AGANO
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 17, 2019
- 3 min read
Updated: Sep 2, 2022

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Ni aina ya makubaliano ya kudumu baina ya pande mbili tofauti. Agano ni zaidi ya mkataba kwa maana mkataba una muda wake wa kuisha,bali agano hudumu katika muda usiojulikana kuisha kwake. Mbali na maagano makubwa mawili tuyajuayo ( Agano la kale na agano jipya),biblia ni kitabu kinachoeleza kwa undani kuhusu “maagano mbali mbali “ pamoja na athali zake. Kwa maana inafahamika wazi kuwa dhambi ilipoingia,ilikolofisha uhusiano/ushirika baina ya Mungu na mwanadamu. Kwa sababu ya pendo la Mungu, kwa mara ya kwanza kwenye biblia Mungu akafunga agano na Nuhu. Katika agano hili,ukweli ni kwamba watu wote walifungamanishwa nalo ( Alama yake ni upinde wa mvua -Mwanzo 9:9-11)
Hata hivyo,Kwa “pendo kuu,la ajabu ” alilonalo BWANA Mungu wetu,hakuishia hapo katika kufunga maagano na watu wake,kwa kusudi moja, “wasipotee watu wake” Yeye ndio maana huitwa ni Mungu wa maagano,Yeye,hukumbuka agano lake. Sifa pekee ya kila agano,ni kwamba pande mbili za wanaoingia agano lazima ziwepo,hata hivyo kuna siri kubwa katika agano. Mbali na agano la kale na agano jipya,bado kuna maagano mengi tunayoweza kujifunza. Agano linafungwa kati ya pande mbili;
Agano kati ya Mungu na mtu.
Agano kati ya mtu na mtu.
01.Agano kati ya Mungu na mtu
Maagano 7 makubwa katika agano la kale.
Katika maagano yaliyoandikwa kwenye kitabu cha agano la kale yanatofautiana katika wahusika,lakini Mungu Yeye ni yule yule. Watu wote waliofungamanishwa na agano, walipata neema. Haikutokana n jitihada zao binafsi,isipokuwa mkono wa Bwana ulikuwa juu yao. Hata hivyo,wao pia walionesha nia. Maagano makubwa hayo ni;
Nuhu ( Noahic covenant) – Mwanzo 9:8-17
Ibrahimu (A) ( Abrahamic covenant) – Mwanzo 15:9-21 ; Yeye Ibrahimu mwenye haki pamoja na taifa zima.
Ibrahimu (B) ( Abrahamic covenant) Mwanzo 17 yote. Abrahamu mwenyewe,kuwa baba wa mataifa mengi.
Sinai ( Sinaitic covenant)- Kutoka 19-24; Kufunuliwa kwa sheria za kwanza.
Finehasi mwana wa Eliazari ( Agano kati ya Mungu na kuhani Finehasi) – Hesabu 25:10-13
Daudi ( Davidic covenant)- 2 Samweli 7:5-17, Mungu akampaka mafuta,wa kipekee.
Agano jipya / Mungu na watu wake – Yeremia 31:31-34.
02. Agano kati ya mtu na mtu.
Watu wanaweza kuwekeana maagano wao kwa wao ,wakimuhusisha Mungu au mungu kutegemea na imani zao. Agano la aina hii ndilo linalotusumbua hata sasa,kwa maana watu wengi wapo kwenye maagano pasipo kujijua!!! Wakati mwingine hali wakijuja lakini hawajui watokeje huko kwa sasa! Biblia inatupa mfano mmoja mzuri,wa agano baina ya mtu na mtu “Labani na Yakobo ( Mwanzo 31:43-44)”.
Tabia za agano.
“Kuwepo kwa Mungu au mungu”– Mwanzo 31:50. Agano ili liwe agano kweli, lazima Mungu wa mbinguni ahusike/ awe sehemu ya agano hilo. Au watu huingia kwenye maagano na miungu,miungu yao inahusishwa.
“Kiapo ” Mwanzo 31:53
“damu ” agano linahusika sana na damu – Mwanzo 15:9-21,31:54
“Sadaka” agano huambatana na sadaka Mwanzo 31:54
“Shahidi” agano linatabia ya kuhusisha mashahidi,shahidi wa kwanza ni Mungu.,Mwanzo 31:46
“Uwajibikaji” kila aliyekuwa ndani ya agano hana budi kuwajibika kile alichokiapa.
“Athali” tabia kubwa ya agano ni kuleta athali,kizazi hata kizazi.
Agano jipya, huvunja la kale.
Agano hufutwa kwa agano, agano humalizwa kwa agano,hivyo dawa ya agano ni agano. ( Haina maana agano la kale limeangushwa na agano jipya, bali agano aliloingia mtu na mtu pamoja na miungu,dawa yake ni agano jipya la Kristo Yesu.) Yesu mjumbe wa agano jipya amefanyika upatanisho kati ya aliyefungwa na maagano ya miungu,au watu na Mungu. Kwa maana kumbuka,agano limebeba tabia gani,moja wapo ni sadaka za damu,lakini Kristo naye amelipa sadaka ya damu yake ( Mathayo 20:28).
Hivyo,ikiwa upo bado kwenye kongwa la mateso ya kimaagano ya kiukoo au familia,dawa yake ya kwanza kabisa ni kuingia kwenye agano jipya kwa kumpokea Kristo,awe Bwana na mwokozi wa maisha yako. Na kutoka hapo,badiliko utaanza kuliona. Nipigie simu sasa,tuombe pamoja.
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe.
Na kwa msaada zaidi wa MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
Whatsapp namba kwa+255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments