top of page

BIBLIA KITABU PEKEE KINACHOELEZA KWELI YOTE.

Na mch. Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Duniani kuna vitabu vingi vinavyoeleza mambo kadhaa wa kadhaa. Lakini cha ajabu vitabu vyote hivyo haviwezi kueleza kweli. Pale ambapo kiongozi kakosea vitabu haviwezi kuandika makosa yake,tena pale ambapo kiongozi anapotakiwa arekebishwe vitabu vya duniani hii hunyamaza kana kwamba hakuna kosa wala hakuna kujirekebisha. Lakini sivyo ilivyo biblia,yenyewe inafichua maovu ya kiongozi hata kuyaweka wazi ili kila mtu asomaye aone makosa yaliyopo ili kusudi yeye asomaye asije akaanguka!

Ni nani angelijua kwamba biblia ingeeleza makosa ya Nuhu baada ya kutoka kwenye safina? Ni kweli usiopingika Nuhu alikuwa mtu wa haki,mkamilifu( yaani zaidi ya mlokole wa leo,ingawa tupo watu wenye sifa kama hizo alizokuwa nazo Nuhu)-Mwanzo 6:9. Nuhu alikuwa mwenye haki na mkamilifu tena aliyekwenda pamoja na Mungu. Huyu ni mfano wa mtu wa kuigwa tena kiongozi. Lakini ebu angalia baada ya gharika alipoonza kuwa mkulima kile alichokifanya;

“Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu;akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.” Mwanzo 9:20-21

Biblia haikusita kuyaandika na mabaya aliyofanya Nuhu ingawa alikuwa mtu wa haki,mkamilifu. Laiti kingelikuwa kitabu kingine yasingeliandikwa na mabaya,wangeliandika mazuri tu kama lengo la kupotosha kwa maana yakiwepo mazuri basi yafaa yaandikwe na yakiwepo mabaya yaandikwe vivyo hivyo kwa lengo la kutufundisha. 

Ni mfalme gani aliyekuwa mkuu kama mfalme Daudi? ( ingawa Yesu ndie mfalme wa wafalme,lakini ufalme wake si wa dunia hii). Daudi alikuwa mtu mkubwa zaidi ya vile ujuavyo. Yeye Daudi ndie aliyeonekana kuyafanya mapenzi ya Mungu yote tena anayeupendeza moyo wa Mungu ( Matendo 13:22). Je kulikuwako mtu kama huyo? Je hata sasa ni wakristo wangapi watakaoweza kufanana na Daudi? Je unajua Yesu naye ni uzao wa Daudi? ( Isaya 11:1-4,Marko 10:48 n.k)

Lakini Daudi naye alifanya makosa kama mfalme,na habari zake je hatuzisomi kwenye kitabu cha 2 Samweli 11:1-27.? Ijapokuwa alikuwa ni mfalme lakini alipokesea kwa kuanguka dhambini kwa kulala na Bath-sheba mke wa jemedari wake Uria,tena akamua na huyo Uria jemedari wake kwa kumtanguliza mbele za vita. Ebu fikiria ukuu alionao Daudi lakini aliandikwa bado! Hiyo ndio biblia isiyoficha kitu bali yenye kueleza kweli yote bila wasi wasi. Niseme nini zaidi kuhusu kweli tunayoipata kwenye biblia,ebu fikiria tungeyajuaje haya yote bila biblia? 

Lakini tunajifunza nini katika hili?

01. Ni lazima tuseme kweli siku zote bila woga wala wasi wasi.

Tunasemaga ,hivi“msema kweli ni mpenzi wa Mungu” na hii ndio kweli yenyewe. Ifike wakati sasa tuseme kweli kwa watu wote,mahali penye makosa basi tuseme kuna makosa,na mahali penye uzuri basi tuseme uzuri. Wewe usomaye hapa hivi sasa,ni lazima ujifunze kusema kweli hata kama itakugharimu lakini usiogope kusema kweli,wewe sema tu Mungu atakupigania,kwa maana Mungu hajawaacha upweke wasema kweli. Siku zote wasema kweli wanachukiwa na jamii,lakini hao ndio kipenzi cha Mungu.

Mfano,ukiwa mtumishi wa Mungu umepewa ujumbe juu ya watu fulani. Na ukiwaangalia watu hao unagundua kwamba kama utawahubiria kweli hawataipenda maana wanataka ya kuwapendeza pendeza,alafu cha ajabu na wewe kama mtumishi wa Mungu unabadili kweli kwa uongo kwa kuficha ficha neno la Mungu kwa lengo la kutaka kuwapendezesha wanadamu hao!!! Hapana,hapana,hapana!!!usifanye hivyo

Inakubidi useme kweli kama isemavyo biblia,mahali pa makosa sema hayo makosa uwarekebishe wanaosikia,mahali penye uzuri sema tu. Hakuna kitu kibaya kama kuijua kweli kisha usiiseme na kuficha ficha au ukasema uongo!. Jiulize je wewe ni msema kweli siku zote?Je kwenye ndoa yako wewe ni msema kweli?kazini kwako je wewe ni msema kweli?

Ukiwa mkristo huna budi kusema kweli siku zote kama biblia isemavyo kweli. Jambo hili ni muhimu sana,maana kwa kuogopa kusema kweli unajitenga na Mungu sababu Mungu ni kweli yote.  Usiposema kweli utasema uongo na ijapokuwa wewe ni mkristo lakini kule kuogopa kusema kweli hatimaye ukawa unasema uongo basi utambue shetani atakuwa ndio baba yako maana yeye shetani ndio baba wa huo uongo (Yohana 8:44)

Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900

Namba ya what’s app ni +255 746 446 446

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page