IBADA YA SANAMU!
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 17, 2022
- 4 min read
Updated: Aug 29, 2022

Katika agano la kale A.K,neno “ sanamu” ilimaanisha kitu chochote cha kutengenezwa na mwanadamu mfano wa jiwe au kipande cha mti wa kuchongwa au yaweza kuwa ni mnara uliosimamishwa kwa ajili ya kupokea ibada,sanamu za kusubu kwa patasi… n.k halafu vitu hivyo kulinganishwa na Mungu kwa kufanyiwa ibada ( Isaya 39:19-20).
Ukweli ni kwamba vitu hivi vilivyotengenezwa kwa mikono ya mwanadamu havina nguvu yoyote itakayoleta badiliko. Isipokuwa nguvu ya kitu ipo nyuma ya kitu hicho.
Kwa maana ibilisi na mapepo yake ndiyo yapo nyuma ya vitu vilivyofanywa kwa mikono ya mwanadamu maana yeye siku zote hutafuta kuabudiwa kwa ghalama yoyote. Ndio maana hata pale alipokutana na Yesu alitaka asujudiwe na kuabudiwa maana alimwambia Yesu ukiniangukia na kuniabudu nitakupa vyote ( Mathayo 4:9)
Lakini ni vyema ukumbuke kwamba ibilisi ujitafutia nguvu zake katika sadaka za kafara zinazotolewa katika ibada ya sanamu
Ibada ya sanamu ni machukizo makubwa kwa Mungu,tena ni dhambi
Kisa cha kwanza cha ibada ya sanamu kilifanyika huko katika Uru ya Wakaldayo katika kipindi cha mzee Tera baba wa Abramu ambaye baadae Bwana akamwita Ibrahimu jina lenye maana ya baba wa mataifa mengi.
Imeandikwa;“ …Tera,baba yake Ibrahimu,naye ni baba yake Nahori;wakaitumikia miungu mingine ” Yoshua 24:2
Na baada ya hapo tunaona watu wakiendelea na ibada za sanamu hata Taifa la Israeli lilipokuwa Misri walijichanganya nao wengine waliangamia kwa sababu ya kuifanyia ibada sanamu.
Na tena hata walipokuwa wamekwisha tolewa Misri baadhi yao waliendelea na ibada za sanamu kuonesha ibada hizo zilikuwa zimewaganda mioyoni mwao. ( Mfano tu soma Kutoka 32:1 na kuendelea )
Na ikumbukwe, kwamba wakati wa kipindi cha Waamuzi mara nyingi Israeli waliiabudu sanamu hata wakawapa adui zao kisogo nao walianguka mbele za adui zao. Lakini Kwa rehema za Bwana, Bwana aliwainulia Waamuzi mbali mbali pale walipomlilia Bwana.
Lakini pamoja na historia ya watu wa kale vile namna walivyoathiriwa na ibada za sanamu,Chakushangaza; bado hata sasa ibada za sanamu zinafanyika kwa wingi sana,Kwa maana bado hata leo kuna watu wanaendeleza ibada za mizimu,kupiga ramli, kupiga bao,kuloga,mambo ya usihiri na uchawi,ibada za kuongea na wafu , matambiko na mambo kadha wa kadha!!!
ingawa kwa namna fulani mfumo wa leo wa kuabudu sanamu wakati mwingine unatofautiana kidogo ukilinganisha na hapo mwanzo, lakini bado mambo haya yanaendelea tena kwa kasi mno! ( Sanamu nyingine za leo ni fedha,mali,watoto,mume,mke nk pale kinapochukua nafasi ndani ya moyo zaidi ya Mungu kisha kupewa heshima anayostahili Mungu pekee)
Kwa nini watu wanaabudu sanamu ?
Zipo sababu kadha wa kadha,lakini nadokoa sababu chache ambazo mimi ninazoziona kuwa ni kubwa,nazo ni;
1. Tamaa za kupata mali na utajiri wa haraka haraka!
Wakati ambapo mtu hutafuta kutoka kimaisha ni wakati mgumu,bila kutulia na Mungu waweza ukajikuta ukienda kusujudia sanamu kwa lengo la kupata mali za chap chap!!! Bila kujua au kwa kujua kwamba unachokifanya ni Ibada ya sanamu. Hivi unajua hata Sauli alipoenda kwa mwanamke mchawi wa Endori ( 1 Samweli 28:1-7) ilikuwa ni ibada ya sanamu?kwa sababu alitaka apate majibu haraka haraka ya namna atakavyowapiga watesi wake Wafilisti
Maana Bwana hakumjibu apoomba, naye akaona atafutiwe mchawi. Kumbuka pia,tamaa mbaya nayo ni ibada ya sanamu – Wakolosai 3:5
Leo wengi wameinamishwa kwa waganga na kujikuta wakifanya ibada za sanamu kwa sababu ya kutaka kutoka,akufanikiwa au kupata wanachokihitaji “ Kwa haraka “
2. Kufungwa na nguvu za giza
Kuna watu wamefungwa na mapepo kiasi kwamba hata ukimwambia aachane na ibada za ajabu ajabu hakuelewi hata kidogo! Watu wa namna hiyo sio wao kama wao,bali ni kwamba wamefungwa. Na inawezekana wakawa hawahitaji mafanikio ya haraka haraka bali wao hujisikia raha tu kwenda kupiga ramli,yaani ni vifungo vya kawaida. Wakiombewa wanafunguliwa.
3. Kushikamana na wasioamini.
Kipindi kile Israeli ilichangamana na wapagani wengi kiasi kwamba hawakuweza kumfanyia Bwana Ibada kamilifu. Lakini hata Sasa,kuna watu wamekuwa na mwingiliano mkubwa na wasioamini hivyo hawawezi kumfanyia Bwana Ibada kamilifu na hatimaye kuna wakati wanajikuta wakiyafanya mambo kama yale ya wasioamini.
Na kufanya hivyo wanajikuta wakiabudu sanamu bila kujali kwa maana wanaogopa kutengwa na jamii ya wasioamini waliochangamana nao. Mfano: cheki katika ofisi nyingi walipokuwapo wapendwa na wasioamini,na hapo kuna wakati mpendwa anajisahau kwamba yeye ameokoka na kujikuta akifanya ibada Kwa ngono, fedha au kwa namna yoyote kama wale wengine wasioamini.
4. Matokeo ya uongo wa ibada za sanamu
Kwa kuwa shetani ni mwongo,mara nyingi hujaribu kuleta matokeo chanya katika ibada za sanamu ili kuendelea kuwashika walio wake. Mfano kama kuna miungu ya uzazi,inapoabudiwa basi familia inajikuta inaweza kupata watoto, Lakini ni watoto wa kichawi!
Au kuna miungu/ sanamu za wizi Kwa wale ambao ni wezi wanaziabudu ili wakiiba wasikamatwe,miungu ya jua,mwezi, miungu ya mvua. N.K.Hivyo ibilisi aweza kutumia kuleta matokeo ya muda mfupi ili awanase zaidi na kuwatumikisha
5. Mapokeo ya mila na desturi zisizofaa.
Kuna watu ambao wanaendeleza mila zao na desturi za kuabudu sanamu. Mfano wengine bado wanatambika mpaka leo,endapo wakirejea vijijini kwao basi mambo yote ya mila za kizamani hata zile ambazo hazifai lakini itawabidi waendelee nazo maana wao ni sehemu ya ukoo.
Kuna watu wanaabudu watu kimila kabisa,yaani utakuta mzee wa ukoo lazima umwinamie kwa magoti na kumwomba baraka kisha ibada fupi na kafara zinatolewa hapo.
Na wengine ni mapokeo ya kidini kama vile kuabudu sanamu zilizochongwa kwa kile kinachoitwa picha ya Yesu au picha ya Mariamu mama yake Yesu au sanamu zao kisha mtu anakwenda kuziomba,
kuzibusu na huku akiwa amepiga magoti ya heshima na kumalizia kutoa sadaka katika picha au sanamu yenye kusadikika kuwa ni Mungu.
Kwa mujibu wa biblia inayokataza kufanya sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote Kisha ukakisujudia ni dhambi kwa maana hiyo ni moja ya ibada ya sanamu – Kutoka 20:4-5
Kwa andiko hilo linaonesha “ wivu” wa Mungu kwa miungu yote na kwa waabuduo sanamu. Hii ni sawa na kusema kwamba Mungu hawezi kuvumilia aina yoyote ya ibada ya sanamu au hawezi kuacha watu waabudu sanamu kwa sababu ni machukizo makubwa kupita maelezo yanayoweza kutolewa kibinadamu!!!
Hivyo inawezekana kabisa ukajikuta wewe upo katika ibada za sanamu ambapo ulikuwa hujui kama ulikuwapo huko. Au inawezekana kuna mtu/watu wa karibu yako wapo huko. Basi ni vyema sasa ukachukua hatua ya dhati ya kutoka huko.
Na njia pekee ya kwanza ni “Toba ” Kisha Wasiliana na mtu wa Mungu aliyekaribu nawe kwa maelekezo zaidi.
Ikiwa kama umefaidika kupata kitu,au ikiwa;
Unahitaji msaada zaidi tafadhali usisite kuwasiliana nami kwa + 255 683 877 900
What’s app number ni + 255 746 446 446
Na Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
댓글