AJIKWEZAYE ATADHILIWA NAYE AJIDHILIYE ATAKWEZWA (Luka 18:14)
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 20, 2017
- 4 min read

Na Mch.Gasper Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
Siku moja nalimuona mtumishi aliyekuwa madhabahuni akijisifia na kusema kwamba “ upako umejaa kwangu,mimi ndio nabii bhana! Mimi ni balaaa! Usicheze na mimi,hakuna nabii kama mimi…” hayo ni baadhi tu ya maneno ya kujigamba aliyokuwa akisema mtumishi. Nikajiuliza swali moja kwamba “kuna haja gani ya kujisifia namna ile?,hata kama ni kweli kwamba ana upako mkubwa,Lakini ndio ujitambe namna hiyo? ” ndipo nikamuomba Mungu amuhurumuie huyo ndugu,kwa kuwa inaonekana hajui alitendalo awapo madhabahuni. Kwa kuwa madhabahu ya Bwana sio ya kueleza mambo ya kipuuzi.
Tabia hii ni mbaya sana ya kujisifia uwapo madhabahuni,kwa nini usipeleke neno la Mungu kama ilivyokusudiwa na Bwana? Tabia hii ndio mfano wa kwanza wa kujikweza. Lakini labda tujue ya kwamba kila mwanadamu ana tabia ya kupenda kuonekana bora zaidi ya mwingine. Tabia hii ni tabia ya kiburi cha uzima. Hii ni sawa na kusema kila mtu ana kiburi fulani ndani yake, Ikiwa kama hujaokoka,au umeokoka nusi nusu basi ujue tabia ya kiburi itakutesa sana kwa maana itajitokeza nje. Na ikiwa umeokoka kwa kumaanisha,basi tabia hii ya kiburi inashughulikiwa na Roho mtakatifu na kuanzia hapo haina nafasi tena.
Roho mtakatifu anaigandamiza tabia ya namna hii kiasi kwamba kiburi hakitaweza kukutawala kabisa,Lakini ukirudi nyuma au ukiiacha njia ya kweli katika Kristo Yesu,basi kiburi nacho kinapanda juu hatimaye kinajitokeza nje,ni kama vile unavyozamisha mpira wa miguu katika maji gafla utazama wote kwa sababu umeushikilia na umeuzidi nguvu, lakini ukiuachilia nao unapanda juu ya maji tena na ndivyo kilivyo kiburi.
Roho mtakatifu ukishusha na kukigandamiza kiburi mpaka chini kabisa,lakini ukimuacha Bwana Roho uondoka na gafla utashangaa kiburi kimepanda juu. Na ndio maana waweza ukamuona mtu ameokoka vizuri kiasi kwamba hana kiburi bali yeye siku zote ni mtu wa kushuka mbele za Bwana,lakini mtu huyo huyo akimuacha Bwana kiburi nacho chaja.
Mojawapo ya tabia mbaya ya shetani ni kiburi. Kiburi ni kinyume cha unyenyekevu,hivyo kiburi ni ile hali ya kujiona wewe ni bora kuliko wengine. Au ni ile hali ya kujihesabia haki kuliko wengine,tena ni ile hali ya kujifikilia wewe tu.
“Kujikweza” ni hali ya kujiinua au kujipandisha,au ni ile hali ya kujikinai na kujiona mwenye haki kuliko wengine na kuwadharau wengine pia. Mfano mtu aweza kusema “fulani anajikweza sana..” ni sawa na kusema “fulani anajiinua sana,au fulani anajiona bora sana kuliko wenzake…” Mara nyingi mtu anayejikweza hujitamkia maneno ya kujisifia,kujipamba pamba kwa uongo na kushindwa kumpa Mungu utukufu.
Jiulize Je wewe ni mmoja wao? neno hili “kujikweza” linapotumika linaeleza ile tabia ya kale iliyokuwa haijafa bado ndani ya mtu,tabia ya mtu kupenda sifa ambazo yamkini wala si kweli katika hayo ayasemayo. Leo hii kuna watu wanaojiinua kupita kiasi tena bahati mbaya wengine ni watumishi wa madhabahuni,kujiinua huku ndio kujikweza,yaani kutaka kusifiwa kilazima lazima.
