya kicho,kwa maana hata alipotendewa mabaya na mtangulizi wake Sauli,yeye hakulipa baya kwa baya,bali alilipa baya kwa wema.
Leo,najaribu kuangazia maisha ya Daudi tangu alipozaliwa hata mambo kadha wa kadha yaliyotendeka kwenye maisha yake sawa sawa na yasemavyo maandiko. Mtu huyu ameacha alama kubwa ya kujifunza. Jambo moja la msingi la kukumbuka ni kwamba, katika uzao wake Daudi,Mungu alituletea Mwokozi yaani Yesu kama alivyoahidi ( Matendo 13:23). Hivyo unavyomtazama Daudi, yafaa kumwona Mwokozi Yesu Kristo. Ikiwa Kristo alipitia kwenye uzao wa Daudi basi si jambo dogo hili!!! Kristo kupitia kwenye uzao wa Daudi ni kutimilika kwa nabii zilizotangulia,nabii kama ya Isaya,(Isaya 11:1).
Daudi ni nani hasa?
Daudi ni mtoto wa nane wa Yese ( 1 Samweli 16:10-11). Hata hivyo inaonekana ni mtoto wa nje ya ndoa ( Zab.51:5). Ni mjukuu wa Obedi,aliyemzee Yese ( Ruthu 4:22), Ni baba mwenye familia kubwa – wake na watoto ( 1 Samweli 18,25:39-44,2 Samweli 3:2-5,5:13-16). Daudi alipakwa mafuta na Samweli ( 1 Samweli 16:1-13). Alikuwa ni mwana Zaburi / mwimbaji ( Mathayo 22:43-45),lakini pia alikuwa ni nabii (2 Samweli 23:2-7,Matendo 1:16). Kama mtunga Zaburi,aliandika Zaburi kama zifuatavyo,( Zab ya 2,3-32,34-41,51-65,68-70,86,95,101,103,108-110,122,124,131,133,138-145 ).
Matukio ya awali.
Kwanza kabisa, alikuwa mchungaji wa kundi la Yese,pia alikuwa mwana mziki mzuri kwa Mungu, na kwa Sauli mfalme ( 1 Samweli 16:14-23). Akiwa kijana mdogo mwenye Roho wa Mungu ndani yake,aliweza kupiga kinubi hata pepo likatoka. Hii ni nguvu ya ajabu tunayohitaji ziku za leo,kwamba kwa upigaji tu wa chombo cha mziki,husababishe mapepo kukimbia na kutoka ndani ya watu. Lakini alikuwa ni mtu mwenye kujua vyema suala zima la uhusiano,alifanya patano na Yonathani mwana wa Sauli ( 1 Samweli 18:1-4 n.k)
Mwenye moyo wa kuachilia
Chanzo kikuu na cha kwanza cha uhasama alioupata kutoka kwa Sauli,kilikuwa ni “wivu” Sauli alimwonea wivu Daudi hata kumtafuta amwue akidhani ya kuwa atanyanganywa ufalme wake ( 1 Samweli 18:6-9). Kwa jitihada zote za Sauli kutaka kumwangamiza Daudi, lakini hakufanikiwa kwa maana Bwana alikuwa pamoja naye ( Daudi). Lakini mara chache,Sauli alijisahau,naye Daudi hakutaka kabisa kulipiza kisasi,( 1 Samweli 24: 6). Daudi angeliweza kumwangamiza Sauli, lakini hakuona ni kitu cha kuchukuliana nacho,kwa maana alimwona Sauli kama mpakwa mafuta wa Bwana. Huu ni moyo wa kuachilia,si rahisi kumwachilia mtu anayekutafuta kukuua halafu mtu huyo yeye mwenyewe ajisahu / aingie kwenye 18 zako,halafu ukamwacha tu,si rahisi jambo hilo,lakini kupitia Daudi tunaona namna ambavyo moyo wake ulivyo.
Bwana akimtumia
Alimwua Goliathi / anayepaswa kutazamwa ni Mungu aliyempa kushinda ( 1 Samweli 17)
Alipakwa mafuta tena awe mfalme wa Yuda ( 2 Samweli 2:1-4) Ingawa kulikuwa na kutoelewana na nyumba ya Sauli ( 2 Samweli 2-4)
Alitiwa mafuta tena awe mfalme juu ya Israeli yote ( 2 Samweli 5:1-4)
Aliishindia Yerusalemu ( 2 Samweli 6)
Alikuwa mwenye kuutafuta uso wa Bwana kabla ya kupanda vitani,Bwana akampa kushinda kwa sababu hiyo.
N.K
Changamoto katika huduma yake.
Kama mwanadamu,naye alikutana na changamoto nyingi tu. Hii yote ni kujaribu kueleza kwamba na yeye ingawa alikuwa ni mpakwa mafuta lakini alikuwa ni mwanadamu. Changamoto chache ndizo ninazokuandikia;
Uzinzi na mke wa mtu pamoja na uuaji ( 2 Samweli 11-12)
Mtoto wake kumbaka dada yake ( Amnoni kumbaka Tamari,kisha Absolumu akamwua Amnoni 2 Samweli 13)
Kuishi kwenye maisha ya mazomeo baada ya dhambi,ingawa Bwana alimsamehe.
Aliadhibiwa na Bwana kwa makosa ya kuwahesabu watu. Naye akaangukia kwenye mkono wa Bwana kwa kupigwa na tauni ( 2 Samweli 24:1-25)
N.K
Ingawa Daudi alikuwa na changamoto nyingi, nyingine ni za kufanya uovu,lakini bado Daudi alikuwa ni kipenzi cha Mungu. Tena pamoja na hayo yote,wakati wake wa kufa ulipokaribia,Daudi alikuwa na neema ya kujua. Na alihakikisha anamwusia Sulemani mwanawe,kwamba sulemani “ajionyeshe mwanamume” yaani afanye kiume. ( 1 Wafalme 2:1-2). Huyu hakika alikuwa ni shujaa,kwa maana shujaa yeyote huacha wosia mzuri kwa mwanawe.
Neema ilimwinua Daudi.
Ukitafakari kwa nini Mungu alipendezwa na Daudi, utagundua ilikuwa ni neema tu,wala haikuwa kwa akili zake Daudi, ingawa moyo wa Daudi ulikuwa tofauti sana na mioyo ya kaka zake. Lakini ni nani aufanyaye moyo wa mtu kumwelekea Bwana kama si Bwana mwenyewe? Neema ilimwinua sana Daudi. Lakini ni vyema ukafahamu kwamba ingawa kulikuwa na neema lakini pia Daudi alikuwa mnyenyekevu.
Hii inatufundisha kwamba Mungu ana sehemu yake,lakini pia wewe una sehemu yako. Ikiwa Daudi alikuwa mwanadamu kama wewe,naye akafaulu kuupendeza moyo wa Mungu, wewe pia unaweza ukaupendeza moyo wa Mungu, nawe ukafanyika kipenzi cha Mungu. Lakini ukweli utabaki pale pale kwamba, wokovu / kuokoka / kuzaliwa mara ya pili ndio kigezo muhimu na cha kwanza hata kuwa kipenzi cha Mungu. Daudi amekuwa na historia ndefu,laiti ningeliandika yote basi somo lingekuwa lefu sana,lakini katika kidogo nilichokiandika ujifunze kitu,kwamba wewe nawe unayo historia yako,ni vyema ukawa mmoja wa watu ambao Mungu apendezwe nawe.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900
Na.Mch. G.Madumla
Whatsapp namba +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comentarios