BWANA ATAKUWA NA VITA NA AMALEKI KIZAZI BAADA YA KIZAZI.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 16, 2019
- 2 min read
Updated: Sep 5, 2022

Kwa ufupi,
“Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga. BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi; akasema, BWANA ameapa; BWANA atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.” Kutoka 17:13-16
Hakuna hatari kubwa kama ile ya kuwa na vita na Bwana, kwa maana mwenye vita na Bwana atakimbiliya wapi apate msaada? Ni nani atakayesimama kuwa mtetezi wake ikiwa Bwana mwenyewe kasimama kinyume naye? Kwa maana;Ukiwa na vita na mwanadamu,utakimbilia kwa Bwana. Na ukiwa na vita na shetani bado utakimbilia kwa Bwana. Je ukiwa na vita na Bwana, utakimbilia wapi? Katika kitabu cha Kutoka sura ya 17,tunaona maneno “makali” kutoka kwa Bwana mwenyewe dhidi ya “ mataifa ” kwamba atakuwa na vita nao,ataufuta ukumbusho wao. Bila shaka maswali ya kujiuliza “ kwa nini Amaleki?, wamekosea wapi? Hao akina Amaleki ndio akina nani hasa? Tunajifunza nini kisa hiki? N.K”
Amaleki ni nani?
Amaleki alikuwa ni mtesi( adui) mkubwa wa Israeli. Biblia haisemi Amaleki ametokea wapi hasa,kwa maana ni miongoni mwa taifa/kabila la kwanza la mataifa ( Hesabu 24:20).Wengine hudhani kuwa Amaleki ametokana na kizazi cha Esau ( Mwanzo 36:12,16),lakini ukifuatilia kwa umakini utagundua Amaleki alikuwepo kabla ya Esau ( Mwanzo 14:7). Kipindi cha mfalme Kedorlaoma,wakati wa Abramu kabla ya kuwa Ibrahimu,zamani hizo – Amaleki alikuwepo. Hata hivyo,inaonekana kwamba Amaleki aliendelea kuwa kwazo kwa Israeli. Israeli ilipigwa pale ilipomwacha Bwana, Amaleki na mwenzake Mkanaani walishinda ( Hesabu 14:39-45).
Hivyo,nataka umtazame Amaleki kama adui wa Israeli ( watu wa Mungu), na ndio maana hata kipindi cha Sauli aliambiwa awaangamize kabisa ( 1 Samweli 15:3).Kwa mara ya kwanza, Israeli anakutana na Amaleki baada ya kutoka Misri,Israeli akiwa amepanga Refidimu kwenye jangwa la Sinai. Lakini Israeli alishinda. Ushindi wa Israeli ulitokana na Bwana, kwa maana Bwana aliwapigania. Haikuwa vita nyepesi,bali kwa mkono wa Bwana tu,Israeli walishinda pale walipoitegemeza mikono ya Musa,kisha mpambanaji Yoshua kama kiongozi akilichapa kundi la Amaleki.
Kwa nini Bwana awe na vita na Amaleki? Akina Amaleki ni nani?
Katika mtazamo wa Amaleki kama mtesi wa Israeli, hapo ndipo Bwana asemapo atakuwa na vita naye na atamfutilia mbali ukumbusho wake. Hii ina maana; Israeli ni mtoto wa Mungu aliyenunuliwa kwa damu ya thamani,Israeli wa leo ni yeyote aliyeokoka,amehesabiwa haki bure kwa njia ya imani. Mtu wa namna hii hana tofauti na Israeli aliyeandikwa kwenye biblia. Na Amaleki ni yeyote yule anayemkwamisha Israeli. Amaleki anaweza akawa shetani na wakala wake,na ufalme wake ambao utawala wake hufanya vita dhidi ya watu wa Mungu.
Sasa,Bwana husimama kinyume na adui hao,ili kuhakikisha watoto wake wawe salama. Bwana huwapigania watu wake dhidi ya Amaleki. Hata hivyo,Amaleki aweza kuwa ni “laana,umaskini,magonjwa n.k” ambayo Bwana yeye mwenyewe ndiye mtu wa vita kinyume na hayo yote ( Kutoka 15:3,26). Moja kati ya jambo la msingi unalojifunza ni kwamba, ukiwa upande wa Mungu, umezaliwa mara ya pili,
Bwana atawaangusha Amaleki wako,naye atakuwa na vita nao siku zote.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI,
piga kwa +255 683 877 900
Whatsapp namba +255 746 446 446
Mch.G.Madumla
UBARIKIWE.
Comments