MSAMAHA – 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 14, 2019
- 3 min read

“Msamaha / Forgiveness”
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi;
Neno “msamaha” ni neno dogo sana lakini ndilo neno linalobeba matokeo makubwa katika maisha yetu.Thamani ya msamaha ni pale mahali penye kosa/makosa (Kwa sababu maana ya msamaha inapatika panapo kosa).Msamaha una pande mbili muhimu;
Kusamehewa,( Mkosaji ajifunze namna ya kuachiliwa kutoka kwenye kosa lake)
Kusamehe (Mkosewa ajifunze namna ya kumwachilia mkosaji)
01. Kusamehewa / to be forgiven.
Awali ya yote ni vyema ukafahamu kwamba,Msamaha ni tabia ya Mungu,Yeye husamehe mno (Nehemia 9:17-20,Yoeli 2:13). Kwa sababu Mungu wetu ni mwema,haimaanishi kwamba tuendelee kumkosea,tukitegemea atatusamehe makosa yetu. Ukweli ni kwamba Mungu anautaratibu wake,ndio maana hatuwezi kukosea-kosea katika dhambi kwa makusudi tukijua tutasamehewa. Kanuni ya kusamehewa ni “toba” (Zab.32:5, Matendo 3:19) hii ikiwa na maana mkosaji yeyote hana budi kutambua kosa lake,pasipo kujihami au kujitetea kisha,atubie kosa hilo kwa yule aliyemkosea,akiomba asamehewe.
Msamaha hauongwi!
Ikiwa mkosaji atatoa hongo ya aina yoyote ili kusudi asamehewe,basi huo si msamaha sahihi. Kwa maana huwezi kumwonga Mungu ili akusamehe. Ni vyema ukalijua hili,kwa maana wapo watu ambao ili wasamehewe inawalazimu watoe chochote,wengine hudiriki hata kuonga penzi,kwa wapenzi wao ili kusudi wasamehewe kosa. Hali ikiwa hivyo,ni ubatili mtupu kwa maana anayesamehe kwa kupokea hongo,hana Mungu ndani yake (Hawezi kuwa na hofu halisi ya Mungu). Matokeo ya hongo ni uharibifu utakaoendelea siku zote! Ukweli ni kwamba unahitaji kusamehewa katika kosa ulilo nalo,lakini Je unafahamu kwamba unahitaji kufanya maamuzi ya kutokurudia tena ulichokifanya? Je upo tayari kushuka kwa toba mbele za Mungu,na yule uliyemkosea?
Wanaume ndani ya ndoa,ni vigumu kusamehewa!
Tokea enzi za Adamu hata sasa,wana ndoa ya kiume huangamizwa kwa makosa yao kwa maana hawapo tayari kushuka na kuomba toba mbele za Mungu hata kwa wake zao. Hali inatisha kwa sasa,kwa maana wanaume walio wengi huona si kitu kulia mbele za Mungu wakijutia makosa yao. Na ikiwa watu wa namna hiyo wameshindwa kujutia,basi kamwe hawawezi kuwaomba msamaha wake zao,la kama watawaomba basi haitoki moyoni,isipokuwa ili amfurahishe tu mke wake. Ebu tazama; pale Adamu alipokosa,kisha Mungu alimpa nafasi ya kutubu ili asamehewe,lakini badala yake,akaanza kujitetea na kumwona mkewe ndiye aliyekosea,Biblia inasema Mungu alipomwuuliza Adamu kuhusu kosa lake la kula tunda alilokatazwa,Adamu akasema “ huyo mwanamke uliyenipa,ndiye aliyenipa nami nikala,” Mwanzo 3:12
Yaani,ni kama vile anasema “tatizo sio mimi,bali tatizo ni huyo mwanamke uliyemleta”. Kwa hali hii,ya kujitetea hata kushindwa kuomba toba,ndio inayowaangamiza wanaume wengi ndani ya ndoa,Hivyo matokeo yake wanaume wamejikuta wakitembea kwenye makosa yasiyoisha hali makanisani wanaenda. Unajua wengi wa wanaume hawawezi kuomba msamaha kwa wake zao,kwa sababu labda ya nafasi zao,hii ni mbaya!!! Wewe usiwe hivyo,pale unapogundua kwamba umemkosea mkeo,au mwenzako,mara moja inuka ukaombe msamaha. Jifunze kuomba msamaha kuanzia leo.
Msamaha urejesha uhusiano.
Makosa au dhambi ndio adui wa kwanza anayevunja mahusiano yetu na Mungu. Kwa maana pale unapotenda dhambi unajitenga mwenyewe mbali na uwepo wa Mungu ( ingawa bado pendo la Mungu lipo juu yako). Hivyo,msamaha ni lazima ili kurejesha uhusiano wako na Mungu. Hali hii,ndivyo ilivyo hata sasa,kwa maana pale makosa yanapoonekana kati yako na mwingine,ujue hapo ndipo uhusiano wako na huyo ndugu ndipo unapopotea. Hivi unajua hata kwa wanandoa wengi leo hii,ingawa wanaishi pamoja lakini hawana uhusiano mzuri? Unafikiri ni kwa nini? Ukichunguza sana,utagundua ni kwa sababu ya “ makosa yasiyotubiwa/yasiyosawazishwa” (Ni lazima mmoja kati yao atakuwa na shida,hataki kushuka na kuomba msamaha kwa dhati)
Nifanyeje ikiwa ninaomba nisamehewe,lakini mwenzangu hataki?
Kwa Mungu,kila anayetambua kosa lake akiomba toba huku akiamua kuacha makosa hayo,akaomba toba kwa njia ya damu ya Yesu husamehewa makosa yake (1 Yoh.1:9). Na ukiwa umemkosea mwenzako katika kosa la aina yoyote ile, kisha ukajitahidi kutafuta suluhu kwa njia ya kuomba msamaha kwa dhati kabisa. Ujue kwa kitendo hicho,Mungu anaona “nia yako ya ndani” naye atakusamehe. Lakini mwanadamu akikataa kukusamehe,ujue kazi yako wewe umemaliza isipokuwa utakuwa umempalia makaa ya moto huyo aliyeshindwa kusamehe. Kwa sababu Mungu ndiye atakayeshughulika naye,na si wewe!!! Jambo la pekee utakalohitajika kufanya ni kumwombea,pili tafuta mtu mwenye Roho wa Mungu ndani yake,akaye chini naye ili msuluhishwe pamoja.
Je unastahili kusamehewa?
“Hapana! ” Haustahili kusamehewa hata kidogo bali lile unalostahili kupata ni hukumu juu ya makosa yako kwa maana mtu hulipwa sawa sawa na kazi aliyoifanya. Ujue kwamba mshahara wa dhambi ni “mauti” Warumi 6:23. Ukitambua hilo,basi ni vibaya kulazimisha usamehewe. Kwa maana suala la kusamehewa si la kwako,ni la yule uliyemkosa!!! Katika kusamehewa,pendo la Mungu linahitajika kwa sababu hakuna msamaha nje ya pendo. Ukijua kwamba kinachokufanya kusamehewa sio maneno yako mazuri au uzuri ulio nao,bali ni “pendo la Mungu” ambalo limemiminwa,basi hapo hakutakuwa na namna yoyote ya kulazimisha kusamehewa…
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
Whatsapp +255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments