MWANADAMU HASA NI NANI?
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 4, 2018
- 5 min read
Updated: Sep 5, 2022

Kwa ufupi
Wewe ni nani hasa?
Bwana Yesu asifiwe…
Akitokea mtu na kukuuliza “mwanadamu ni nani hasa? ” Wewe utamjibu nini? Au ukaulizwa wewe ni nani? Sio unaitwa nani, bali wewe halisi ni nani? Wakati nimekaa na kutafakari swali hili, ilinisumbua kidogo kujitambua mimi hasa ni nani, na hapo ndipo nikagundua watu wengi hatujitambui ingawa tunaishi na maisha mengine yanaendelea kama kawa!.
Hivi tena,umeshawahi kujiuliza kwamba umekuja duniani kufanya nini? Au mbona wenzako wengi tu wamekufa na wewe hujafa mpaka sasa? “Usichukulie poa maswali haya” ni vyema ifike wakati ujihoji maswali wewe mwenyewe nami nataka nikuambie leo kwamba ukifanikiwa kujua majibu ya maswali hayo kamwe hutabaki kuwa hivyo ulivyo. Hivi unajua hivyo ulivyo sasa ni matokeo ya ufahamu wako, vile unavyoweza kufikiri. Kumbuka ;
kile unachofikiri ndicho unachoamini, hivyo kama unafikiri vibaya, utaamini vibaya pia. Unajua hilo lakini? Ndio unachoamini sasa ndicho unachofikiri, na kile unachokiri ndio matokeo ya kufikiri kwako. Hapa ndipo mtego wenyewe ulipo. Sasa mwanadamu ni nani?
Zamani fulani tulifundishwa na wahuni wa mtaani kwamba mtu akifa roho yake inapewa mnyama au mdudu, hivyo eti roho ile ile sasa inazaliwa kwa kiumbe kingine!!! Duh! Hii kali. Hivyo hatukuweza kujua mwanadamu ni nani hasa!!! Leo nimekuwa nikaona kumbe mambo mengi tunafundishwa kinyume kabisa na neno la Mungu. Na cha ajabu hata sasa kumezuka mafundisho ya kidanganyifu mengi juu ya elimu ya Mungu, kweli hizi ni nyakati za hatari sana! 🏃🏃🏃.
Nimegundua siri kubwa ya kupata ufafanuzi wa kiungu ni kwa njia ya Roho mtakatifu tu, kisha kutafakari juu ya tatizo au swali husika pamoja na huyo huyo Roho mtakatifu. Je neno la Mungu linamwelezaje mwanadamu kuwa ni nani? Awali ya yote kumbuka hili, “ Mungu ni Roho ” Yoh. 4:24a. Na ukumbuke ya kwamba, ni Mungu ndiye aliyeumba vitu vyote pamoja na mwanadamu kaumbwa na Mungu. Hivyo ni sawa na kusema Mungu ( Roho) alimuumba mwanadamu, lakini alimwuumbaje? Tunasoma hapa ;
“ Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu;… ” Mwanzo 1:26 katika andiko hili, tunagundua kwamba Mungu baba hakuwa peke yake katika zoezi zima la uumbaji, bali alikuwa pamoja na Roho mtakatifu pamoja na Neno. Hawa watatu ni umoja, huitwa nafsi tatu katika Mungu mmoja ( 1 Yohana 5:8).
Biblia inasema Mungu akamuumba mwanadamu kwa sura na kwa mfano wake. Hivyo ikiwa Yeye Mungu ni Roho na mwanadamu akaumbwa kwa “ mfano na sura yake ” hii ina maana pia mwanadamu ni roho pia, kwa maana ameumbwa kwa mfano na sura ya Roho ambaye ni Mungu. Katika kitabu cha Mwanzo, tunapewa uhalisia / chimbuko la mianzo ya kila kitu, na andiko hilo linatupa taswira ya mwanzo wa mwanadamu. Na linatuonesha dhahiri kwamba mwanadamu aliumbwa na Mungu kwa sura na mfano wake naye ni roho pia.
Ufafanuzi huu wa kina unakuonesha jinsi gani ulikuwa ukidanganywa na walimu wa sayansi wanaosema “mwanadumu katokana na sokwe” Mungu hakuumba sokwe azae mwanadamu, bali alimuumba mwanadamu. Sasa shikilia neno hili “ sura na mfano wa Mungu ” kuonesha jinsi vile Mungu alivyo ndivyo mwanadamu alivyoumbwa.
Mwanzo 1:26,inatueleza mambo ya uumbaji wa mwanadamu katika roho kwa maana mwanadamu tunamsoma kwenye Mwanzo 1:26 hana mwili, bali ni roho kama alivyo Mungu. Upo hapo? Hivyo, tumepata kujua moja ya jibu la swali hili -mwanadamu ni nani hasa? jibu la kwanza mwanadamu ni “ roho” lakini je hiyo inatosha? Hapana bado, ebu tuangalie biblia unaendeleaje kumweleza mwanadamu, tunasoma hapa tena;
“ BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.“ Mwanzo 2:7
Hapa, unaona nini? Tafakari sasa….
