INAONEKANA NYOKA ALIKUWA RAFIKI WA KARIBU WA MWANAMKE.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 6, 2017
- 3 min read

Na Mch. Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi…
Nyoka alikuwa ndiye mnyama mwerevu kuliko wanyama wote aliowaumba Mungu. Ni sawa na kusema kwamba nyoka alikuwa zaidi ya mnyama mjanja ambaye kama anataka kukudanganya basi anaweza akacheza na akili zako na kukudanganya zaidi ya mara kumi kwa siku, pasipo kujua kama umedanganywa..
Kwa mujibu wa biblia isemavyo mwanamke alikuwa akizungumza na nyoka wakati ule ambao shetani alipokuwa akimwinda mtu. Mpango mkakati wa ibilisi ulikuwa kumwinda Adamu,na mpango huo ulianzia mbali kiasi kwamba ibilisi alifikiri namna ya kuanza kumtafuta mtu,alipopata nafasi alimtumia nyoka aliyekuwa akizungumza mara kwa mara na mwanamke kwa maana ndivyo inavyoonekana kwamba kulikuwa na urafiki mkubwa kati ya nyoka na mwanamke. Maana biblia inasema;
“ nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,…” Mwanzo 3:15
Neno hili linatupa picha ya kwamba kulikuwa na urafiki kati ya nyoka na mwanamke. Ndio maana baada ya anguko la dhambi tunaona mojawapo ya maamuzi ya Mungu ni kuweka uadui kati ya nyoka na mwanamke. Kama uadui huu umewekwa baada ya anguko la dhambi,basi ni dhahiri kabisa kulikuwa hakuna uadui uliopo kati ya nyoka na mwanamke hapo mwanzo. Ibilisi alipata nafasi kwa Hawa,akimtumia nyoka mnyama mwerevu aliyekuwa karibu kimazungumzo na Hawa. Ibilisi alipompata Hawa,basi alijua na Adamu kampata kiurahisi,na ndivyo ilivyo hata sasa;
Kwa maana ikiwa shetani anamtafuta mmoja kwenye ndoa na akiona kumkosa ujue atamtumia mwingine akianzia mbali tena kwa rafiki yake wa karibu. Mfano shetani akiwa amemkosa baba anaweza kumtafuta mama,na akiona mama naye amekaza kwa Bwana,basi atamtumia rafiki wa karibu wa mama lakini lengo lake ni kumpata baba,hivyo akifanikiwa kumkamata mama,hapo uwe na uhakika baba naye atapitikana tena kwa urahisi tu.!
Unajua katika bustani ya Mungu,nyoka anaonekana alikuwa na ukaribu sana na mwanamke,kusema hivi hakuna maana kwamba mwanamke alikuwa rafiki wa shetani!!!hapana! Nyoka hakuwa shetani,bali mnyama kama wanyama wengine ila alikuwa mwerevu sana (Mwanzo 3:1). shetani alimtumia nyoka kwa sababu ya uelevu wake na ile hali ya ukaribu na mwanamke,maana kumbuka;shetani anamtafuta mtu avuruge kusudi lake,yeye shetani ni kama simba awindaye (1 Petro 5:8).
Tunajifunza nini tunapoangalia ukaribu wa nyoka na mtu?
01. Kuwa makini sana na rafiki uliyenae kwa maana shetani ananafasi kubwa sana ya kumtumia huyo huyo ili akuangushe. Tumeshuhudia wengi wakiangushwa na marafiki zao ambao wanatumika na shetani pasipo wao kujua.
02. Ikiwa kama rafiki yako anakuambia mambo ambayo ni kinyume na mambo akuambiayo Mungu,huyo si rafiki mzuri. Na ibilisi anaweza akawa akimtumia ili uangushwe. Wapo marafiki ambao wanasema mambo yaliyo kinyume kabisa na mambo ya Mungu,mfano;badala ya kukwambia uende kanisani,wenyewe hukuambia uende disco! Hao marafiki ni kuwakimbia kama ukoma.
03. Ogopa kushea mambo yako yote kwa rafiki yako ambaye ni mjanja mjanja fulani hivi. Kwanza,ukishamuona rafiki ambaye hajatulia yaani ni mwerevu mara kumi yako! Huyo hafai,ujue kuna siku atakutumbukiza shimoni pasipo kujua. Angalau muendane na rafiki yako,lakini asiwe too much ujanja ujanja yaani kila kitu anajua yeye,kwa hiyo wewe unakuwa kama mwanafunzi wa vitu vyote. Rafiki wa namna hiyo hakufai kabisa!
04. Shetani hutumia watu werevu kukuangusha wewe. Ebu liangalie hili siku hizi; hivi unajua hata waimbaji wa kidunia wenye viwango vya juu vya uimbaji,vipaji vyao vimetoka kwa Mungu? Ndio vipaji walivyonavyo ni mali ya Mungu,lakini shetani amewatumia hao hao,badala ya vipaji vyao vitumike kumsifu na kumuabudu Mungu wao wamejikuta wakimuimbia shetani. shetani ameangalia yule ambaye amepewa kitu cha uelevu kisha akamtumia huyo,ili ampoteze kabisa! Wewe unajua haya? Au unajua vipaji walivyonavyo vimetoka kwa shetani? Hapana !! Bali asili yake ni MUNGU.
Nataka nikutazamishe hivyo kwamba uadui kati ya nyoka na mwanamke umekuja baada ya ibilisi kuleta hila zake. Hivyo inawezekana kabisa,ibilisi alijua kwamba haitawezekana kwenda kwa Adamu na kuanza udanganyifu wake labda nyoka angeumbuka!. Hakuna maana kwamba mwanamke ni mdhahifu hata kudanganywa hapana! Mwenye shida hakuwa mwanamke bali mwenye shida alikuwa mwanaume kwa sababu mwanaume alishindwa kusimamia kusudi alilopewa!
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni+255 746 446 446 .
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments