top of page

UMEUMBWA KWA MFANO NA SURA YA MUNGU.

Na Mch. Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi…

Hivi, unaelewa kweli msemo huo? Hivi unapoambiwa kwamba wewe uliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu, unapata picha gani katika ufahamu wako? Inawezekana kabisa mara nyingi umekuwa ukilisoma au kulisikia neno hili lakini pasipo kuelewa haswa maana yake ni nini!!

“ Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; ….” Mwanzo 1:26

Andiko hilo linatupa kujua kwamba mtu ameumbwa na Mungu wala mtu hakujiumba mwenyewe. Tena neno la Mungu linaeleza kuwa mwanadamu wa kwanza hakuwa sokwe kama wanasayansi wasemavyo leo. Neno linatuambia mtu aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Hii ndio kweli ya kwanza ya uumbaji wa mwanadamu. Lakini sasa;

Ni vyema ukajiuliza kwamba, “mfano na sura ya Mungu” ni nini hasa?. Ili uweze kuelewa vyema ni lazima ujue kwamba,kwa nini Mungu ametumia wingi wa kusema “tumfanye mtu…” Wingi huu umetumika kuonesha kwamba katika uumbaji nafsi zote tatu katika Mungu mmoja zilihusika ( yaani Mungu Baba,Neno na Roho mtakatifu – Mwanzo 1:1-3)

Bwana Mungu ni mmoja afanyaye kazi katika nafsi tatu ( 1 Yoh.5:8) Hatuna Miungu watatu bali tuna Mungu mmoja aliyeziumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyo onekana,Yeye hana mwanzo wala mwisho,ni Mtakatifu wala hakuna kama Yeye. Hivyo; Suala la uumbaji limefanywa katika nafsi zote za Mungu,nafsi ya tatu yaani Roho mtakatifu Yeye ndiye mkamilishaji wa kazi ya uumbaji naye hufanya kazi yake sambamba na nafsi ya Neno(Yesu). Hivyo basi mtu akauumbwa mwenye pande tatu yaani roho, nafsi,na mwili.

Kabla ya kujua mfano na sura ya Mungu ikoje,Je mtu ni nani basi ?

Mtu ni “roho”mwenye“ nafsi “aishiye ndani ya “mwili”. Wewe ni roho mwenye nafsi uishie ndani ya mwili. Na hii ndio maana pale mtu anapokufa, huwa tunasemaga “ mwili wa marehemu fulani, haujafika bado?” Sasa huyu mtu mwenyewe yupo wapi,maana mwili wake upo hapo! Kufa ni roho kutengana na mwili (Yakobo 2:26)

Hivyo basi, tunaposema mtu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu tuna maana ifuatayo;

01.Kwa mfano wa Mungu…

Neno “mfano” lina maana ya ulinganisho,kuwa kama sehemu ya uhalisia wa kitu kilicho halisi. Kwamba ukiambiwa “mfano wa simu hii ni kama ya mwalimu wangu” maana yake ni kwamba simu hiyo imefanana sana kama simu ya mwalimu. Hivyo neno “ mfano “ni kufanana na kile kilichopo. Sasa, Mungu amemuumba mtu kwa mfano wake yeye,hii ikiwa na maana vile jinsi Mungu alivyo ndivyo mtu alivyo maana huyo mtu amefanana sana na Mungu, “ ingawa mtu sio Mungu wala Mungu sio mtu” Bwana Mungu ni Roho mwenye nafsi tatu, mtu naye ni roho mwenye pande tatu. Huu ni mfanano mkubwa sana kaliko viumbe vyote vilivyoumbwa. Hivyo mtu amepewa kufanana na Mungu kwa maana yeye pia ni roho.

02. Kwa sura ya Mungu…

Mtu aliumbwa pia kwa sura ya Mungu,kitu ambacho hakuna kiumbe chochote kile kilichoumbwa kwa sura ya Mungu. Sura ni nini? Tafsiri nyepesi ya neno sura ni “ utambulisho”. Bwana MUNGU anautambulisho wake wa kipekee, ambao amemshirikisha mtu aliyeumbwa awe na utambulisho huo lakini bado Mungu atabaki kuwa Mungu. Utambulisho wa Mungu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu,utu wema, fadhili, uaminifu, upole pamoja na kiasi; utambulisho huu ndio sura halisi ya Mungu wetu. Biblia imeyataja haya yote katika neno moja na kuyaita hayo yote ni “tunda la Roho” – Wagalatia 5 :22

Ukweli ni kwamba mwanadamu wa kwanza aliumbiwa hayo yote,naye alikuwa mfano na sura ya Mungu kabla ya anguko. Ibilisi akitambua hayo, alimfuata mwanadamu Hawa na kumdanganya akimwambia:

“ lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Mwanzo 3:3-5

Kile ibilisi asemacho kwamba anawaambia eti wakila matunda ya mti uliokatazwa watafanana na Mungu,hali wao akina Adam na Hawa waliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Kwa lugha nyepesi walikuwa wamekwisha fanana na Mungu. Sijui kama umepata pointi hiyo ninayoilelezea hapa.

Hivyo Tunda la Roho ni tunda la Roho mtakatifu na ndio sura kamili ya Mungu wetu, ambayo mtu aliumbiwa nayo tangu awali. Leo hii ukimuona mtu ameuawa na upendo kwa Mungu na kwa watu wote,basi ujue amekuwa na sura ya Mungu katika sehemu moja ya sura ya Mungu. Lakini ukiona mtu ni muuaji,msengenyaji n.k ujue ana sura ya ibilisi sio Mungu.

Sasa jiulize wewe; Je wewe una sura ya Mungu au ya ibilisi? Upo vipi,Je tunda la Roho limeumbika kikamilifu kwako? Kama Lah? unasubiri nini kwa nini usichukue hatua sasa?

Kuokoka ndio njia ya kwanza na ya kipekee ya kurudisha mfanano na Mungu na sura yake. Kwa sababu baada ya anguko la dhambi, wanadamu wote walihesabiwa makosa na hukumu ilikuwa juu ya kila atakayezaliwa na ndivyo hali ilivyo hata sasa. Lakini kwa kuwapa Mungu ametupenda sana,amemtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo atukomboe kwa laana hiyo. Unapompokea Bwana Yesu unakuwa umefanya kitendo cha kurejesha ule mfanano na sura ya Mungu ndani yako ambayo kwa kweli ilikuwa imepotea kwa sababu ya dhambi.

Leo ingawa unapumua na kuishi bado unahitaji mfanano huo na sura ya Mungu iumbike kwako. Ikiwa haujaumbika kwa kuzaliwa kwa mara ya pili,basi ujue huna mfano na sura ya Mungu ingawa ni mwanadamu unayeishi bado. Fanya maamuzi hayo,upate tena huo mfanano na sura ya Mungu kwa maana bado hujachelewa…

Waweza sasa kunipigia simu yangu kwa msaada zaidi+255 683 877 900

Na mch. Gasper Madumla

What’s app ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comentários


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page