Jambo la kwanza linaloonekana, ni kwamba mwanadamu au mtu “kuvikwa mwili”. Biblia Mungu akamfanya mtu “kwa mvumbi ya ardhi “ neno hili limesimama kuwakilisha “mwili” kama kifuniko cha mtu mwenyewe. Mfano ; vijana wa kisasa wakinunua simu smart phone, utakuta wananunua na kava kwa ajili ya kuifunika simu.
Sasa nikuulize swali;
Je kava la simu ndio simu yenyewe? Jibu hapana. Kava ni kufunika tu simu yenyewe. Hivyo, Mungu akamvesha mtu mwili ili kwamba huyo mtu aishi kwenye mwili na kwa sababu hiyo pakawa na mpaka kati ya Mungu na mwanadamu kwamba ;
mwanadamu anapaswa amwombe Mungu, ashuke kwake kwa sababu mwili umebeba hasili ya kuchakaa, kuharibika na hapo mwanadamu ni lazima aombe sana Kwa Mungu. Lakini mwanadamu alipewa kitu tofauti na wanyama. Mungu alimweshimisha sana akampa “ nafsi, au utashi / akili” ili aweze kufanya maamuzi yake binafsi, aweze kuchagua baya au zuri.
Na ndio maana unaliona hili hata sasa, watu hukataa wokovu kurejea kwenye asili ya rohoni na matokeo yake hufanya maamuzi kuitumikia dunia 😭😭😭ni mbaya!!!
Kwa mujibu wa Mwanzo 1:26,2:7 tunaweza kuelewa sasa, mwanadamu ni nani hasa. Ukionganisha maana hizo utapata jibu hili ; “ mwanadamu ni roho mwenye nafsi aishie kwenye mwili ” hivyo wewe halisi ni “roho” umepewa akili / nafsi na umepewa kuishi kwenye mwili, na ndio maana unapokuwa msibani utasikia watu husema “ mwili wa marehemu fulani, haujafika bado ” sasa, huyo marehemu mwenye mwili yupo wapi? , maana “mwili wa marehemu fulani, huyo mwenye mwili yupo wapi? Wewe unanielewa lakini? Hii ni kuonesha kwamba yeye mwenye mwili hayupo hapo, ila mwili wake upo hapo.
Je mwili wako ni wa nani?
“ Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;” 1 Wakorintho 6:19. Kumbe 😱! Mwili wako pia si wa kwako, biblia inatuambia tumepewa tu dhamana. Mwili ulionao sasa si mali yako, ni mali ya Mungu nalo ni hekalu la Roho mtakatifu. Sasa fikiria ikiwa unalichafua hekalu la Mungu, Mungu atakufanya nini? Labda hunielewi vizuri, nikupe mfano ili unielewe vizuri.
“ Chukulia umepewa nyumba na mtu mmoja hivi, na akakuambia “rafiki ishi tu kwenye nyumba yangu, tazama; nimekupakia rangi nyeupe nzuri inayowakilisha usafi wa nyumba yangu, kila kitu nikuwekea, lakini nitakurudia na kuitaka nyumba yangu mikononi mwako” kisha huyo mtu akasafiri mbali akitaraji kurejea kwenye nyumba yake kwa muda usiojulikana. ”
Sasa fikiria hivyo, na gafla wewe ukaamua kuiharibu hiyo nyumba kwa kuifanyia mambo mengi, Je akirudi mwenye nyumba, itakuwaje? Bila shaka atakuadhibu vikali kwa kuichafua nyumba yake. Mfano huo huo ndio biblia inatueleza hapo, kwamba mwili wako, si wako bali umepewa dhamana ya kuishi tu. Je ukiuharibu mwili huo, unafikiri Mungu mwenye mwili atakufanyeje? Wewe jijibu tu mwenyewe!!!
Ebu angalia yule anayevuta sigara na kuunguza mapafu. Hajui kwamba anaunguza hekalu la Bwana,! Yule mzinzi, hajui analinajisi hekalu la Bwana! Yule mlevi, hajui analichafua hekalu la Bwana? N. K angalia wewe,! Huo mwili usilingie maana sio wako, ni wa Mungu. Wewe ni roho, na kwa sababu hiyo kuna siku utahukumiwa kwa matumizi mabaya ya mwili ulionao sasa.
Mimi nawashangaa watu ambao wanalinga kwa sababu wanafikiri ni wazuri au warembo sana hata kushindwa kujitoa kikamilifu kwa Bwana. Maskini, hawajui hiyo miili si ya kwao ni mali ya Mungu. Mimi nataka nikuambie kwamba “utatoa hesabu yake ya huo mwili wako, katika yale yute unayoyafanya sasa. Kwa sababu si wako huo mwili”
shetani anajua ufahamu huu?
Ndio, anajua ufahamu huu na ndio maana yupo bize kuwafunga watu wasije kujua haya. Na kwa sababu hiyo, watu wamefungwa wasiokoke. Hivi unajua ni nini kinachookoka kwako? Ni roho yako, ni wewe halisi ndiwe unaokoka ili makusudi urejee kwenye mahusiano mema na Mungu wako aliyekuumba kwa mfano na sura yake.
Kwa msaada zaidi, ushauri pamoja na maombezi +255 683 877 900
Na Mch. Gasper Madumla.
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
留言