“Kudhiliwa” ni hali ya kushushwa. Kumbuka jambo moja ya kwamba ukijiinua basi utashushwa. Labda sasa tuangalia biblia inasema nini kuhusu tabia hii ya kujikweza,Tujifunze katika mfano huu;
“ Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang?anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Luka 18:9-14
Maandiko hayo yanatueleza habari za watu wawili waliokwenda hekaluni kusali ambao ni Farisayo na wa pili ni mtoza ushuru. Farisayo alikuwa ni mtu wa kujihesabia haki,mtu wa kujiinua na inawezekana yale ayasemayo hayana ukweli ndani yake. Tunaona tabia ya kujiinua jinsi inavyofanya kazi kwa mtu. Tabia hii ni roho ya shetani,kwa maana mtu ujisifia kuliko kumsifia Mungu.
Leo wapo sampuli nyingi za akina Farisayo katika jamii yetu hususani kwenye nyumba za ibada. Watu wanajipenda wenyewe na mara nyingi wanajipamba kwa maneno mazuri mazuri kuonesha wao ndio babkuwa! Mfano wa akina Farisayo wa leo katika nyumba za ibada,; utakuta mtumishi akihubiri huku mikono yake imo mifukoni mwa suruali yake,au akisema kejeli kwamba;
“ yeye ni noma” mara wengine hujipachika majina yasiyo nautukufu wengine hujiita “maburudoza,mzee wa upako,transforma ya Yesu,mzee wa miujiza,..n.k” Sasa ujiulize kwamba ile nia ya ndani ya wote wenye kujipachika majina ya ajabu ajabu ni ipi? Je si wao kutaka kuonekana ni bora zaidi ya wengine? Tena wengine hujiona bora kuliko Yesu!!! Kwa sababu mtu akiwa anajielezea sifa zake kuliko kulitaja jina la Bwana,Je mtu huyo kweli hafikirii ubara wake kuliko Mungu?
Farisayo alijikweza kwa maneno mengi ya kujipamba kwamba yeye ni bora sana wala sio kama huyo mtosha ushuru. Angalia Bwana Yesu asemavyo “ Kila ajikwezaye atadhihiliwa naye ajidhiliye atakwezwa ” Luka18:14
Kumbuka yafuatayo;
Mtu yoyote akijikweza katika maneno au matendo anakuwa ni adui wa Mungu tena adui wa watu. Angalia, Mungu hawezi kuendelea kupitisha utukufu wake kwa mtu mwenye kujikweza. Matendo ya Mungu ufika wakati yanakomea hapo,lakini pia watu nao wanakwazika sana kiasi kwamba hata wengine wanaamua kuama kanisa au huduma. Mfano mdogo ni huu;
Ikiwa kama kuna mtumishi wa Mungu ana tabia hii ya kujiinua,akiwa anafundisha iwe ni kwenye radio,basi kule kujikweza kwake kunasababisha wengine wachukizwe naye na kufanya maamuzi ya kubadilisha chaneli ya radio au TV.
Ukijiinua katika eneo lolote katika maisha yako,ujue Bwana atakushusha tu hata kama itachukua muda lakini ipo siku utashushwa. Bwana Mungu hupendezwa na yule mwenye kujishusha mbele yake ili yeye Mungu apande.Paulo anasema kwamba kwa kusudi asipate kujivuna kupita kiasi,alipewa mwiba katika mwili wake,huo mwiba ni mjumbe wa shetani ili ampige asijisifu ( 2 Wakorintho 12:7). Wewe ambaye wajisifu kupita kiasi,Je unasubiri upate mwiba?
Ukipewa neno hubiri neno yatosha,ukiwa mwalimu basi fundisha sifa na utukufu uwe ni kwa Mungu katika Kristo Yesu. Hauna haja kujinadi kwa maneno mengi ya kwako,maana injili sio siasa. Eleza ujumbe wa Mungu kisha songa mbele,Bwana ainuliwe pekee. Ifike wakati uichukie tabia hii mbaya,tabia ya rusifa/shetani.
Kwa huduma ya maombezi nipigie sasa + 255 683 877 900
what’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.G.madumla.
UBARIKIWE.
Comments