AGANO LA KALE NI LIPI?
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 8, 2018
- 3 min read
Updated: Sep 30, 2022

Akitokea mtu mmoja na kukuuliza sasa,kwamba hivi agano la kale ni lipi katika biblia? Au agano la kale lipo wapi hasa katika biblia? Swali hilo ni zuri sana maana wengi tunajua agano la kale lipo kwenye biblia,lakini hatufahamu hilo agano la kale likoje?au ni lipi hasa? Maana kwenye biblia kuna maagano mengi.
Neno “ agano” lina maana ya makubaliano au mapatano ya kudumu kwa muda usioweza kuhesabika,kati ya pande mbili Mungu akiwa ni shaidi au mungu akiwa ni shaiodi. Sifa kubwa ya agano ni kuhusishwa kwa damu,na kutovunjika lakini pili linamuhisisha Mungu au mungu kutegemea ni mtu / watu wa namna gani wenye kuingia agano.
Awali ya yote ni lazima ufahamu kwamba kuna vipi vinne muhimu vilivyokuwa kwenye biblia. Hata leo tupo kwenye kipindi kimojawapo kati ya vipindi hivyo. Navyo ni;
01.Kipindi cha mababa (wa kale)
Kipindi hiki ni kile cha akina Ibrahimu,Isaka na Yakobo. Abramu kabla ya kuitwa Ibrahimu aliambiwa atakuwa taifa kubwa na kubarikiwa ( Mwanzo 12:2). Bwana Mungu alichagua watu maalumu waliokwenda naye asema nao. Ibrahimu mtu aliyechaguliwa na Mungu,na mwenye maagano na Mungu,alikwenda na Mungu. Ibrahimu alimuamini Mungu sana,kiasi kwamba alifanya yote aliyoamriwa na Mungu.Katika kipindi hiki,malaika wa Bwana walikuwa wakishuka kwa mfano wa wanadamu wa kawaida ( Mwanzo 18:2-3,19:1-3,32:1-2,24-30). Tunakiita kipindi cha mababa kwa kuwa watangulizi wetu wa mwanzo walikuwa ni mababa wa imani haswa Ibrahimu.
02. Kipindi cha sheria.
Hapa ndipo swali letu lilipo;
Hapa tunamzungumzia Musa nabii mkubwa wa Bwana aliyekuwa na kazi moja kubwa ya kuwatoa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri mpaka nchi ya ahadi, ( lakini kwa bahati mbaya au nzuri yeye mwenyewe hakufanikiwa kuingia isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni pamoja na kizazi chao kipya ) agano la kale ni agano lililofungwa kati ya Mungu na watu wake,Israeli kupitia Musa likihusisha sheria zote zilizotolewa na Mungu mwenyewe. Hili ndilo agano la kale!
Musa alikuwa kama chombo cha kuwakomboa wana wa Israeli waliokuwa Misri utumwani,kwamba kwa yeye Musa watu wapokee sheria hizo na waziishi wasije kufa. Na ndio maana Kazi hii aliyoifanya Musa inafananishwa na kazi ya Bwana Yesu katika kipindi cha agano jipya,kwa maana Yesu alikuja ili kutafuta na kuokoa kilichopotea ( ushirika wa kiroho) ( Luka 10:19).
Naye Yesu ndiye mwokozi wetu,ambaye Kwake utimilifu wote wa Mungu unakaa hata sheria ya Neno lake liandikwe kwenye vibao vya mioyo yetu.
Kipindi cha sheria kilikuwa ni kigumu sana kwa sababu adhabu ilikuwa ni papo kwa papo. Yeyote atakaye kwenda kinyume na sheria aliadhibiwa mara moja. Hivyo agano la kale ni kipindi kile cha sheria alizokabidhiwa Musa. Kumbuka;Musa alipokuwa amekwea mlima Sinai ( Kutoka 19,-40) Mungu mwenyewe aliandika sheria / agano kwa chanda chake na kumkabidhi Musa. Lakini hata hivyo watu wa kipindi kile walilivunja agano hilo la kale,hawakuweza kuenda nalo ( Yeremia 31:31-34)
03. Kipindi cha ukimya takribani miaka 400.
Kabla ya kipindi cha ukimya,kulikukuwako na vipindi mbalimbali vilivyotangulia kama vile kipindi cha waamuzi na wafalme n.k lakini vipindi hivi vingine vinajumuishwa kwenye kipindi cha sheria kwa sababu waamuzi na wafalme walitembea kwenye sheria,hakukuwa na neema kipindi hicho. Na hapa kwa kuruka,tunakutana na kipindi cha ukimya baada ya nabii wa mwisho Malaki na kabla ya ujio wa agano jipya ( ujio wa Yesu). Kipindi hiki cha katikati ya nabii wa mwisho Malaki na kabla ya ujio wa Yesu kinaitwa kipindi cha ukimya kwa sababu hapakuwa na nabii,wala ujio wa malaika lakini shughuli mbalimbali ziliendelea kama kawaida na kila mmoja alifanya aliyoyaona sawa machoni mwake.
04. Kipindi cha neema – Ujio wa Yesu na agano jipya.
Kipindi hiki ni kipindi cha mwisho,ambapo Bwana Mungu kwa huruma zake,amemtuma mwanaye wa pekee ulimwenguni ili kila mtu atakaye muamini na kumpokea asipotee dhambini na kwenye hukumu ya moto wa milele bali awe na uzima wa milele ( Yohana 3:16). Ni kwa neema tu,hata Bwana MUNGU kutufikiria watu tuliohukumiwa adhabu ya mauti kwa sababu ya makosa na dhambi zetu,kwamba sasa kwa kumuamini tu Yesu na kumpokea yaani “kuokoka” tunahesabiwa haki bure. Huu ni upendeleo wa Ki-Ungu tusiohustahili kabisa katika kipindi hiki ukilinganisha na vipindi vingine hapo juu. Katika kipindi hiki ni lazima uokoke,Yesu yupo hata sasa,anaishi kwa ajili yako kumbuka yeyote asiyemuamini na kumpokea Yesu amekwisha hukumiwa!
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments