top of page

SIFA NA KUABUDU – 01

Updated: Sep 29, 2022


Karibu 70% ya ibada tunazozifanya zimetawaliwa na “sifa na kuabudu” ( Kwa maana 30% iliyobaki ni mahubiri,matangazo,maombi na maombezi,sadaka,na mengineyo). Hii ina maana kwamba sifa na kuabudu ni “ibada” na ni ibada muhimu sana kwa mwamini pamoja na kwa kwa kanisa kwa ujumla. Katika sifa na kuabudu ndipo mahali penye uwepo wa Mungu,kwa maana Yeye Mungu ndio wa kusifiwa sana ( Zb.145:3-4,135:1-2,150 yote n.k).


Lakini katika kanisa la leo, kuna shida kubwa  katika huduma hii ya sifa na kuabudu. Shida ipo katika maeneo matatu (a) Kwa wana sifa wenyewe (b) Kwa wachungaji (c)Kwa waamani.

Haya maeneo matatu hayafahamu kikamilifu ibada ya kusifu na kuabudu. Kwa mfano; ukianzia kwa kundi la kwanza ( Wana praise),wengi wao hamfahamu kikamilifu huyo Mungu wanayemsifia na kumwabudu / wamekosa Neno ndani yao. Kuimba na kupiga kweli wanafanya,lakini wanafanya nje ya ufahamu,na kwa sababu hiyo ndio tunaona matokeo mabaya ya sifa na kuabudu yanayojitokeza hivi sasa.


Ile kuendesha ibada ya kusifu na kuabudu katika “roho na kweli” inakosekana. ukirudi kuliangalia kundi la pili, (Wachungaji na viongozi wa kanisa),utagundua na wenyewe wanashida ya “mtazamo mbaya”juu ya ibada ya sifa na kuabudu. Mtazamo kama vile wao hawahusiki katika kusifu na kuabudu,isipokuwa wao wanahusika na kufundisha tu! Na ndio tunaona matokeo mabaya ya kupwaya katika sifa na kuabudu.


Na hapo ndipo utaona mchungaji/wachungaji hawapo kabisa kwenye kipindi cha sifa,badala yake mchungaji atakuja katika eneo la kufundisha/kuhubiri na akimaliza wengine huondoka na kwenda ofisini kunywa juisi! Lol… Hii ni shida,ya kimtazamo zaidi!Kwa maana mchungaji wa namna hii,hudhani kuwa yeye hausiki katika kusifu na kumwabudu Mungu,kitu ambacho hakiko sawa. Ukimalizia kwa wahusika/Waamini ndani ya kanisa,nao wanashida mno katika eneo hili,shida yao ipo katika maeneo mawili (i) Kufungwa akili wasielewe (ii) Misimamo ya dini zile za awali walikotoka. Sasa,angalia;waamini waliotoka kwenye makanisa ya kidini (si ya wokovu),


wanapokuja huku katika kanisa la kiroho,wao huja na mtazamo wa kwanza,mtazamo ule tunaouona kwenye mechi za mpira wa Simba na Yanga,ambapo mechi zinacheza uwanjani kisha mashabiki wakikaa na kuangalia,(Mashabiki wanakuwa nje ya mchezo,kazi yao kubwa ni kushangaa au kushangilia!) Hivyo shida hii inawafanya waamini kushangaa praise inapoanza mpaka kumaliza kwake,wao ni watazamaji kwa maana misingi waliyotoka nayo huko kwenye dini zao ndiyo ilivyo,kwamba Wanakwaya wanaimba kisha wao wanawatazama mwanzo mwisho.


Hivyo utagundua makundi haya matatu yakishindwa kutembea pamoja katika kusifu na kuabudu,basi hapo hakuna ibada ya kweli,na uwepo wa Bwana ni vigumu kushuka.

Kwa kuwa uwepo wa Bwana haupo,ndio tunaona sasa mchungaji akitafuta njia zake binafsi za ujanja ujanja ili kuwaaminisha watu kwamba Bwana yupo hapo,lakini kwa kweli hayupo Bwana kabisa bali ni akili zake tu ndio zinamtuma atengeneze mambo yake. Katika kanisa,ikiwa watu wataelewa vyema huduma ya sifa na kuabudu,basi hapo kutakuwa na wepesi hata kwa mchungaji katika kufundisha kwake,na miujiza itamiminika mingi,haitakuwa ya kupapasa papasa. Biblia imeeleza kwa upana sana kuhusu sifa na kuabudu,na kwa namna gani ifanyike….


ITAENDELEA…


Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900


Whatsapp namba .+255 746 446 446


Mch. G.Madumla.


UBARIKIWE.

Commentaires


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page